Ukimya wa wanazuoni pale demokrasia inapokanyagwa hautaiacha nchi salama

Jamii Africa
young graduates standing in front of university building on graduation day

Wajibu wa wasomi au wanazuoni katika jamii ni mada muhimu na pana sana. Hakuna mtu yoyote anayeweza kukataa mchango muhimu wa wasomi katika jamii yoyote na hasa katika kipindi hiki ambacho kina mabadiliko ya haraka mno.

Wasomi ni watu wenye elimu, maarifa, fikra na mawazo mapana ambayo wanatakiwa kuyatumia ili kuinusuru jamii isiingie katika matatizo. Wasomo wana wajibu wa kutafakari na kuchambua changamoto zilizoko mbele ya jamii na kuiamsha jamii ili iweze kuchukua hatua zinazopasa.

Wanaisaidia jamii kutoka katika muelekeo potofu na kuipeleka katika mueleke  wenye manufaa. Yapo mambo muhimu ambayo wasomi kwa kawaida huwa nayo, nayo ni: Elimu au Maarifa, Uwezo na Ushupavu wa kuiamsha jamii.

Kutokana na ukweli huu, ndio maana naona maneno ya Mwanazuoni Eistein ni muhimu sana kuyarejea hapa.

Yeye alisema: “Dunia ni mahali hatari sana si kwasababu ya watu wanaofanya uovu, bali ni kwasababu ya wale wanaona uovu na hawafanyi lolote au hawachukui hatua yoyote.”

Wasomi pamoja na Watanzania kwa ujumla, sote hatuna budi kujitathimini katika hili. Je, tunachukua hatua zinazostahili katika kupambana na rushwa, matumizi mabaya ya madaraka, uvunjifu wa haki za binadamu kama vile uhuru wa kutoa maoni, uhuru wa kubadilishana taarifa.

Pia Mtume Muhammad (S.A.W), katika kitabu cha Quran  alisema. “Unapoona jambo baya basi liondoe kwa mkono wako, kama huwezi basi liondoe kwa ulimi wako na kama hayo yote huyawezi basi angalau chukia katika moyo wako, na huo ni uchache wa imani.”

Hivyo basi, wasomi wanao wajibu mkubwa wa kukosoa, kuzuia maovu na kuiamsha jamii ili iweze kuepukana na mambo ambayo hayana faida. Wasomi wapo katika nafasi nzuri ya kuweza kubaini ghilba za wanasiasa au serikali, kuchambua sera, mipango na utekelezaji wake, hata yale malengo yaliyofichika.

Lakini wanaweza kufanya hivyo katika mazingira ambayo haki za kiraia zinaheshimiwa, kuna upatikanaji wa taarifa na kuna uhuru wa kujieleza kupitia njia mbalimbali.

Wana wajibu mkubwa katika kutafuta ukweli wa mambo na kubadilishana mawazo na wananchi. Kazi hii ya kutafuta ukweli ni kazi adhimu na ndio huwafanya wafanye uchambuzi na tafiti mbalimbali ili waweze kubaini si tu matatizo bali pia chanzo cha matatizo hayo na pia kutafuta majibu na kutoa mapendekezo ya namna bora ya kukabaliana na changamoto hizo.

Wana jukumu la kutafakari  na kutueleza, hivi ni kwa nini nchi yetu ni tajiri kwa rasilimali za asili lakini pia ni nchi masikini sana! Wapi tunakosea? Na je, tufanye nini? Wasomi hawana budi kufanya tafiti na kutueleza ni kwa nini tunasikia kila siku kukua kwa uchumi, lakini kukua huku kwa uchumi hakujaweza kubadili maisha ya Watanzania walio wengi? Je, tufanye nini ili tuweze kuwa na ukuaji wa uchumi mpana ambao utawagusa Watanzania walio wengi.

Ni jukumu pia la wasomi kuchambua vipaumbele vyetu na kushauri iwapo vipaumbele hivyo ni sahihi kulingana na changamoto tulizonazo. Tunaweza vipi kuboresha ubora wa elimu na huduma nyingine za jamii kama vile afya, maji, na miundombinu. Katika jamii yetu, kundi la wasomi na asasi za kiraia hutarajiwa sana kuangalia mienendo ya wanasiasa na kuifanyia uchambuzi na kuwaeleza wananchi ukweli juu ya mienendo hiyo.

Pale ambapo Wasomi na asasi za kiraia zinaposhindwa kufanya hivyo, ama kwa kuogopa au kwa tumaini la kupata uteuzi basi jamii hukosa uchambuzi na hiyo ni hatari kubwa sana kwa maendeleo kwani mawazo mbadala ndiyo huleta maendeleo na. Haitarajiwi kwa wasomi kukaa kimya pale katiba inapovunjwa, haki za binadamu zinapovunjwa au pale utawala wa sheria unapokiukwa.

Kazi na wajibu wa wasomi ni kuchambua masuala haya na kuyaweka bayana na hadharani, ili wananchi waweze kuyaelewa na kuchukua hatua zinazopasa. Uchambuzi pia huweza kuisaidia serikali ili iweze kufanya marekebisho katika sera zake na mipango yake na hivyo Taifa kusonga mbele.

Ni haki kabisa kuuliza maswali kadhaa; Katika nchi yenye wasomi lukuki, ilikuwaje tukaingia katika sera ambazo ziliua uchumi wetu na kuturudisha nyuma. Uchambuzi wa sera hizi ulifanyika kweli? Sera za kurekebisha uchumi kama vile ‘Structural Adjustment Programme’(SAP)! Sera za ubinafsishaji na uuzaji wa mashirika ya umma? Je, kwanini vilikufa viwanda vilivyoanzishwa miaka ya 1960? Je, uchambuzi wa sera ya kilimo kwanza na Matokeo Makubwa sasa vimefikia wapi? Je, mbona hatusomi uchambuzi wa kwanini zoezi la kuandika katiba mpya lilikwama?!

Mabilioni ya JK na Machinga Complex, nini tunaweza kujifunza katika haya? Tulifanikiwa kwa kiasi gani na labda tungefanya nini ili kupata matoke mazuri zaidi? Haya ni baadhi tu ya maswala ambayo yana walazimu wasomi na pia asasi za kirai kufanya chambuzi na tafiti ambazo zitaweza kuboresha mipango yetu ijayo.

Wasomi wanaijua historia ya nchi yetu. Wanajua tulikotoka, tulipo sasa na hilo huwasaidia kujua tunakokwenda.  

 

Mwandishi wa makala hii ni Selemani Rehani anapatikana kwa namba. 0755 209666, [email protected]

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *