Ufisadi waponza walimu kukosa malipo ya 283m/-

Jamii Africa

WALIMU zaidi ya 200 wa shule za msingi na sekondari mkoani Mbeya wanalalamikia vitendo vya ufisadi unaofanywa na watendaji serikalini na kusababissha kukosa fedha zao za mapunjo kiasi cha Sh milioni 283 licha ya kuhakikiwa majina yao mwaka 2009, imefahamika.

Mkurugenzi Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Juma Iddi

Walimu hao wanasema pamoja na majina yao kuhakikiwa mwaka 2009, lakini wameshangazwa kuona majina yao hayakutokea kwenye orodha ya madai kwenye halmashauri zao.

Aidha, wamesema kwamba, orodha hiyo ya madai iliyotolewa mwaka jana kwenye halmashauri zote inafuatia tishio lao la mgomo baada ya madai ya walimu 432 wa mkoa huo kushindwa kutekelezwa kwa karibu miaka miwili.

Katika madai ya awali, walimu hao walitishia kugoma kama shinikizo kwa Serikali kulipa malimbikizo ya madai yao kiasi cha Sh. 550,289,470.40.

“Madai yetu yalikwishahakikiwa muda mrefu, tangu mwaka 2009, tulipotishia kugoma wakaleta orodha ya wanaostahili kulipwa, lakini bado majina yetu hayapo,” alisema mmoja wa walimu hao aliyeomba kutotajwa jina lake kutokana na kuhofia hatima yake katika ajira.

Katibu wa Chama cha Walimu mkoani Mbeya, Kasuku Bilago, alikiri kuwepo kwa malalamiko ya walimu hao na kuongeza kwamba chama chake kimekuwa kikishughulikia suala hilo bila mafanikio.

“Ni kweli kwamba walimu kadhaa hawamo kwenye orodha ya wanaostahili kulipwa licha ya kuhakikiwa na kuonekana wanastahili. Tumejitahidi kulishughulikia suala hili bila mafanikio na watendaji wa serikali wanaonekana kupiga danadana.

“Awali tulipokuwa tunashughulikia walisema wanasubiri fungu kutoka serikalini, lakini fungu lilipotoka tunashangaa wanachama wetu wengine wameachwa licha ya ukweli kwamba wanastahili,” alisema Bilago.

Taarifa zinaeleza kwamba, kiasi cha Sh 35 milioni kilichopelekwa mwaka jana katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya Vijijini hakijalipwa hadi sasa, huku walimu wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya wakiidai Serikali kiasi cha Sh 63 milioni. Walimu waliostahili likizo ya mwezi Desemba 2011 na walimu wapya nao hawajalipwa haki zao hadi sasa.

Kwa upande wa Wilaya ya Rungwe, walimu wapato 40 hawajalipwa zaidi ya Sh 100 milioni wakati fedha hizo zilipelekwa Halmashauri, wakati wilayani Mbozi, walimu wapatao 85 wanadaiwa kuondolewa kwenye orodha baada ya uhakiki na kwamba wanadai Sh 85.4 milioni.

Katibu Tawala mkoa wa Mbeya, Beatha Swai

“Fedha hizi hazikuletwa kwa kuwa zilinyofolewa kwa mbinu za kuficha ukubwa wa deni wilayani, wahusika ni watendaji wa Halmashauri,” amebainisha Bw. Bilago.

Mwaka jana walimu hao walitishia kuitisha mgomo mwezi Julai kufuatia Serikali kushindwa kulipa malimbikizo ya mapunjo ya mishahara yao yanayofikia Sh 550 milioni tangu walipopandishwa daraja mwaka 2007.

Juhudi za kumpata Katibu Tawala wa Mkoa,  Beatha Swai na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Juma Iddi, hazikuweza kuzaa matunda, lakini Chama cha Walimu mkoani humo kimeahidi kulisimamia suala hilo ili wanachama wake wapate haki zao.

 

1 Comment
  • Wale wote waliohusika na ubadhirifu huo wa fedha za umma wachukuliwe hatua kali kwani hawa wachache ndio wnaoichafua serikali ionekane haitekelezi majukum yake ipasavyo.
    Natumai Mkoa wa Mbeya utachukua jitihada za dhati kuhakikisha watu hao wanashughulikiwa kwa mujibu wa sheria pia kuhakikisha suala la walimu hao nao linapata ufumbuzi,tuliopewa dhamana ya kuongoza tuwe waadilifu jamani

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *