Uboreshaji wa sheria, elimu kwa wananchi kupunguza ajali barabarani

Jamii Africa

Serikali imetakiwa kuzifanyia marekebisho sheria na kanuni zinazosimamia usalama barabarani ili kuokoa vifo vinavyozuilika na kukuza uchumi wa taifa.

Sheria ya Usalama Barabarani ya mwaka 1973 ni sheria inayoongoza shughuli zote za barabarani ambapo katika utekelezaji wake zinatoa mwanya wa kutokea kwa ajali na kugharimu maisha ya watu.

Maeneo ambayo yanapaswa kufanyiwa marekebisho ni mwendo kasi, ulevi wakati wa uendeshaji, uvaaji wa kofia ngumu, kufunga mikanda na vizuizi kwa watoto.

Hali ya  Usalama Barabarani Duniani

Kwa mujibu wa takwimu za Kikosi Cha Usalama Barabarani nchini zinaeleza kuwa kuanzia Januari hadi Julai 2016, watu 1,580 wamekufa kutokana na ajali za barabarani, wengine 4,659 walijeruliwa katika ajali 5,152 zilizotokea nchi nzima. Kwa upande wa pikipiki waliokufa walikuwa 430,, waliojeruliwa 1,147 katika ajali 1,356.

Ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO-2017) juu ya Ajali za Barabarani zinaonyesha kuwa watu milioni 1.25 hufariki  kila mwaka ambapo watu milioni 20 hadi milioni 50 hubaki na majeraha na ulemavu wa aina mbalimbali.  Asilimia 90 ya ajali zote za barabarani hutokea katika nchi zinazoendelea likiwemo bara la Afrika ambapo nchi hizo zina 54% ya magari yote yaliyopo duniani.

Nusu ya wanaokufa katika ajali za barabarani zinazotokea duniani kote ni watembea kwa miguu, madereva wa bodaboda na madereva wa magari. Ajali hizo zinaathiri 3% ya pato la ndani la taifa kila mwaka. Bila hatua stahiki kuchukuliwa kupunguza tatizo, kufikia 2030 ajali za barabarani zitakuwa nafasi ya 7 katika kuchangia vifo vyote vinavyotokea duniani.

Pikipiki baada ya ajali

Chama Cha Wanawake Wanahabari Tanzania (TAMWA) kupitia taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa chama hicho, Edda Sanga ameeleza kuwa  wanaungana na watanzania katika wiki ya maadhimisho ya usalama barabarani ambayo yameanza leo 16 hadi 21, Oktoba 2017 ambapo  amewataka wadau kupaza sauti zao ili sheria na kanuni za usalama barabarani zifanyiwe marekebisho.

“TAMWA inawaasa wadau wa usalama barabarani kupaza sauti na kutoa wito wa kufanyiwa marekebisho ya sheria na kanuni za usalama barabarani hasa ‘Sheria ya Usalama Barabarani ya mwaka 1973’” inaeleza ripoti hiyo na kuongeza kuwa,

“Mfano Sheria ya usalama barabarani ya 1973 Kifungu cha 51 (8) inatambua maeneo machache katika kuzuia mwendokasi, ni muhimu sheria itamke maeneo yote na si yale ya mjini tu au makazi, itamke wazi kuhusu maeneo ya shule, nyumba za ibada, maeneo ya michezo na mbuga za wanyama”.

Kutokana na  kutotekelezwa kikamilifu kwa sheria za usalama barabarani kumechangia ongezeko kubwa la ajali na kusababisha vifo, ulemavu na kupungua kwa nguvu kazi ya taifa na kuwataka wadau kuchukua hatua za haraka kuokoa maisha ya wananchi.

“ TAMWA inaona kuna umuhimu wa kuchukulia hambo hili kama dharura kwa kuzifanyia marekebisho sheria na kanuni za usalama barabarani ili kuipa nguvu sheria hiyo kuwadhibiti wanaokiuka matumizisahihi ya barabara.

Pia kifungu cha 45 cha Sheria hiyo kinakataza mtu kuendesha gari akiwa amekunywa pombe zaidi ya kipimo ambacho ni 0.08g/dl. Kiwango hicho kinachotumika katika nchi yetu ni kikubwa ikilinganishwa na kiwango ambacho kimewekwa kimataifa ni 0.05g/dl kwa dereva mzoefu na 0.02g/dl kwa dereva asiye na uzoefu.

Mgongano mwingine wa sheria hiyo ni kuwataka madereva wa pikipiki za magurudumu mawili na matatu kuvaa kofia ngumu  muda wote wanapoendesha chombo hicho. Sheria haitambui uvaaji wa kofia ngumu kwa abiria wa chombo hicho.

Takribani watanzania 4,000 hufariki kila mwaka kutokana na ajali barabarani ambazo kwa sehemu kubwa husababishwa na kutozingatiwa  kwa sheria zinazosimamia matumizi sahihi ya barabarani.

Kwa nyakati tofauti Jeshi la Polisi limekuwa likitoa elimu kwa wananchi juu ya ufungaji wa mikanda kwenye magari ili kujikinga na madhara ambayo yanaweza kutokea gari likipata ajali. Lakini bado suala hilo la kufunga mikanda halijazingatiwi kikamilifu na madereva na abiria.

Hali hiyo inaweza kuwa ni matokeo ya Sheria ya Usalama Barabarani kifungu 39 (1) kumtaka dereva na abiria wa kiti cha mbele kufunga mkanda muda wote. Sheria haijatamka  chochote kuhusu abiria wa nyuma pamoja na watoto. 

Pia sheria haijamhakikishia mtoto ulinzi akiwa kwenye gari ikizingatiwa kuwa watoto bado hawana uwezo kufanya maamuzi sahihi mpaka waongozwe na watu wazima.

“Kuhusu vizuizi kwa watoto Sheria ya Usalama barabarani  haijatamka chochote juu ya suala la vizuizi kwa watoto. Hivyo basi mtoto hana ulinzi wowote akiwa kwenye chombo cha usafiri” inaeleza ripoti hiyo.

Wiki ya Usalama Barabarani imezinduliwa leo kitaifa mkoani Kilimanjaro ikienda sambamba na kauli mbiu “ Zuia Ajali, Tii Sheria, Okoa Maisha” na itaendelea mpaka tarehe 21 Oktoba2017.

Maadhimisho hayo yataambatana na shughuli mbalimbali ikiwemo kutoa elimu kwa madereva na wananchi juu ya matumizi sahihi ya barabara ili kuokoa maisha ya watu na kuongeza nguvu kazi ya taifa katika uzalishaji.

Watu walio katika hatari ya kupata ajali

Inaelezwa kuwa wananchi wanaoishi katika nchi maskini kama Tanzania ambazo zinakabiliwa na ubovu wa barabara na usimamizi mdogo wa sheria wako katika hatari ya kupatwa na ajali na kuwasababishia majeraha na kifo.

Vijana ambao ni watumiaji wakubwa wa barabara nao wanatajwa kuwepo katika kundi hilo ikizingatiwa kuwa 48% ya watu wote wanaokufa kwa ajali duniani wako katika umri wa miaka 15 na 44.

Vijana wa kiume wana uwezekano mara 3 zaidi wa kukumbana na matukio ya ajali za barabarani kuliko wasichana. Karibu robo tatu (73%) ya ajali za barabarani huusisha vijana wa kiume wenye umri wa chini ya miaka 25.

Vifo hivyo vinawakuta vijana wengi wa kiume kwasababu wao ndio wanaendesha vyombo vya usafiri kuliko kundi lolote na wanakabiliwa na kutozingatia sheria za usalama barabarani.

 

 

 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *