Katika kile kinachoaminika kuwa ni utekelezaji wa agizo la Waziri wa Mambo ya Ndani Bw. Shamsi Vuai Nahonda la kuwataka maafisa uhamiaji kuonesha ndani ya wiki tatu wamefanya nini kudhibiti uhamiaji haramu mmiliki wa kampuni ya Jandu Construction & Plumbing, Indertit Sigh Jandu, amekamatwa na Uhamiaji kwa tuhuma za kuwahifadhi na kuwatumikisha wahamiaji haramu 18.
Jandu ambaye ameshiriki kujenga jengo la Uhamiaji Kurasini, alionyesha jeuri akidai kuwa na mahusiano na vigogo Uhamiaji, serikalini na wanasiasa lakini sasa yuko mahabusu. Walikamatiwa eneo la kampuni hiyo Buguruni Dar es Salaam Jumatatu usiku. 17 ni raia wa India na mmoja wa Pakistan. Jandu aliamua kutafuta njia ya kuzima sakata hilo kwa ‘wakubwa’ kwa kwenda makao makuu ya Uhamiaji lakini akakwaa kisiki.
Wafanyabiashara wenye asili ya Kiasia wamekua wakifanya biashara ya watu kwa kuingiza wahamiaji wengi na kuwatumikisha katika kampuni zao, baadhi wakiwa katika maandalizi ya kwenda kufanya kazi Afrika Kusini.
Wahamiaji wanaoletwa nchini kwenda Afrika Kusini hutozwa hadi Dola za Marekani 10,000 ambazo kwa ajili ya kupelekwa kufanya kazi nchini Afrika Kusini, biashara ambayo hufanywa na wafanyabiashara wengi nchini. Wageni ambao huwa hawana fedha za kulipia gharama hizo, hufanyishwa kazi kwa muda mrefu bila malipo ya kutosha kabla ya kusafirishwa kwenda Afrika Kusini.
Pichani chini watu hao wanaotuhumiwa uhamiaji haramu mikononi mwa maofisa wa Uhamiaji. Kwa mujibu wa taarifa zilizopatakana jioni Jandu na wenzake wanatarajiwa kupandishwa kizimbani siku ya Alhamisi wakikabiliwa na mashataka kadhaa ya kukiuka sheria za uhamiaji.