WABUNGE wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mkoani Mwanza, Highness Kiwia (Ilemela), na Salvatori Machemli (Ukerewe), wamenusurika kuuawa baada ya kuvamiwa na watu wanaosadikiwa kuwa ni wafuasi wa CCM kisha kukatwa
mapanga sehemu mbali mbali za miili yao, ambapo Mbunge Kiwia inadaiwa hali yake ni mbaya sana.
Mbali na wabunge hao kujeruhiwa vibaya, pia mbunge wa Jimbo la Nyamagana jijini hapa, Ezekiel Wenje (Chadema), naye inadaiwa amenusurika kipigo pamoja na kukatwa mapanga na wafuasi hao wa CCM, huku wafuasi wengine watano wa Chadema wakijeruhiwa vibaya katika tukio hilo la aina yake ambalo limelaaniwa vikali na wananchi wa mkoa wa Mwanza na taifa kwa ujumla.
Tukio hilo limetokea majira ya saa 7 usiku wa kuamkia leo, ambapo wabunge hao wakidaiwa walikuwa wakiwasambaza mawakala wa chama chao kwenda majumbani kwa ajili ya kujiandaa kwenda kusimamia kura za mgombea wa Chadema Kata ya Kirumba, Dany Kahungu katika uchaguzi mdogo uliofanyika jana.
Taarifa zaidi zinadai kwamba, wabunge hao walikutwa na wafuasi wa CCM wakiwa wanatoa rushwa nyumba kwa nyumba, katika eneo la Ibanda Kabuholo kata hiyo ya Kirumba ambapo, jambo ambalo Jeshi la Polisi limeshindwa kuthibitisha juu ya madai ya utoaji huo wa rushwa.
Kwa mujibu wa taarifa hizo ambazo mwandishi wa habari hizi alizipata wa kuamkia jana, Mbunge wa Ilemela, Kiwia ndiye aliyeumizwa zaidi kutokana na kupata majeraha makubwa sehemu za kichwani, mgongoni pamoja na maeneo ya makalio, ambapo alikimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando (BMC), ya jijini Mwanza kwa matibabu zaidi.
Wakati Mbunge Kiwia akidaiwa kuumizwa vibaya na wafuasi hao wa CCM, taarifa zingine zinasema Mbunge wa Ukerewe, Machemli yeye alikatwa mapanga sehemu mbali mbali za mwili wake, lakini hajaumia sana.
Uongozi wa Hospitali ya Bugando umethibitisha kufikishwa na kupatiwa matibabu kwa wabunge hao pamoja na baadhi ya wafuasi wa Chadema katika hospitali hiyo, na kwamba Mbunge wa Ilemela aliondolewa haraka hospitalini hapo kwa ajili ya kupelekwa sehemu nyingine kwa matibabu zaidi.
“Kweli Mbunge wa Ilemela na yule wa Ukerewe waliletwa hapa Bugando wakiwa wamejeruhiwa vibaya sana. Lakini baada ya kupatiwa matibabu, huyo mbunge Kiwia aliondolewa haraka sana na wenzake hospitalini hapa. Hatujui walimpeleka wapi maana hiyo sasa ni mambo binafsi.
“Inawezekana huyu mbunge wa Ilemela amesafirishwa kwenda Dar es Salaam au KCMC. Lakini ni vizuri ukawasiliana na Muuguzi wa zamu ili upate ufafanuzi zaidi”, alisema Ofisa Tawala wa Hospitali ya Bugando, Joackim Wangabo.
Jitihada za kumpata muuguzi wa zamu ziligonga mwamba, baada ya kuelezwa kwamba yupo sehemu nyeti akitoa huduma kwa wagonjwa wengine. Lakini Daktari mmoja aliyekutwa mapokezi hospitalini hapo ambaye alikataa kutaja jina lake alipoulizwa alikiri kumpokea Mbunge Kiwia na watu wengine wawili akiwa amejeruhiwa vibaya kwa mapanga, na kwamba alishaondolewa hospitalini hapo na hajui kapelekwa wapi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow (RPC), aliwaambia waandishi wa habari leo kwamba: “Ni kweli wabunge hao wamevamiwa na kujeruhiwa kwa mapanga usiku, na sisi leo (jana), majira ya saa 7:20 tulipokea taarifa kuwa wafuasi wa CCM wamewateka na kuwaweka chini ya ulinzi wabunge watatu wa Chadema”.
Alisema baada ya kupata taarifa hizo, muda mfupi polisi walifanikiwa kufika eneo la tukio na kuwakuta wabunge hao ambao ni Kiwia, Wenje na Machemri wakiwa wamewekwa chini ya ulinzi na wafuasi hao wa CCM, ambapo polisi walipambana na kufanikiwa kuwaokoa.
“Mbunge Kiwia alikuwa amejeruhiwa kichwani na kukimbizwa katika hospitali ya Rufaa ya Bugango kwa ajili ya matibabu. Majeruhi wengine ni pamoja na dereva wa mbunge wa Ukerewe jina hatujalipata yeye amejeruhiwa mguu wa kushoto, na Ahmed Waziri ambaye amekatwa sehemu ya kiganja mkono wa kulia”, alifafanua RPC Barlow.
Kamanda Barlow aliwataja majeruhi wengine watatu waliokimbizwa katika hospitali ya mkoa ya Sekou Toure na kulazwa kuwa ni pamoja na Haji Mkwenda (21), ambaye amevunjika mguu wa kulia, Judith Madaru (26), ambaye amechomwa kisu sehemu ya ziwa upande wa kushoto na Ivori Festo Machimba (26), ambaye amejeruhiwa kichwani na mdomoni.
Barlow alifafanua kuwa walipofika katika eneo la tukio polisi walikuta magari matatu huku mawili yakiwa na funguo na kuyaokoa kwa kuyaondoa, baada ya wananchi kuanza kuyarushia mawe huku gari moja ambalo halikuwa na funguo liliondolewa eneo hilo kwa kuvutwa na gari la kuvutia magari.
Alitaja namba za magari yaliyokutwa kwenye eneo la tukio kuwa ni pamoja na T 377 ARF linalomilikiwa na mbunge Kiwia, T 729 DAD linalomilikiwa na Mohamed Juma pamoja na T 397 ANU aina ya Land Cruiser ambalo mmiliki wake hakupatikana.
Wabunge hao simu zao zote zilikuwa zimezimwa hadi tunakwenda mitamboni.
Baadhi ya wananchi wakiwemo wanaharakati na wachambuzi wa mambo ya kisiasa mkoani Mwanza, wamelaani vikali unyama huo uliofanywa na wafuasi wa CCM, na kusema kamwe chama hicho tawala hakitapoteza muda kuondoka madarakani.
“Tunalaani vikali sana unyama huu waliofanyiwa wabunge wetu hawa. Hizi ni siasa chafu zilizoanza kutumiwa na CCM, na kamwe siku za mwisho za utawala wa chama hiki tawala umefika.
“Tunaliomba jeshi la polisi lihakikishe linawakamata na kuwafikisha mahakamani watu wote waliohusika katika tukio hilo bila kuangalia wanatoka chama gani na ni akina nani. Uonevu huu hauvumili, tunataka kuona hatua kali zinachukuliwa”, alisema mkazi mmoja wa jiji la Mwanza, Neema Marco.
Imeandaliwa na Sitta Tuma, Mwanza
Wakati huo huo, Mbunge wa Ubungo, John Mnyika ametoa taarifa kulaani tukio hoilo.
Taarifa kamili ya Mnyika hii hapa.
Sunday, April 1, 2012
CCM inategemea matusi, mafisadi na wamwagaji damu; ‘kudumisha amani na utulivu’ ni maneno ya kuficha matendo yao maovu
CCM ni chama chenye kukumbatia matusi, mafisadi, uongo na umwagaji damu; maneno yao juu ya amani na utulivu ni ya kuficha matendo maovu ya viongozi wake.
Poleni wananchi wa Mwanza na wapenda demokrasia na maendeleo kote nchini. Nami nimesikitishwa na naalani tukio la wabunge Highness Kiwia na Salvatory Machemli kushambuliwa kwa mapanga na mawe usiku wa kuamkia leo mara baada ya kampeni za uchaguzi wa udiwani unaofanyika leo. Hakika tukio hili halitaishia kusikitika na kulaani, tutachukua hatua za ziada. Naendelea na mawasiliano na mashauriano na viongozi wakuu walioko Arumeru Mashariki na maeneo mengine na tutaeleza hatua zitazofuata.
Ushahidi wa kimazingira unaonyesha kwamba tukio hilo la Mwanza limefanywa na WanaCCM, ushahidi wa tuhuma za kihistoria unathibitisha kwamba CCM na serikali yake imekuwa na kawaida ya kumwaga damu nyakati za chaguzi kwa njia mbalimbali ikiwemo kwa kukata viongozi wa CHADEMA mapanga, sasa wamefikia hatua ya kushambulia viongozi wa wananchi; wabunge.
Niliwahi kutahadharisha miaka michache nyuma kwamba kadiri CCM inavyoelekea kuondoka madarakani rangi yake halisi kinyume na maneno yao ya kinafiki ya ‘kudumumisha amani na utulivu’, matendo yao halisi yatajihidhirisha ya kuwa chama na serikali inayokumbatia vitisho, vurugu na umwagaji damu kama njia ya kujaribu kujiokoa na kukataliwa na umma. Wanafanya hivyo kwa kutumia vyombo vya dola na vikosi vya chama chao vya vitisho, vurugu na umwagaji damu.
Orodha ya chaguzi ndogo za ubunge zenye matukio kama hayo ni ndefu: Kiteto (2007) wanatuhumiwa mashambulizi ya aina hiyo tena ndani ya kituo cha polisi kwa ushirikiano baina ya askari polisi na vikosi vya CCM; Tarime (2008) wanatuhumiwa kukata mapanga wanachama wa CHADEMA; Busanda na Biharamulo (2009), wanatuhumiwa kukata mapanga viongozi wa CHADEMA; Igunga (2010), walituhumiwa kummwagia tindikali mwanachama wao na kuisingiza CHADEMA na hatimaye CCM ikahusishwa na kifo cha aliyekuwa wakala wa CHADEMA Mbwana Masudi. Nyakati zote hizo Polisi walifungua majalada ya uchunguzi, watuhumiwa baadhi walitajwa kwa majina, lakini mpaka sasa hakuna aliyetiwa hatiani kwa udhalimu huo dhidi ya binadamu.
Vyombo vya dola vinaposhindwa kusimamia utawala wa sheria na chama tawala kinapofanya siasa chafu za uongo, ufisadi na matusi ni wazi huvuka mipaka na kufikia hatua ya kufanya siasa za vitisho, vurugu na umwagaji damu nchi iko mashakani, amani na utulivu unaohubiriwa na CCM ni barakoa tu ya kufisha matendo yao maovu yenye baraka za viongozi wa chama hicho.
Viongozi hao hao watawahi kujitokeza kinafiki mbele ya vyombo vya habari kukanusha kuhusika, kulaani na kutoa pole za uongo; ujumbe wangu kwao na kwa vyombo vya dola, CCM haiwezi kulinda utawala wake kwa njia hizi za kihuni na kiharamia; kwa ukweli, haki na nguvu ya umma hatimaye tutashinda.
Nayaandika haya nikiwa Vijibweni kwenye uchaguzi wa marudio wa udiwani, mbinu hizi haramu za CCM za kutumia uongo, ufisadi na vitisho ndizo hizo hizo zimekuwa zikitumika hapa usiku wa kuamkia jana; matukio ya Arumeru Mashariki, Mwanza na kwingineko yanatupa moyo zaidi kwa kusonga mbele na kuchukua hatua; mpaka kieleweke.
John Mnyika (Mb)
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi
Chadema
01/04/2012
http://mnyika.blogspot.com/2012/04/ccm-inategemea-matusi-mafisadi-na.html