TANZANIA imejaliwa ardhi nzuri yenye rutuba inayokuza mamia ya aina mbalimbali za nafaka, matunda, mbogamboga, viungo vya vyakula na mazao mengine ya biashara.
FikraPevu inatambua kwamba, asilimia kubwa ya wakulima wanafanya kilimo kidogo huku wachache wakifanya kilimo kikubwa cha mashamba makubwa yenye zao moja tu.
Ni sekta hiyo ya kilimo inayobeba uchumi wa Tanzania ambapo uzalishaji umekuwa ukipanda na kushuka kila mwaka kulingana na hali ya hewa.
Katika msimu wa 2014/2015, uzalishaji wa mazao ya chakula ulikuwa tani 15,528,820 zikiwemo tani 8,918,999 za nafaka na tani 6,609,821 za mazao yasiyo ya nafaka.
Uchunguzi wa FikraPevu unaonyesha kwamba, uzalishaji wa mazao makuu ya biashara kwa msimu huo ulikuwa tani 915,665.9, wakati uzalishaji wa mazao ya bustani ulikuwa tani 5,931,906 huku ule wa mazao ya mbegu za mafuta ukijumuisha alizeti, ufuta, mawese, karanga na soya ukiwa tani 5,936,527.
Si hivyo tu, Tanzania pia imejaliwa mifugo ya aina nyingi na ndiyo nchi ya pili barani Afrika kuwa na mifugo mingi.
Katika mwaka 2015/2016, idadi ya mifugo nchini ilikuwa ng’ombe milioni 25.8 mbuzi milioni 17.1 na kondoo milioni 9.2, ambapo kuku wa asili walikuwa milioni 42.0, kuku wa kisasa milioni 34.5 na nguruwe milioni 2.67.
Pamoja na sifa zote hizo, FikraPevu inatambua kwamba, Tanzania imeendelea kuwa miongoni mwa nchi zinazoshika mkia katika usambazaji wa bidhaa za kilimo nje ya mipaka yake.
Wakulima wengi huzalisha mazao ya ziada yenye kutosha kuuza hadi soko la nje lakini wengi hawafahamu njia za kufuata kuweza kupata soko hilo adhimu.
Hali hiyo hufanya wajikute wakiharibikiwa mazao yao kutokana na wingi wa mizigo huku walaji wakiwa wachache.
Zipo njia nyingi za kufuata ili kumwezesha mkulima kuuza nje ya nchi.
Njia pekee iliyo rahisi ni kuanzisha ushirika wa wakulima wa aina fulani mazao, mfano, muungano wa wakulima wa machungwa, matikiti maji, mbogamboga, maparachichi, maembe, mafuta ya alizeti, mawese, uzalishaji wa asali na kadhalika.
Faida kubwa ya kuwa na muungano wa aina hiyo ni kuwasaidia wakulima katika kutimiza vigezo na masharti yaliyowekwa katika masoko ya kimataifa kwa wazalishaji, ikiwemo viwango vya ubora vilivyowekwa na nchi husika.
Muungano huo huwezesha pia kuwa na kiasi cha kutosha cha mazao kulingana na mahitaji ya nchi husika huku ukisimamia vizuri shughuli zote za uzalishaji na kuhakikisha hakuna matumizi ya kemikali mbaya.
FikraPevu inatambua kwamba, wakulima wa kahawa wa Mkoa wa Kilimanjaro walianzisha chama chao, Kilimanjaro Native Cooperative Union (KNCU) kabla ya uhuru, kama ilivyokuwa kwa Kagera na Mbeya.
Kazi ya chama hicho ni kusaidia wakulima kuzalisha kahawa iliyo bora na inayokidhi soko la kimataifa.
Baada ya uzalishaji vyama hivi huchukua kahawa kutoka kwa wakulima kulingana na mahitaji ya mzigo na kusimamia mauzo nje ya nchi, ambapo baadaye wakulima hulipwa fedha zao kupitia chama hicho.
Kwa ujumla, wakulima wanahitaji vyama kama hivyo kwa kila aina ya mazao ya kilimo yenye soko nje ya Tanzania, kama vile nyama, matunda, asali, mazao ya viungo (spices), maziwa, ngozi, nafaka, na mafuta.
Mkoa wa Tanga, mbali ya mkonge na mazao mengine, lakini unasifika kwa kilimo cha matunda, ambapo wakati wa msimu, matunda kama machungwa huwa ni mengi kiasi cha kukosa soko na kuozea shambani.
Kama kungekuwa na chama cha wakulima wa machungwa chenye dhamana ya kusimamia uzalishaji bora wenye viwango, huku kikiwa pia na jukumu la kutafuta masoko nje ya nchi, ni dhahiri wakulima wa Muheza na vijijini vinavyozunguka ikiwemo Segera wangeweza kunufaika na kilimo chao.
Vivyo hivyo kwa bidhaa nyingine za kilimo katika maeneo mbalimbali hapa nchini kama vile mafuta ya alizeti, mawese, ufuta, pamba pamoja na mazao ya bustani na ufugaji wa nyuki.
Njia nyingine rahisi ya kupata soko ni kupitia intaneti kwa kujitangaza kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii kama jamiiforums, faceook, twitter, instagram, whatsapp na mingineyo ambayo ina watembeleaji wengi kutoka nje ya nchi.
Ushiriki wa wakulima katika matamasha na maonyesho makubwa ya wazalishaji na wafanyabishara unawezesha pia upatikanaji wa masoko nje ya Tanzania.
Maonyesho kama ya wakulima (Nane Nane), maonyesho ya wenye viwanda, maonyesho ya biashara ya kimataifa ya Saba Saba na mengineyo, serikali hualika wadau mbalimbali kutoka nje ya nchi kuhudhuria, jambo ambalo ni fursa muhimu kuwakutanisha wakulima kutoka ndani na nje.
Pia yapo matamasha mbalimbali ya biashara nje ya Tanzania ambayo ni muhimu kwa mkulima kuhudhuria na kuwasaidia wakulima wetu kupata masoko ughaibuni.
Utafiti wa kina pia unahitajika katika kupata soko la muda mrefu na la uhakika.
Ni vizuri kujua soka unalotaka kwenda kuuzia bidhaa zako, ubora wa bidhaa zako, uzalishaji wake, mahitaji ya soko na mambo mengine kadha wa kadha.
Kwa mfano, unataka kuuza matikiti maji nchini Denmark lakini huko pia kuna wakulima wanaozalisha zao hilo na kwa ubora wanaoufahamu, hivyo itakuwa vigumu kwako kushindana labda kama bidhaa zako zitakuwa zimewazidi viwango.
Lakini pia lazima ujue sheria za nchi husika, maana nchi kama Denmark ina utaratibu wa kulinda wazalishaji wa ndani.
Gaotsenelwele Ontwetse ni raia wa Botswana anayesoma nchini Tanzania, katika mahojiano na FikraPevu anakiri kuwa nchini mwake kuna fursa kubwa kwa wakulima wa matunda kutoka Tanzania kwani wao hawazalishi maembe, ndizi, matikiti maji, na mananasi, lakini bidhaa hizo hazipelekwi huko.
Soko kubwa la bidhaa za kilimo kwa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara ni Ulaya, Arabuni pamoja na Marekani ya Kaskazini.
Kwa mujibu wa uchunguzi wa FikraPevu, katika nchi za Arabuni kuna uhitaji mkubwa wa matunda ya kitropiki kama mananasi, maembe, matikiti maji, ndizi, maparachichi, machungwa, malimao, mapera pamoja na mazao ya viungo hasa vitunguu maji na swaumu, karafuu, pilipili, iliki, tangawizi na bidhaa za wanyama kama maziwa na jibini.
Nchi za Ulaya zina uhitaji mkubwa wa mboga za majani aina mbalimbali zinazozalishwa barani Afrika, uhitaji wa mafuta ya mimea kama alizeti, ufuta na mawese, lakini pia wanahitaji sana nyama, asali, nta, maua na baadhi ya matunda ya kitropiki.
Umoja wa Ulaya (EU) ndicho chombo kikuu chenye jukumu la kusuimamia uingizaji mazao ya chakula barani humo, ambapo wao ni waagizaji na wasambazaji wakubwa wa chakula duniani kote.
Jukumu la EU ni kuhakikisha kwamba, bidhaa zote za chakula zinazoingia huko lazima ziwe zimekidhi vigezo na zina ubora unatakiwa ili kulinda afya za walaji wa mwisho, ndiyo sababu imeweka sheria kali za uzalishaji unaozingatia vigezo hivyo.
Katika kuwalinda wazalishaji wa ndani dhidi ya ushindani kuna sheria pia zimewekwa kama vile kutoza kodi kubwa kwa bidhaa zinazoingizwa.
Katika kukwepa hilo wazalishaji wa Tanzania wanatakiwa kufanya utafiti ili kupeleke bidhaa katika nchi ambazo hazina uzalishaji wa bidhaa husika, hali ambayo itafanya kodi kuwa nafuu na kuwepo kwa wigo mpana wa soko.
Kwa upande wa nchi za Arabuni, lazima bidhaa za kilimo zinazoingizwa ziwe zinakidhi vigezo vya Imani ya dini ya Kiislamu (Halal).
Pia ubora mkubwa katika uzalishaji unahitajika ikiwemo uandaaji uwe unakidhi vigezo vya kimataifa, kutotumia kemikali zenye sumu, na kadhalila.
Sheria za Marekani hazina tofauti na zile za Ulaya ambapo zina masharti magumu kwa bidhaa zinazoingizwa kutoka nje.
Kwa mfano, nyama inayoingizwa huko lazima ifanyiwe ukaguzi wa kina na mamlaka zinazotambulika.
Ukaguzi huo ni pamoja na hali ya kiafya ya mnyama kabla ya kuchinjwa, machinjio ya kisasa inayokidhi vigezo vya kimataifa, lakini pia wameweka vikwazo kwa nchi ambazo ziliwahi kuzuka magonjwa mbalimbali ya mifugo.
Serikali ya Tanzania imejitahidi kuwawezesha wakulima wake, kwani vibali vya usafirishaji wa mazao ya chakula nje ya nchi hutolewa kupitia Wizara ya Kilimo bila gharama yoyote.
Uuzaji wa mazao hayo ya kilimo unasimamiwa na Sheria ya Usalama wa Chakula (Nafaka na mazao mchanganyiko) ya mwaka 2009, inayompa mamlaka Waziri wa Kilimo kutoa vibali kwa mtu yeyote aliyekidhi vigezo vinavyohitajika.
Sheria hiyo inamtaka pia mkulima au chama cha wakulima kuorodhesha kiwango na aina ya mazao ili serikali ipate takwimu halisi ya bidhaa za kilimo zilizosafirishwa nje ya nchi.
Mkulima anatakiwa awe na cheti cha ubora wa kimataifa wa mazao anayosafirisha kwa mujibu wa Sheria ya Ubora wa Mazao ya mwaka 1977.
Aidha, mkulima anatakiwa kuwa na cheti cha biashara, cheti cha mlipa kodi na utambulisho maalumu kutoka wilaya husika.
Tayari serikali imeonyesha jitihada kwa kuongeza idadi ya ndege za mizigo zinazokwenda nje ya nchi hali ambayo imeanza kusaidia baadhi ya wakulima wa matunda kama vile maembe na maparachichi ambao wanasafirisha nje japo kiwango chake bado kiko chini.
Wakulima wakichangamkia fursa hiyo ni dhahiri kilimo kitasadifu dhana halisi ya ‘uti wa mgongo wa taifa’.