Viongozi wa Afrika wamekubaliana kuondoa vikwazo vya lishe vinavyowazuia watoto na jamii kutambua na kutumia rasilimali zilizopo katika nchi zao.
Viongozi hao walifikia uamuzi huo katika uzinduzi wa Programu ya Viongozi wa Afrika ya Lishe (ALN) kwa kushirikiana na Bank ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Tume ya Umoja wa Afrika jijini Addis Ababa, Ethiopia ambapo wamekubaliana kupambana dhidi ya utapiamlo na kuinua lishe kama kichocheo cha ukuaji wa uchumi na maendeleo endelevu.
Kwa mujibu wa rais wa Bank ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Akinwumi Adesina amesema watoto waliodumaa leo watasababisha uchumi wa kesho uliodumaa. Athari za udumavu hazikwepeki lakini zinazuilika.
Lishe duni ni sababu kuu ya udumavu kwa watoto ambapo huathiri zaidi maendeleo yao katika elimu na uchumi kwa siku zijazo. Mwaka 2016 pekee watoto milioni 59 wa Afrika walidumaa na milioni 14 walidhoofika na kupungua uzito. Ukiweka pamoja, idadi hiyo ni zaidi ya wakazi wote wa Ufaransa na Afrika Kusini; pia ni mara saba zaidi ya idadi ya wakazi wa Switzerland.
“Kuna kila sababu ya kujali: lishe duni ni kisababishi kikubwa cha vifo vya mamilioni ya watoto walio na umri chini ya miaka mitano. Watoto milioni 3 wanafariki kila mwaka barani Afrika kwa utapiamlo. Ikiwa hali hii itaendelea hadi 2030, Afrika itapoteza watoto milioni 36 kwasababu walikuwa hawana chakula cha kutosha au hawakula vizuri”, amesema Adesina.
Umoja wa Afrika (AU) umeidhinisha Programu ya ALN katika mipango yake na imeanzisha majadiliano na wadau mbalimbali wa afya ili kuimarisha lishe kwa watoto wa Afrika.
Waziri Mkuu wa Lesotho, Thomas Thabane, akisoma makubaliano ya viongozi wa ALN katika Makao Makuu ya Umoja wa Afrika amesema usalama wa chakula bila kuwa na lishe iliyoboreshwa hautaleta matokeo yalikusudiwa katika ukuaji wa uchumi wa Afrika. Pia amezitaka nchi zilizofanikiwa kumaliza udumavu kwa watoto kuzipa somo nchi nyingine zinazokabiliwa na tatizo hilo.
Inaelezwa kuwa Afrika ni bara pekee ambalo idadi ya watoto waliodumaa imeongezeka kutoka milioni 47 mwaka 1990 hadi milioni 59 mwaka 2016.
“Tuna wajibu wa kimaadili na kiuchumi wa kutatua janga hili la Afrika linalozuilika. Afrika itatokomeza udumavu na utapiamlo ikiwa viongozi wake wataungana na kutumia utashi wao”, amesema Adesina.
Kwa upande wake rais wa Madagascar, Hery Rajaonarimampianina, ambaye aliiwakilisha Tume ya Umoja wa Afrika kwenye utafiti wa Gharama za Njaa Afrika (COHA) amefanunua kuwa utapiamlo ni moja ya vikwazo vikubwa vinavyowazuia watoto na jamii kutambua na kutumia rasilimali zinazowazunguka.
“Watoto walioduma wanaumwa mara kwa mara- huongeza gharama za matibabu kwa familia ambayo ni asilimia 1 mpaka 30 ya bajeti yote inayoelekezwa kwenye afya au 3% ya GDP (Pato la ndani). Ikiwa tutapunguza kiwango cha udumavu kwa 50% ifikapo 2025, tunatarajia kuokoa Dola za Marekani bilioni 21.7. Ikiwa tutafikia lengo AU la Malabo na kupunguza udumavu kwa 10% na watoto walio chini ya uzito kwa 5% ifikapo 2025, tunatarajia kuokoa Dola bilioni 39.3”, amesema rais Rajaonarimampianina.
Hali ya Udumavu nchini Tanzania
FikraPevu imepata Ripoti ya Uchunguzi ya Taifa ya Lishe (2014) ambayo inabainisha kuwa asilimia 34.7 ya watoto wenye umri wa mwezi 0 hadi miezi 59 (0-59) wamedumaa au wana Utapiamlo wa kiwango cha juu.
Kwa Tanzania Bara, matokeo ya uchunguzi yanaonesha kiwango cha utapiamlo kiko juu zaidi ya asilimia 40 kwa mikoa 9 (Iringa, Njombe, Kagera, Dodoma, Ruvuma, Rukwa, Kigoma, Katavi na Geita) na katika mikoa hiyo iko yenye kiwango cha juu ya asilimia 50, Iringa (51.3%), Njombe (51.5%) na Kagera (51.9%).
Zanzibar ina viwango vya udumavu ambavyo vinatofautiana kati ya eneo na eneo, Mjini Magharibi ni asilimia 20 na Unguja Kusini ni asilimia 30.4.
Kwa mujibu wa matokeo hayo, zadi ya watoto milioni 2.7 walio chini ya umri wa miaka mitano wamedumaa nchini Tanzania ripoti hiyo inaeleza na kushauri hatua za haraka zichukuliwe katika mikoa ya Kigoma, Kagera, Mwanza, Iringa na Mbeya ambayo tatizo ni kubwa.
FikraPevu imeelezwa kuwa utapiamlo unatajwa kuwa sababu kubwa inayofanya watoto wengi kutokuwa na maendeleo mazuri ya ukuaji. Lishe duni isiyo na virutubisho muhimu kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano humfanya mtoto kupungua uzito na urefu kutoendana na umri alionao.
Takwimu kutoka Shirika la Misaada la Marekani (USAID), zinabaanisha kuwa utapiamlo unachangia karibu robo tatu ya vifo vya vichanga na watoto nchini Tanzania na asilimia 21 ya watoto wanaozaliwa wana uzito wa chini kuliko ule wanaopaswa kuwa nao.
Pia lishe duni kwa wanawake wakati wa ujauzito huchangia watoto wengi wanaozaliwa kudumaa. Kukosa virutubisho muhimu kwa mjamzito husababisha maambuki ya magonjwa ambayo humdhuru kiumbe aliyepo tumboni.
Mimba za utotoni, shinikizo la damu na kuzaa watoto mfufulizo bila kufuata uzazi wa mpango huongeza ukubwa wa tatizo kwa wajawazito kujifungua watoto waliodumaa.
Udumavu huathiri zaidi ufahamu wa mtoto na kupunguza uwezo wa kujifunza na kupokea maarifa mapya. Wanafunzi wengi wanafeli mashuleni na kukosa muelekeo wa maisha kwa sababu ya udamavu wa akili ambao huanzia wakiwa tumboni mwa mama zao.