KUNA Hospitali ya Taifa Muhimbili. Kuna hospitali kubwa binafsi na zenye vifaa vingi vya kisasa vya tiba. Kuna miundombinu bora. Kuna wataalamu mabingwa waliobobea kwenye sekta ya afya, lakini bado Dar es Salaam ni miongoni mwa mikoa inayoongoza kwa vifo vya wagonjwa.
Nini sababu ya kuwepo hali hiyo? Jibu ni kwamba kuna uzembe, rushwa na kukosekana kwa wito wa kazi, FikraPevu inaripoti.
Mbali ya uzembe wa watumishi hao, inaelezwa kwamba uhaba wa dawa na vitendanishi ni sababu nyingine iliyofanya Dar es Salaam kuwa miongoni mwa mikoa inayoongoza kwa idadi ya vifo vya wagonjwa.
“Uwajibikaji ni jambo la muhimu sana, kwa hiyo hata kama kuna watendaji wengi, kama ni wazembe haiwezi kusaidia kupunguza idadi ya vifo na kutoa huduma bora kwa wagonjwa,” anasema Dk. Jackson Mboya kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Dk. Mboya anasema, kuongezeka kwa vifo hivyo pia kunachingiwa na kukosekana kwa vitendanishi pamoja na motisha na maslahi duni kwa watumishi, jambo ambalo alisema linapaswa kufanyiwa kazi na mamlaka husika.
Hata hivyo, alisema uwiano wa idadi ya wafanyakazi na wagonjwa ni muhimu katika sekta hiyo kwani ni moja ya changamoto zinazokwamisha utoaji huduma kwa wakati.
“Ukiacha uzembe na uwajibikaji mbovu, lakini upungufu wa watendaji unaweza kuongeza vifo kwa wagonjwa, lakini ieleweke kwamba, bila kuwepo na uwajibikaji makini idadi pekee haitasaidia chochote,” anasema.
Wananchi wamekuwa wakilalamika kuwepo kwa madai ya watendaji wa hospitali za Dar es Salaal, ikiwamo Muhimbili kupokea rushwa.
Madai haya ya rushwa hayakuanza leo wala jana, yamekuwepo muda, pamoja na kwamba baadhi ya viongozi wa Hospitali ya Muhimbili wamekuwa wakikanusha.
Kwa upande mwingine, Dk. Mariam Mbegi kutoka Hospitali ya Rufaa ya Temeke, Dar es Salaam, ameiambia FikraPevu kwamba, kuongezeka kwa vifo vya wagonjwa kumechangiwa na uwiano usioridhisha baina ya wafanyakazi wa sekta hiyo na wagonjwa.
Aidha, alisema kuongezeka kwa magonjwa mapya pamoja na mabadiliko ya teknolojia nako kunachangia vifo hivyo, kwani si watendaji wote wenye uelewa wa magonjwa mapya yanayoibuka.
“Kwa ujumla, uwiano wa wafanyakazi wa afya na wagonjwa haukidhi haja kutokana na ongezeko la maradhi pamoja na mabadiliko ya teknolojia ya matibabu, inalazimu watumishi wa sekta ya afya wawe na ujuzi wa kutosha na weledi wa kufanya kazi,” alisema Dk. Mbegi.
Lakini FikraPevu imebaini kwamba, upungufu pekee wa watendaji siyo kigezo cha ongezeko la vifo vya wagonjwa, kwani ipo mikoa yenye watendaji wachache ambayo idadi ya vifo iko chini.
Mikoa inayoongoza kwa vifo vya wagonjwa ni Arusha, Singida, Mara, Mtwara na Dar es Salaam wakati mikoa yenye vifo vichache ni Mwanza, Dodoma, Pwani, Kigoma na Morogoro.
Aidha, mikoa yenye idadi kubwa ya watendaji katika sekta ya afya inatajwa kuwa Kilimanjaro, Iringa, Dar es Salaam, Mbeya na Tanga wakati Tabora, Kigoma, Kagera, Mara na Manyara ina watendaji wachache.
FikraPevu inaona kwamba, kuna haja ya serikali na idara zake kuangalia chanzo cha ongezeko la vifo kwa wagonjwa, mbali ya suala la upungufu wa watendaji na vitendanishi.
Licha ya serikali kutilia mkazo umuhimu wa utoaji wa huduma bora za afya, lakini kwa miaka mingi sekta hiyo imekumbwa na changamoto mbalimbali zikiwemo upungufu wa vituo vya huduma, dawa, madaktari na wauguzi, huku wahudumu wa sekta hiyo wakilalamikia maslahi duni na malimbikizo ya madai yao, jambo ambalo limesababisha migomo mara kadhaa iliyochangia pia vifo vya wagonjwa.
Sera ya Afya ya mwaka 2007 inasisitiza umuhimu wa kuwepo kwa wataalam wa kutosha, wenye ujuzi wa kutoa huduma bora katika ngazi zote, lakini pia inakiri kuwepo kwa changamoto lukuki ikiwemo ufinyu wa bajeti.
Kwa miaka 16 sasa Serikali imeshindwa kuiongeza bajeti ya afya kufikia asilimia 15 ya kuu kama inavyosisitizwa kwenye Azimio la Abuja la mwaka 2001, hali ambayo inaendelea kuleta changamoto katika utoaji wa huduma bora.
Miongoni mwa mambo yanayosisitizwa kwenye Sera hiyo ni pamoja na kupunguza viwango vya vifo vya wanawake vinavyotokana na uzazi, kupandisha ari ya utendaji kazi wa watumishi wa sekta ya afya kutokana na mishahara midogo, ukosefu wa motisha na upungufu wa vitendea kazi, na kudhibiti ongezeko kubwa la bei za dawa, vifaa na vifaa tiba.
Wakati ambapo Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2016/17 ni Shs. 29.5 trilioni, ni kiasi cha Shs. 1.99 trilioni tu, sawa na asilimia 9.2 ambacho kimeelekezwa kwenye afya, ingawa Bajeti ya Wizara ya Afya inaonyesha kuwa fedha zilizoidhinishwa na Bunge zilikuwa Shs. 845,112,920,056.00.
Kati ya fedha hizo, Shs. 317,752,653,000.00 ni kwa Matumizi ya Kawaida na Shs. 527,360,267,056.00 ni kwa ajili ya utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo.
Suala la afya bora linatiliwa mkazo na Serikali hata kupitia mipango yake mbalimbali kama Mkakati ya Kukuza Uchumi na Kuondoa Umaskini (Mkukuta) na Dira ya Taifa ya Maendeleo kuelekea mwaka 2025.
Aidha, kutofikiwa kwa bajeti ya afya kunaweza kukwamisha Lengo Namba 3 la Malengo Endelevu ya Dunia (SDG) linalosisitiza Afya Bora na Ustawi kama ilivyoazimiwa Septemba 25, 2015 jijini Geneva, Uswisi.