JUMLA ya kaya 12I katika kitongoji cha Kabayondo Kata ya Kabirizi wilayani Muleba,zinatoa taswira ya hali mbaya ya uchumi wa mkoa wa Kagera ambao uko nafasi ya 19 kwa kuwa na pato dogo la mwananchi.
Pia mikoa ya Kigoma,Shinyanga,Dodoma na Singida wakazi wa mikoa hiyo wanakabiliwa na umasikini mkubwa wa kuwa na pato dogo,mikoa ambayo pia inashika nafasi za mwisho kwa kipindi kirefu kama ulivyo mkoa wa Kagera.
Miaka kumi iliyopita ulikuwa kati ya mikoa kumi bora kwa wastani mzuri wa pato la mwananchi.Taasisi ya Taifa ya Takwimu(NBS)inaonyesha mwaka 2009 wastani wa pato la mwananchi wa Kagera ulikuwa shilingi 483,158 wakati wastani wa kitaifa ni shilingi 693,470 kwa mwaka.
Wakazi wa kitongoji hiki hawajui chanzo cha kuwa taabani kiuchumi wala hakuna mwenye uhakika na mlo wa kila siku.Mwenyekiti wa kitongoji hiki Trazias Daud anasema hali ni mbaya akilinganisha na miaka michache iliyopita.Kwa vyovyote vile ni vigumu kuipata familia iliyopata kitoweo cha nyama kwa miezi sita iliyopita!
Wakazi wote katika kitongoji hiki wanategemea kilimo cha kujikimu kwa kutumia jembe la mkono.Uzalishaji unapungua kila mwaka badala ya kuongezeka na hawawezi kupata mavuno ya ziada.
Matatizo ya kiuchumi yanayoukabiri mkoa wa Kagera yana uhusiano na ongezeko kubwa la idadi ya watu lisilokwenda sambamba na shughuli za uzalishaji,hasa katika sekta ya kilimo.
Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi mwaka 2002 mkoa ulikuwa na watu 2,033,888 huku ikikadiriwa ifikapo mwaka 2011 mkoa utakuwa na watu 2,746,058.Sensa ya mwaka 1967 mkoa wa Kagera ulikuwa na watu 658,712.
Ukuaji wa idadi ya watu unaongeza matumizi huku vijana ambao ni idadi kubwa wakitegemewa kuanzisha familia.Mfumo wa jamii umewajengea utamaduni wa kusubiri kurithi mashamba ya wazazi bila kufungua mashamba mapya.
Vijana ambao ndiyo nguvu kazi hawana ardhi ya kulima hali ambayo imewafanya kugeuka wachuuzi kupitia biashara ndondogo ambazo hazileti mabadiliko makubwa ya kiuchumi katika familia zao.
Katika familia ndogo mapato hugawanywa kwa wachache na kumwezesha kila mmoja kupata rasilimali zaidi.Kuongezeka kwa migogoro ya ardhi mkoani Kagera ni dalili ya ukuaji wa watu unaofanya mahitaji kuongezeka.
Takribani katika wilaya zote za mkoa wa Kagera inatajwa kuwepo kwa ongezeko kubwa la migogoro ya ardhi hali inayoweza kuhusishwa na ongezeko la watu linalofanya mahitaji ya raslimali hiyo kuwa kubwa.
Kuna uhusiano mkubwa kati ya idadi ya watu na maendeleo na kwa muda mfupi ni vigumu kupima athari za ukuaji wa watu ambazo hujitokeza baadaye katika sura tofauti kwenye jamii.
Mathalani uzazi wa kiwango cha juu unazuia fursa za watoto kupata elimu katika familia masikini.Uzazi wa mpango huwawezesha wanawake kushiriki shughuli za kiuchumi na hivyo kuongeza pato la familia.
Kwa mujibu wa utafiti wa bajeti ya kaya wa mwaka 2001,uliofanywa na Wizara ya Mipango Uchumi na Uwezeshaji familia zinazotegemea kilimo cha kujikimu zina kiwango cha juu cha umasikini.
Hali ni mbaya zaidi kwa familia zenye watu wengi wasio na shughuli za kiuchumi na haziwezi kupiga hatua zaidi pale kiongozi wa kaya anapokuwa hana hata elimu ya msingi.
Sio rahisi kuongeza pato la mwananchi wa mkoa wa Kagera bila kutekeleza mikakati ya kupunguza kiwango cha uzazi na kuongeza uzalishaji.
Mkoa wa Kagera una hekta 1,593,758 zinazofaa kwa kilimo na mkoa pekee unaopakana na nchi za Uganda,Rwanda na Burundi ambazo ni wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.Hata hivyo eneo linalolimwa ni hekta 674,174.
Hizi ni miongoni mwa fursa kubwa zilizopo mkoani Kagera ambazo hazijatumika ipasavyo kupunguza umasikini.Hata hivyo wafanyabiashara wengi hawanalamikia vikwazo vingi vya kupata vibali vya kusafirisha bidhaa nchi jirani, tofauti na nchi nyingine wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mwisho
Picha.Wanafunzi wa shule ya msingi Kumubuga kata ya Mulusagamba wilayani Ngara ambao hali yao inaakisi hali ya umasikini katika familia wanazotoka
2.Balozi wa Jumuiya ya Ulaya Tim Clarke kushoto akiwa katika shamba la miwa la kiwanda cha sukari cha Kagera ambapo uwekezaji kama huu haujasaidia kuinua hali ya maisha ya wananchi wa mkoa huu.