Wataalamu wakiri uwezo wa Dawa ya Babu; Marekani yataka wagonjwa wasiache dawa!

Jamii Africa

Hatimaye taarifa ya Kitaalamu iliyokuwa inasubiriwa kwa hamu kuhusu uwezo wa “kikombe cha babu” wa Loliondo imepatikana na inaonesha kuwa kwa kiasi kikubwa madai ya Mch. Ambilikile Mwasapila kuwa hiyo ambayo alidai kuwa alioteshwa na Mungu ina sifa za kitabibu za kuleta ahueni ya afya kwa watu wenye kusumbuliwa na magonjwa kadhaa makubwa.

Ripoti hiyo ambayo imeandaliwa na wataalamu waliobobea katika sayansi ya madawa kutoka taasisi za Kitaifa imeelezea kwa lugha ya kitaalamu sifa za kikemia za mmea unaotumiwa na Mchg. Mwasapila na jinsi ambavyo kemikali zilizomo katika mmea huo zinaweza kusaidia kutibu magonjwa mbalimbali.

Babu Loliondo akitoa Kikombe
Mchungaji Ambilikile akitoa huduma huko Loliondo

Dr. Hamisi Malebo pamoja na Dr. Zakaria Mbwambo ndio waliofanya utafiti huo na kutoa ripoti hiyo ambapo pamoja na kutoa mahitimisho ya awali ya kisayansi juu ya dawa hiyo wametoa vile vile mapendekezo kadhaa kwa hatua za mbeleni. Dr. Malebo ni mwanasayansi katika Idara ya Utafiti wa Tiba za Jadi ya Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Tiba Jijini Dar-es-Salaam wakati Dr. Mbwambo ni mtaalamu wa mambo ya madawa kutoka Idara ya Tiba za Jadi ya Chuo Kikuu cha Tiba cha Muhimbili pia kutoka Jijini Dar-es-Salaam.

Watalaamu hao ambao walienda kijijini Samunge, Loliondo Mkoani Arusha walishirikiana na wataalamu wengine mbalimbali na katika taarifa yao hiyo walimshukuru kwa namna ya pekee Mchg. Mwasapile “kwa unyenyekevu wake” wa kutoa ushirikiano kwa watalaamu hao kwa kuwapatia mlango wazi wa kuangalia huduma na kuchukua kiasi cha dawa kwa ajili ya kufanyia utafiti.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo majukumu ya timu hiyo ya kitaalamu kufuatilia “kikombe cha babu” yalikuwa ni manne; kwanza, kuyaangalia madai  yanatolewa kuhusu matumizi ya dawa hiyo katika jumuiya husika, usalama wa tiba hiyo kama inavyoandaliwa na Mchg. Mwaisupile, uwezo wa tiba kama inavyodaiwa na babu huyo na vile vile kutoa mapendekezo ya utaratibu unaopaswa kutumiwa kwa siku za mbeleni na wagonjwa.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo mtaalamu wa mimea kutoka Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam Bw. Frank Mbago ndiye aliyeutambua mmea huo ambao kule Samunge unaitwa  Mugarika au Engamuriaki kuwa kwa kitaalamu ni Carissa Spinarum ambao zamani kitaalamu uliitwa Carissa Edulis na unapatikana sehemu mbalimbali nchini na umekuwa ukitumiwa na makabila mbalimbali kama Wagogo, Wabarbergi, Wasonjo na Wakurya.

Wataalamu hao wanaripoti kuwa baada ya kuangalia kemikali mbalimbali zilizomo kwenye mmea huo ni wazi kuwa hauna sumu ambayo inaweza kumdhuru binadamu hasa kiwango kinachotakiwa kugeuza kemikali hizo kuwa sumu ni kubwa mno kulinganisha na kiasi kinachopatikana kwenye kikombe kimoja cha babu. “Matokeo yanaonesha kuwa dawa hii ni salama kwa kunywewa. Kiwango kinachotolewa na Mch. Ambilikile Mwasupile kwenye kikombe kimoja ni salama na haitarajiwi kusababisha kutumia dawa zaidi ya kiwango au kuwa sumu”.

Ikielezea sifa za kikemia za mmea huo kuhusiana na kutibu kifafa ripoti hiyo inasema kuwa baada ya uchunguzI wa kikemia mmea huo unaonesha kuwa na sifa za kutibu matatizo ya kifafa hasa katika uchunguzI wa kimaabara uliohusisha panya. Panya hutumiwa katika tafiti nyingi za kitaalamu za tiba kwa sababu utendaji kazi wa miili yao hufanana sana utendaji kazi wa miili ya binadamu na karibu vitu vyote ambavyo ni sumu kwa panya pia ni sumu kwa binadamu.

Kwa upande wa kutibu magonjwa ya kisukari ripoti hiyo ikitegemea ripoti nyingine ya wataalamu waliofanya utafiti mwaka 1996 inadai kuwa utafiti huo wa mwaka 1996 ambao nao pia ulihusisha panya wenye kisukari dawa hiyo ilionekana kurudisha kiwango cha sukari ndani ya masaa matatu tu baada ya kutumiwa. Kwa mujibu wa ripoti ya kina Mbwambo sifa hizo zinalingana na madawa ya kisukari yenye molekyuli za za biguanide kama ile ya Metformin ambayo hutumika kutibu dawa ya Kisukari Aina 2 (Type 2 Diabetes).

Kwa maoni ya wataalamu hao kutokana na sifa hizo “inaonesha kuwa carrisa edulis(mugariga) unasifa za kutibu magonjwa ya kisukari na hivyo unathibitisha madai ya Mchg. Mwasupile kuwa dawa yake inasaidia kudhibiti kisukari”.

Kwenye kupunguza shinikizo la moyo ripoti hiyo inaonesha kuwa kutoka na sifa za kitabibu ambazo ziligundulika mwaka 1963 mmea huo unazo kemikali ambazo zinasaidia kupunguza matatizo ya msukumo wa damu. Hivyo ripoti inasema kuwa “mmea huo una uwezo wa kupunguza msukumo mkubwa wa damu na hili linaonesha kukubaliana na madai ya Mch. Mwasupile kuwa dawa yake inasaidia kudhibiti msukumo wa damu”

Vile vile taarifa nyingine zilizopitiwa na wataalamu hao kuhusu uwezo wa kikemia wa mmea wa Mugariga ambao maelfu ya wananchi kutoka sehemu mbalimbali nchini wameenda kujaribu kutumia ili kutibu magonjwa mbalimbali zinaonesha kuwa pamoja na sifa hizo nyingine mmea huo unaonekana kusaidia kudhibiti magonjwa ya maini na hata kasarani. Ripoti hiyo inasema kuwa “matokeo mbalimbali yanaonesha kuwa mmea huo unasifa za kukinga magonjwa ya maini” pamoja na kuwa na sifa za kukinga magonjwa ya kasarani. Hili nalo linaonekana kukubaliana na madai ya kuwa dawa hiyo inasaidia kudhibiti magonjwa sugu kama ya kasarani.

Watu wengi hata hivyo walikuwa wanasubiri kujua kama dawa hiyo inasaidia kwa kiasi chochote kudhibiti au kutibu magonjwa yanayotokana na virusi mbalimbali vikiwemo virusi vyenye kusababisha ukosefu wa kinga mwilini na kusababishi UKIMWI. Katika taarifa yao hiyo wataalamu hao wakiangali taarifa mbalimbali wanadai kuwa mmea huo unaonekana kuwa na sifa za kikemia dhidi ya virusi (anti-viral activities).  “Dawa za mmea huo zikitumiwa katika viwango fulanifulani zinaonesha kuwa mmea huo una sifa dhidi ya virusi vya magonjwa ya polio na hata kaswende” inasema ripoti hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mmea huo unaonesha kuw ana nguvu sana dhidi ya magonjwa kama hayo ya kaswende ambayo ni mojawapo ya magonjwa yanayofungua njia ya maambukizi ya virusi vya UKIMWI. “Kutokana na nguvu yake hiyo kubwa kwa magonjwa kama kaswende mmea huo unaonekana kuwa na nguvu dhidi ya virusi” na hivyo kuonesha uwezo wake katika kudhibiti magonjwa kama ya UKIMWI.

Hata hivyo, ripoti hiyo haisemi moja kwa moja kuwa mmea huo unatibu kabisa virusi vya UKIMWI au magonjwa mengine yoyote yale zaidi ya kuonesha kuwa sifa zake za kutibu si za kukisia au kubuni na haionekani kama sifa hizo zinahusiana kwa namna yoyote na imani ya kishirikina bali kanuni zinazopimika za kisayansi.

Katika hitimisho lake ripoti hiyo inasema kuwa baada ya kuangalia taarifa mbalimbali za kisayansi na kuuangalia dawa inayotumika na Mchg. Mwasupile mambo kadhaa yanaweza kuhitimishwa.

Kwanza, dawa hiyo ni salama na kuwa kiwango kinachotumika hakiwezi chenyewe kuwa na madhara kwa binadamu kwani kinahitajika kiwango kikubwa sana kuweza kugeuza kikombe hicho kuwa sumu.

Pili, taarifa ambazo zimepatikana hadi sasa za sifa za kitabibu za mmea huo zinaonesha kukubaliana na madai ya Mchungaji Mwasupile kuwa dawa yake inasaidia katika kutibu na kudhibiti magonjwa ya kifafa, ya moyo, ya kisukari, ya maini na hata yale yanayohusiana na kasarani. Zaidi ya yote wataalamu hao walihitimisha kuwa ni kweli mmea huo unavyotumiwa na Babu husaidia katika kusaidia mashambulizi dhidi ya virusi mbalimbali.

Hata hivyo, uchunguzI wa wataalamu huo haukuhusisha moja kwa moja wagonjwa mbalimbali katika utafiti wa kisayansi kuona wagonjwa wanaendeleaje baada ya kutumia dawa hiyo kwani haikuwa sehemu ya jukumu lake. Kutokana na ukweli huo wataalamu hao wamependekeza hatua kadhaa za kuchukuliwa ili hatimaye kuwa na taarifa za uhakika zaidi juu ya uwezo wa dawa hiyo ili kuweza kujua kwa uhakika ni jinsi gani inaweza kutumika. Kwa vile dawa hiyo ina sifa hizo ndani yake ni wazi kuwa uwezo wake wa kutibu haufungamani pekee na kijiji cha Samunge au na Babu mwenyewe bali sifa zake haziwezi kubadilika hata zikitumiwa nje ya kijiji hicho. Hili linaweza kusababisha mmea huo kuanza kupandwa na kutumiwa sehemu mbalimbali.

Kutokana na ukweli huo wataalamu hao wanapendekeza kuwa utafiti wa kina wa tiba ufanyike ili kuweza kujua wagonjwa watumie kwa kiwango dawa hiyo ili kuendeleza unafuu wanaoupata. Hili ni muhimu kwani japo watu wengi wanapata kikombe kimoja na wanajisikia nafuu watu wengine wamejikuta wakipata matatizo baadaye hasa baada ya dawa hiyo kupungua mwilini. Endapo itaweza kuthibitishwa kiwango gani kinahitajika kutumika ili kuendeleza unafuu huo ni wazi kuwa dawa hiyo inaweza kutumika zaidi ya mara moja na kuwa na matokeo yale yale.

Wataalamu hao wanapendekeza utafiti huo ufanyike mapema ili kuweza kujua kile ambacho kinajulikana kama “kiwango cha juu” kutumika na mara ngapi kitumike na kwa kiasi gani. Hili ni muhimu kwa dawa yoyote inayotumiwa ili kuweza kuwa na kiwango kinachokubalika kutumika kwa wanadamu. Hivyo wanapendekeza utafiti huo ufanyike ili kuweza kujua kiwango kinachohitajika kwa wanadamu kuleta unafuu au tiba.

Hata hivyo taarifa hiyo iliacha kuangalia masuala ya kiimani kwani eneo hilo ni wazi haliangukii mikononi mwa wigo wa sayansi. Pamoja na kutofanya hivyo ni wazi kuwa sifa za kikemia za mmea huo zipo na ni kweli zinasaidia kutibu na kudhibiti magonjwa mbalimbali. Jukumu kubwa lililoko mbeleni ni kuona ni jinsi gani mmea huo unaweza kuingizwa katika tiba za magonjwa mbalimbali na kuwasaidia maelfu ya wananchi wenye kusumbuliwa na magonjwa sugu ambayo yameshindikana kudhibitiwa au kutibiwa na tiba ambazo tayari ziko sokoni.

Changamoto kubwa ambayo inaonekana kuachwa kwa watafiti wengine na vyombo vyetu vya kisayansi ni kuweza kuelewa zaidi ufanyaji kazi wa dawa zilizomo katika mmea huo kwani pamoja na yote yaliyotajwa katika taarifa hiyo haisemwi moja kwa moja kuwa mmea huo unatibu kabisa magonjwa hayo zaidi ya kuonekana una uwezo wa kudhibiti magonjwa na kuleta unafuu. Ni kwa sababu hiyo ushauri unaotolewa na wataalamu mbalimbali kuwa wagonjwa wasiache kutumia madawa yaliyokwisha kuthibitishwa kutibu au kudhibiti magonjwa kadha wa kadha kuzingatiwa na kuendelea kutiiliwa maanani.

Wakati huo huo waraka mfupi ambao unaonekana kutolewa na serikali ya Marekani kupitia Ubalozi wake Jijini Dar-es-Salaam siku ya Jumatano umetoa wasia kwa wagonjwa ambao wanatumia tiba za jadi kutoacha kutumia dawa ambazo wamekuwa wakitumia kwa magonjwa mbalimbali. Waraka huo mfupi unasema kuwa “Serikali ya Marekani inawasihi Watanzania wenye kutumia dawa za jadi na za ziada kutoacha kutumia dawa ambazo wamekuwa wakizitumia ili wasije wakasababisha vijidudu vya magonjwa kutengeneza ubutu wa kutoweza kutibika tena”.

Pamoja na hilo taarifa hiyo hiyo imewataka watu kuacha tabia ambazo zinaweza kuwasababisha maambukizi zaidi na hivyo waendelee kujikinga wao na familia zao.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *