Uhaba wa rasilimali watu, miundombinu kuikwamisha Tanzania safari ya viwanda

Jamii Africa

Benki ya Dunia  imeizishauri nchi za Africa ikiwemo Tanzania kuboresha mfumo wa utendaji wa taasisi za umma, miundombinu na kuwekeza kwenye rasilimali watu ili kukuza uchumi na kuwaondolea wananchi umaskini.

Akizungumza leo katika semina iliyoandaliwa na Benki ya Dunia pamoja na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kuhusu uchumi wa dunia, Mkurugenzi Mkuu wa Uchumi, Biashara na Uwekezaji wa Benki ya Dunia, Dkt. Carlos Felipe Jaramillo amesema uchumi wa Afrika umeimarika na jitihada za kitaasisi zinahitajika kuondoa umaskini kwa wananchi.

“Uchumi wa Afrika umeimarika mpaka sasa, na nchi ambazo uchumi wake unakua ikiwemo Tanzania zinafanya vizuri hasa kwenye pato la ndani la taifa”, amesema Dkt. Jaramillo.

Anasema Ukuaji wa uchumi kwa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara umekuwa hadi asilimia 3.2 mwaka 2018 na utafikia 3.5 ifikapo 2019 ambapo ni juu ya kidogo ya ukuaji wa idadi ya watu.

“Kwa upande wa usafirishaji wa mafuta, ukuaji wa pato utakuwa sio wa kuridhisha lakini utaimarika nchini Ghana. Ukuaji katika nchi ambazo hazitegemei rasilimali asilia utakuwa wa kuridhisha, ukichagizwa na Senegal na Ivory Cost”, amesema Dkt. Jaramillo.

Akizungumzia hali ya uchumi wa Tanzania amesema nchi inafanya vizuri ukizingatia kuwa Tanzania iko miongoni mwa nchi 10 duniani ambazo uchumi wake unakua kwa kasi lakini changamoto iliyopo ni mazingira yasiyo rafiki kwa wawekezaji ikiwemo ubovu wa miundombinu na mlolongo wa kodi ambazo haziendani na halisi ya uzalishaji bidhaa.

“Uchumi wa Tanzania unafanya vizuri duniani lakini changamoto ni kutokuwepo kwa miundombinu imara na mazingira mazuri kwa wawekezaji kuwekeza”, amesema Dkt. Jaramillo.

Kutokana na changamoto hizo wananchi wamebaki kwenye umaskini kwasababu ya kukosa huduma muhimu za jamii. “Lakini jitihada zinahitajika kupunguza umaskini kwa sababu kiwango cha umaskini uliopitiliza (cha Afrika) kimeongezeka kutoka asilimia 15 mwaka 1990 hadi kufikia asilimia 49 mwaka 2015, licha ya idadi hiyo kwa dunia nzima kupungua kutoka watu bilioni 1.9 hadi milioni 702”, amesema.

Baadhi ya washiriki wa semina juu ya Uchumi wa Dunia iliyoandaliwa na Benki ya Dunia na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam iliyofanyika katika ukumbi wa Council Chamber  uliopo UDSM.

Amebainisha kuwa ili Tanzania iondokane na umaskini na kukuza uchumi wenye tija ni muhimu kwa taasisi za umma kufanya kazi kwa uwazi na kuzingatia misingi ya demokrasia inayohimiza matumizi mazuri ya rasilimali za umma.

Pia kuzalisha na kuendeleza rasilimali watu ikiwemo kutoa mafunzo na kuinua ubora wa elimu inayotolewa shuleni ili kuwajengea uwezo wanafunzi kuvumbua na kutumia teknolojia ya kisasa itakayoongeza uzalisha hasa katika sekta ya kilimo na viwanda.

Hakuacha kuzungumzia uboreshaji wa miundombinu ya barabara na reli ili kuvutia wawekezaji kuwekeza katika meneo mbalimbali ya nchi.

 

Wadau wanena

Akichangia katika semina hiyo, Mhadhiri wa zamani wa UDSM, Prof. Samuel Wangwe amesema ili kukuza uchumi ni muhimu kuangalia sekta zipi zinahusika katika ukuaji wa uchumi wa nchi, “Mfano kilimo lazima kiangaliwe upya kwasababu hakijarasimishwa na kuwa rasmi ndio maana uzalishaji wake haukui na kuleta matokeo chanya kwenye uchumi wa nchi”

Amesema kama taifa tujengewe uwezo wa kufahamu utendaji wa uchumi wa dunia na unavyoathiri uchumi wa nchi ili tujiweke katika nafasi ya kukabiliana na mabadiliko yanayotokea hasa kwenye soko la bidhaa.

Kwa upande wake, Prof. Andrew Temu amesema kuna haja ya  kuitazama upya Sekta ya fedha  ili itoe mchango mzuri kwa sekta nyingine za uzalishaji ikiwemo kilimo ili wakulima wapate teknolojia na fedha za kuwekeza kwenye kilimo cha kisasa.

“Benki ya Maendeleo (TIB) ingalie zaidi sekta ya kilimo kwasababu ndio kiungo muhimu cha ukuaji wa uchumi”, amesema.

Naye Azaveli Lweitama, aliyewahi kuwa Mhadhiri wa UDSM amebainisha kuwa ni muhimu kuzalisha bidhaa mpya za kilimo na viwanda lakini uzalishaji huo utafanikiwa endapo utahusisha kuwaongezeka wanafunzi ujuzi wa kujifunza mbinu mbalimbali za uwekezaji utakaofungua milango katika maeneo mbali ya nchi.

 Awali akifungua semina hiyo, Mkurugenzi wa Benki ya Dunia kwa nchi za Tanzania, Malawi, Burundi na Somalia, Bella Bird amesema wataendelea kushirikiana na Tanzania ikiwemo kutoa ushauri wa uchumi na fedha ili kutekeleza miradi ya maendeleo inayolenga kuwaondolea wananchi umasikini.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *