Ubinafsi unamaliza maliasili Tanzania

Daniel Mbega

MACHI 23, 2016 vyombo vya ulinzi na usalama katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) vilifanikiwa kuwanasa wafanyabiashara wawili ndugu, raia wa Uholanzi wakiwa katika harakati ya kusafirisha wanyama hai 61, aina ya Tumbili (velvety monkeys) kuelekea nchini Armenia.

Raia hao wa Uholanzi, Arten Vardanian (52) aliyekuwa na hati ya kusafiria yenye namba NWF8CKJR8 na Edward Vardanian (46) aliyekuwa na hati ya kusafiria namba NY969P96, walikamatwa saa 1:30 usiku kwenye uwanja huo wakiwa na wanyama hao waliowekwa kwenye makasha maalum sita, ambapo walikuwa wasafirishwe na ndege maalumu ya mizigo yenye namba EW/364G iliyosajiliwa nchini Belarus kupitia kampuni ya Arusha Freight Limited ya jijini Arusha.

Ingawa Machi 24, 2016 serikali kupitia kwa Waziri wa Maliasili na Utalii Prof. Jumanne Maghembe, iliamua kuchukua hatua kwa kumsimamisha kazi Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Wanyamapori wa Matumizi Endelevu, Dk. Charles Mulokozi kwa kosa la kukaidi agizo la kusaini vibali vya kusafirisha Wanyamapori nje ya nchi, lakini tatizo bado ni sugu.

FikraPevu inatambua kwamba, kwa mujibu wa maelezo ya Waziri Maghembe, Dk. Mulokozi ndiye aliyesaini vibali hivyo na kwamba Waholanzi hao pamoja na washirika wao hapa nchini walikuwa katika harakati za kukamata tumbili 450.

“Nikiwa Moshi katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa nilimuita Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Wanyamapori Matumizi Endelevu, Dk Charles Mulokozi na kumuarifu juu ya kamata kamata hiyo na kumuagiza kutotoa kibali cha kusafirisha wanyama ili tuwakamate watu hao, lakini baadaye tukagundua yeye ndio amesaini kibali hicho kutoka Dar es Salaam,” alisema Profesa Maghembe wakati akitangaza kumsimamisha kazi Dk. Mulokozi.

Profesa Maghembe alitangaza pia kumsimamisha kazi Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu nchini (TFS) Juma Mgoo pamoja na wakurugenzi wawili wa taasisi hiyo ili kupisha uchunguzi kutokana na mwenendo usioridhisha wa ukusanyaji wa maduhuri ya Serikali na usimamizi mbovu wa rasilimali za misitu nchini.

Wakurugenzi waliosimamishwa ni Mkurugenzi Rasilimali Misitu, Zawadi Mbwambo pamoja na Kaimu Mkurugenzi wa Mipango na Matumizi endelevu ya Misitu, Nurdin Chamuya, ambao nafasi zao sasa zinakamiwa na Gerald Kamwendo na Mwanaidi Kijazi.

Hao nao pamoja na wakuu wa kanda wanakabiliwa na kashfa ya kukamatwa kwa shehena kubwa za magogo aina ya mninga katika Mkoa wa Rukwa wilayani

Kalambo yakiwa yamekatwa na kuwekwa ndani ya makontena ndani ya msitu pamoja na kutengenezewa nyaraka feki zinazoonyesha magogo hayo yanatoka nchini Zambia tayari kwa kusafirishwa kupelekwa China.

Licha ya kuagiza magogo hayo yapelekwe Matai katika makao makuu ya wilaya hiyo, lakini inadaiwa kwamba yalimwagiwa petroli na kuchomwa moto.

Kukamatwa kwa watu hao ni mwendelezo tu wa madudu yanayofanyika ndani ya Wizara ya Maliasili na Utalii ambako vigogo wa wizara hiyo wameigeuza kuwa ‘shamba la bibi’ lisilo na mwangalizi.

Nakumbuka wakati fulani, mbunge wa zamani wa Jimbo la Monduli, mkoani Arusha, Luteni Kanali (mstaafu) Lepilall Kimani Naityamieng’ishu ole Molloimet aliwahi kusema kwamba tangu Baba wa Taifa, Malimu Julius Nyerere alipoondoka madarakani, sekta ya maliasili na utalii ndiyo imegeuzwa na vigogo wengi kama sehemu ya kujichumia mali watakavyo.

“Utajiri wa wanyamapori ni sawa na petrol, ikiungua hakuna mbadala. Wanyama wakiisha wa kulaumiwa ni viongozi wa sasa. Maliasili inatoweka kwa sababu watu wana chuki na wanyama na wana ubinafsi mno.

"Nina ushahidi. Aina nyingi za wanyama zimeanza kutoweka hivi sasa. Kwa mfano aina ya swala-twiga, swala-pala (impala), duma, tandala wadogo na wakubwa na tongo,” alipata kusema Molloimet.

Maliasili ni janga

Siyo siri kwamba, Wizara ya Maliasili na Utalii, ambayo ina dhamana ya kulinda rasilimali zetu hasa wanyamapori na misitu, imeoza licha ya kuongozwa na wataalamu wengi.

Hakuna waziri aliyepitia wizara hiyo ambaye hakuwahi kukumbwa na kashfa, tena kubwa zinazohusisha kutoweka kwa rasilimali hizo ambazo zinapaswa kuwanufaisha Watanzania wote.

Wengine wameshindwa kuiongoza wizara hiyo kwa sababu ya kukutana na vigingi kutoka kwa watendaji wa idara mbalimbali, baadhi yao wakijivunia ‘mtandao’ walionao na vigogo wa juu wa serikali, ambao inawezekana walikuwa wakiwalea licha ya kufisidi maliasili za taifa.

Kumbukumbu zilizopo zinaonyesha kwamba, wakati akiongoza wizara hiyo, Waziri wa sasa Profesa Maghembe, alizidiwa na kashfa za kushindwa kusimamia vyema uuzwaji wa vitalu na uvunaji wa miti, hivyo akadumu kwa kipindi cha mwaka mmoja tu kati ya 2007-2008.

Mtangulizi wake, Dk. Anthony Mwandu Diallo, ambaye alianza tangu mwaka 2005, aliingia katika mvutano mkubwa na Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Emmanuel Severe kutokana na suala la ukodishaji wa vitalu vya uwindaji na juhudi zake za kutaka mkurugenzi huyo aondoke ziligonga mwamba, kwani badala yake ni yeye aliyeondoka mwaka 2007.

Shamsa Selengia Mwangunga, ambaye aliingia mwaka 2008 katika baraza jipya la mawaziri tangu kujiuzuru kwa Waziri Mkuu Edward Lowassa, naye alikumbwa na kashfa nyingi.

Kwanza lilikuwa ni suala la kuongeza muda wa umiliki wa vitalu vya uwindaji bila kufuata sheria. Aliwaongezea wamiliki hao muda wa miaka mitatu kinyume cha Azimio la Bunge la kuzuia kuongezwa kwa muda wa umiliki wa vitalu ili utaratibu mpya uandaliwe.

Lakini baadaye likaja suala la mgogoro wa Loliondo, ambapo wananchi wa jamii ya Wamasai walichomewa nyumba zao na kufukuzwa kwa nguvu kwa madai ni wavamizi wa eneo la mwekezaji.

Bahati mbaya zaidi ni kwamba, Waziri Mwangunga akatamka kuwa waliofukuzwa na kuchomewa nyumba zao ni Wamasai kutoka Kenya, siyo Watanzania!

Hata kama wangekuwa wametoka katika Sayari ya Mars, sidhani kama utaratibu wa kuwachomea nyumba na kuwafukuza kinyama ulikuwa sahihi.

Ndiyo maana wanaharakati walisema kwamba, hilo lilikuwa shinikizo la wawekezaji wenye fedha ambao waliwafanya watendaji wa serikali wakiuke hata haki za binadamu.

Mrithi wake Mwangunga, Ezekiel Maige, ambaye kabla alikuwa naibu waziri, yeye alidumu kwa miaka miwili kabla ya kuingia kwenye skendo ya kuuza wanyamapori hai kiholela.

Ndicho kipindi ambacho twiga pamoja na wanyamapori wengine walisafirishwa kwenye ndege kupitia Uwanja nwa Ndege wa Kilimanjaro, ambao umekuwa ‘salama’ zaidi kwa majahili wanaohusishwa na usafirishaji wa wanyamapori kinyume cha sheria.

Kashfa ile iliwazoa vigogo wengi katika wizara hiyo kama ilivyotokea katika kashfa ya kupopolewa kwa faru.

Balozi Khamis Kagasheki alikuwa mchapakazi makini. Aliyeuliwa kushika wadhifa huo mwaka 2012. Kagasheki alipata msukosuko wa kwanza wa kisiasa baada ya kutangaza eneo hilo la kilomita 1,500 la Loliondo kuwa ni pori tengefu na wananchi kuachiwa kilomita 2,500. Agizo lake lilitenguliwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

Katika hali ya kushangaza wakati akipambana na tatizo la ujangili, akafanyiwa mizengwe kwa kuhusishwa na Oparesheni Tokomeza Ujangili ambayo inadaiwa ilikiuka haki za binadamu.

Hata hivyo, taarifa zinaeleza kwamba, mizengwe aliyofanyiwa ilitokana na ‘kuingilia maslahi ya wakubwa’ kwa sababu suala la ujangili linawahusisha vigogo wengi nchini.

Katika hali ya kawaida tu, ni vigumu kwa mwananchi wa kawaida kujaza meno ya tembo kwenye kontena, akalipeleka bandari na kulisafirisha bila kuwepo na mtandao wa wakubwa.

Hivi kontena hilo linapitaje kwenye bandari zetu halafu likifika Vietnam au Hong Kong likashindwa kupita?

Msaidizi wa Balozi Kagasheki, Lazaro Nyalandu, ndiye aliyekabidhiwa mikoba na akaanza kwa kasi ya ajabu kwa kuwaondoa vigogo wa wanyamapori, Mkurugenzi Alexander Songorwa na msaidizi wake Jaffer Kidegesho kama njia ya kutekeleza Azimio la Bunge na kusafisha ufisadi, duru zikageuzwa na kuwa ubaya.

Kelele zikasikika kuwa, kitendo cha kuwasimamisha watumishi hao ilikuwa ni njia ya kujisafishia ulaji rahisi, kwamba amewatoa wachapakazi ili iwe rahisi kwake kujisevia maliasili.

Kwa kuwa chemichemi ya maji machungu haiwezi kutoa maji matamu, Katibu mkuu wa wizara hiyo Maimuna Tarishi aliibuka, sijui kwa kutumwa na nani, akawarejesha vigogo waliofukuzwa na Nyalandu, huku Katibu Mkuu Kiongozi (mstaafu) Ombeni Sefue akimfedhehesha waziri huyo kwa kumwambia hakufuata sheria, kanuni na taratibu za kumfukuza mtu kazi.

Ingawa aliendelea katika wizara hiyo hadi serikali ya awamu ya nne ilipoondoka madarakani, lakini tayari Nyalandu alikuwa ameingia katika orodha ya mawaziri waliopwaya kwenye wizara hiyo.

Waziri pekee aliyekaa kwenye wizara hiyo kwa muda mrefu ni Zakhia Meghji, ambaye alidumu kwa miaka saba tangu mwaka 1997 hadi 2005, lakini naye alikumbwa na kashfa kadhaa kama usafirishaji wa magogo kwenda China pamoja na uuzwaji wa Hoteli ya Kilimanjaro.

Arcado Ntagazwa aliiongoza wizara hizo kati ya mwaka 1988-1990, lakini akalaumiwa sana kwa ufisadi kwamba alibinafsisha hoteli za kitalii kiholela na kwa bei ya kutupa zikiwemo Lake Manyara, Ngorongoro, Seronera, Lobo, Mount Meru na Mikumi.

Ntagazwa hakurudi kwenye wizara hiyo baada ya uchaguzi wa mwaka 1990, akaingia Abubakari Yussuf Mgumia, 1990-1993, lakini akaambiwa ameshindwa kudhibiti uharibifu mkubwa wa misitu kutokana na kushamiri kwa biashara ya mbao. Katika kipindi cha uongozi wake ndipo Shirika la Utalii Tanzania (TTC) lilibadilishwa na kuwa Bodi ya Utalii.

Mgumia akampisha Juma Hamad Omar (sasa Mbunge wa CUF). Huyu akakumbwa na kashfa nzito kupata kutokea ya kuliuza Pori la Loliondo kwa Mwana Mfalme wa Saudia.

Kashfa hiyo ni kati ya matukio makubwa yaliyotikisa nchi kwani ilisababisha kuundwa kwa Kamati ya Bunge iliyoongozwa na Mateo Qaresi na chanzo cha kuondolewa kwa Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori wakati huo, Muhidin Ndolanga. Omar aliondoka katika wizara hiyo mwaka 1995 baada ya Rais Mkapa kuingia madarakani.

Juhudi za kumlinda lizifanyika hadi baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 1995, ambapo nafasi hiyo akapewa Dk. Juma Ngasongwa, lakini naye hakufaa. Biashara ya uuzaji wa minofu ya samaki nje ya nchi bila kulipa kodi ikamwondoa. Kamati iliyoundwa chini ya Mbunge wa zamani wa Ilala, Iddi Simba ilifichua madudu katika biashara hiyo.

Kwa hiyo utaona kwamba, kuna matatizo makubwa kwenye wizara hiyo yenye dhamana ya kulinda misitu na wanyamapori, na haijajulikana tiba ya uhakika itapatikana lini kwa sababu watendaji na wataalamu, ambao mara nyingi hupandishwa tu vyeo. ndio wachezaji wakubwa katika kuhujumu maliasili hizo.

Wacha tusubiri miujiza.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *