Ukosefu wa takwimu sahihi za vituo vya maji kikwazo cha maendeleo vijijini

Jamii Africa

Daniel Samson

Baadhi ya wananchi waishio vijijini wataendelea kusubiri kupata huduma ya maji ya uhakika kwa muda usiojulikana  kwasababu ya  kukosekana kwa takwimu za utendaji wa vituo vya maji nchini.

Tanzania kupitia miradi ya maji vijijini imejenga zaidi ya vituo 80,000 vya maji ambavyo vimeunganishwa na mfumo wa maji ya bomba. Kuna baadhi ya vituo  vimechakaa vinahitaji matengenezo lakini ukosefu wa takwimu sahihi juu ya vituo hivyo kunakwamisha serikali kupanga bajeti ya kuwapatia wananchi wa vijijini huduma bora ya maji.

Takwimu zilizopo katika ripoti ya maendeleo ya sekta ya maji mwaka 2016, zinaonyesha kuwa kati ya mwaka 2010/11 na mwaka 2015/16, Serikali ilipanga kujenga jumla ya vituo vya maji 99,515 lakini ilishia kujenga vituo 42,718 pekee.

Vituo hivyo vilivyojengwa ni asilimia 43 tu ya malengo jambo ambalo linaloonyesha kuwa idadi kubwa ya wananchi waliotakiwa kupata huduma hiyo wameshindwa kupata kwa wakati.

 Ripoti hiyo iliyotolewa Oktoba mwaka 2016 inaeleza kuwa theluthi moja ya miradi hiyo ya maji haikutekelezwa ndani ya awamu ya kwanza ya mpango wa maendeleo ya sekta ya maji (WSDPI) jambo lilofanya baadhi ya vituo vya maji vichelewe kujengwa.

“Hadi Juni 2016, jumla 1,210 kati ya 1,810 iliyopangwa ilikuwa imetekelezwa na kusambaza maji kwa wananchi. Miradi mingine 374 ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji katika mwaka huu wa fedha wa 2016/17,” inasomeka sehemu ya ripoti.

Ili kuboresha upatikanaji wa maji maeneo ya vijijini, Idara ya Maendeleo ya Uingereza (DFID) kwa kushirikiana na serikali ya Tanzania kupitia program ya malipo baada ya matokeo (PbR) imeanza kuziwezesha Halmashauri za Miji nchini kuviendeleza vituo vya maji vilivyopo na kutumia takwimu kujenga vingine vipya katika maeneo yenye uhitaji mkubwa wa maji.

Programu hiyo imeteua timu ya wataalamu zaidi ya 20 ambao wanatumia teknolojia ya kisasa kuhakiki na kuchambua idadi ya vituo vya maji vilivyopo. Pia katika maeneo ambayo yana changamoto ya teknolojia ya mawasiliano, wataalamu hao wanalazimika kutembelea vijiji ili kujionea hali halisi ya utendaji wa vituo vya maji

Ili kufikia malengo, mwaka 2017 wataalamu hao walitembelea vituo 9,0000 katika Halmashauri 56 nchini. Changamoto iliyojitokeza ni kutofautiana kwa taarifa za baadhi ya vituo zilizopo Wizara ya Maji na Umwagiliaji na eneo kilipo ikizingatiwa kuwa maeneo mengi ya vijijini hayana anuani na mitaa yenye mpangilio mzuri.

Changamoto hiyo iliwawezesha kutengeneza mfumo wa kiufundi ambao unawawezesha wataalamu kufika kwenye kituo ili kubaini uwepo na uhai wa kituo cha maji. Mfumo huo unajumuisha kifaa cha kutunza kumbukumbu (Ona), kukusanya taarifa (ODK Collect) na ramani huru inayoonyesha vituo vya maji.

Mchakato wa upatikanaji wa takwimu unajumuisha hatua 3 za usimamizi; kwanza ni wataalamu kukusanya taarifa na kuziwasilisha kwa kutumia ujumbe mfupi wa simu. Pili kuthibitisha taarifa zilikusanya na zile za wizara ili kupata picha ya vituo hivyo. Mwisho ni kuhakikisha kama taarifa za vituo vyote zipo.

Programu hiyo ilifanikiwa kwa asilimia 90 na itaendelea kutumika katika maeneo yote nchini kuwezesha serikali na wadau wa maendeleo kupata takwimu sahihi za vituo vya maji maeneo ya vijijini.

Kutokana na kazi nzuri iliyofanywa na timu hiyo ya wataalamu, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji wa wakati huo, Mhandisi Mbogo Futakamba amesema kuwa katika awamu ya pili ya mpango wa maendeleo ya sekta ya maji wamejipanga kuondoa mapungufu yaliyojitokeza yakiwemo yakiundeshaji.

Awamu ya kwanza ya mpango huo ilikuwa kati ya mwaka 2006/07 na 2013/2014.

Futakamba ameeleza katika ripoti hiyo iliyotolewa mwishoni mwa mwaka 2016  kuwa katika awamu ya kwanza kuna zaidi ya wakala 300 wa utekelezaji miradi ya maji nchi nzima ili kufanikisha usambazaji wa huduma za maji safi na salama kwa wananchi zaidi milioni 20.

                                                                      Wataalamu wakikagua kituo cha maji

 

Mipango ya awali ya kutekeleza mpango huo inabainisha kuwa mahitaji ya awali ya kifedha ni Dola za Marekani 3.32 bilioni sawa na Sh7.23 trilioni.

Hadi Oktoba mwaka juzi, Futakamba anasema kiwango ambacho kilishakuwa kimeahidiwa kutolewa kilikuwa Dola za Marekani 1.65 bilioni sawa na Sh3.59 trilioni.

“Kuna jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo kuhakikisha kuwa fedha zinawafikia watekelezaji wa miradi kurahisi kutoka kwenye chanzo kikuu.  Baadhi ya wadau wa maendeleo wameanzisha mipango ya kifedha ambayo imelenga kuongeza upatikanaji wa maji nchini,” anasema Futakamba.

Awamu ya pili ya mpango wa maendeleo ya maji (WSDP II) ilianza kutekelezwa mwaka 2014/15 na inatarajiwa kukamilika mwaka 2018/19.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *