Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali, Mohamed Mchengerwa ameitaka ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kuvifuta vyama vya siasa vinavyodaiwa kukiuka sheria na taratibu za kuendesha shughuli za kisiasa nchini.
Kauli hiyo imetolewa Bungeni wakati wa uwasilishaji wa bajeti ya ofisi ya Waziri Mkuu ya mwaka 2018/2019, ambapo ni mapendekezo ya kamati kuhakikisha vyama vya siasa vinatekeleza wajibu wao uliopo kikatiba na sheria.
“Ofisi ya Msajili ihakikishe kunakuwa na usimamizi wa karibu kwa kufuatilia na kuchunguza mienendo inayoharibu sifa na vigezo vya vyama vya siasa nchini na kwamba msajili asisite kukifutia usajili chama chochote cha siasa kitakachokiuka kanuni, sheria na taratibu za uendeshaji wa vyama vya siasa hapa nchini”, alisema Mchengerwa ambaye ni mbunge wa Rufiji mkoani Pwani.
Hakuishia hapo, lakini ameitaka ofisi ya msajili wa vyama vya siasa kuvifuta vyama vyote vinatumia vibaya ruzuku inayotolewa na Serikali ili kuwa fundisho kwa vyama vingine vinavyokiuka misingi ya matumizi ya rasilimali za umma.
Kwa wadadisi wa masuala ya kisiasa wanapatwa na wasiwasi juu ya ushauri huo wa kamati wa kufuta baadhi ya vyama vya siasa kwa makosa ambayo yanaweza kujadiliwa na vyama hivyo vikaendelea na shughuli zao.
Inaelezwa kuwa vitisho na adhabu dhidi ya vyama vya siasa nchini sio njia pekee ya kustawisha demokrasia ya vyama vingi nchini. Kauli hizo za viongozi hasa kutoka chama tawala zinadaiwa kuwa ni mkakati wa kuzoofisha nguvu ya vyama vya upinzani ambavyo vinatoa ushindani kwa viongozi waliopo madarakani.
Tangu kuingia madarakani kwa Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais John Magufuli, uhuru wa vyama vya siasa hasa vya upinzani kutimiza majukumu yao ya kisheria umepungua kutokana na baadhi ya matukio yasiyo ya kawaida ambayo hayakushuhudiwa katika awamu za Serikali zilizopita.
Bendera za vyama vya siasa zikipepea katika eneo la Ubungo, Dar es Salaam wakati wa uchaguzi mkuu 2015
Kuzuiwa kwa mikutano ya kisiasa na maandamano
Mwaka 2016 Serikali ilizuia mikutano yote ya wazi ya vyama vya siasa mpaka 2020, kwa madai kuwa wakati wa kufanya kampeni na siasa za majukwaani umeisha na wananchi wanatakiwa kufanya kazi kwa bidii ili kuinua uchumi wa nchi ikizingatiwa kuwa Serikali inatekeleza sera ya uchumi wa viwanda.
Lakini zuio hilo lilienda mbali zaidi hadi kupiga marufuku maandamano na mikutano ya ndani ya vyama vya siasa isipokuwa pale wahusika wanapokuwa wamepata kibali kutoka Jeshi la Polisi. Matukio kama haya yamekuwa yakilalamikiwa na wadau wa siasa kuwa ni njia ya kuminya uhuru wa kujieleza na kuikosoa Serikali pale inapokosea.
Mara kadhaa, Serikali kupitia Jeshi la Polisi imekuwa ikizuia vibali vya maandamano kwasababu mbalimbali ikiwemo ukosefu wa usalama, jambo ambalo linakiuka matakwa ya katiba na sheria ambayo yanatoa uhuru wa watu kukusanyika na kutoa maoni yao.
Mnamo Machi 9 mwaka huu, akiwa mjini Chato mkoani Geita, Rais Magufuli aliendelea kusisitiza msimamo wa Serikali wa kuzuia shughuli za kisiasa na kutoa tahadhari kuwa Serikali yake haitasita kumchukulia hatua mtu yoyote atakayejaribu kuandamana.
“Wapo watu ambao wameshindwa kufanya siasa za kweli wangependa kila siku tuwe mabarabarani tunaandamana. Watu hao wanahamia huku wao wanataka wabaki wanaandamana kule,
“Nimeshasema ngoja waandamane wataniona. Kama kuna baba zao wanawatuma, watakwenda kuwasimulia vizuri. Niliapa kwa Katiba kwamba nchi hii lazima iwe ya amani”, alinukuliwa Rais Magufuli.
Katiba na sheria zinasemaje?
Shughuli za kisiasa ikiwemo mikutano na maandamano yanatambulika na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo katika Ibara ya 20 (1) inasema, kila mtu anao uhuru wa kukutana na watu wengine kwa hiari yake na kwa amani, kuchanganyika, kushirikiana na watu wengine.
Kwa muktadha huo, kukutana na kuchanganyika ni sehemu ya shughuli za vyama vya siasa ambayo watu wanaelezea fikra na maoni yao juu ya jambo lolote lile kwa masharti ya kulinda amani na sheria za nchi.
Shughuli za kisiasa zinaenda sambamba na uhuru wa kujieleza na kwa mujibu wa Katiba ya mwaka 1977 ibara ya 18 (a), kila mtu ana uhuru wa kuwa na maoni na kueleza fikra zake.
Kadhalika, Sheria ya vyama vya siasa ya mwaka 2002 ibara ya 11 inatambua maandamano na mikusanyiko kama sehemu ya Demokrasia na watu kufurahia uhuru wao bila kuingilia na mamlaka yoyote.
Sambamba na hilo Mikataba ya kimataifa ambayo Tanzania imeridhia inatoa jukwaa (Civic Space) la watu kukusanyika kutoa maoni au kuelezea yale wanayoyaamini bila kutishwa au kuzuiwa kwa namna yoyote ile ambapo vyama vya siasa vina nafasi yake.
Lakini misingi hiyo inazingatiwa?
Licha ya Katiba na Sheria kufafanua haki za msingi za vyama vya siasa, bado hali ya utendaji wa vyama hivyo nchini siyo ya kuridhisha. Na wanasiasa wanaojaribu kutekeleza haki zao wamekuwa wakikabiliwa na vitisho, adhabu na vifungo.
Hivi karibuni, Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (Sugu) alihukumiwa kwenda jela kifungo cha miezi sita kwa kile kinachotajwa kutoa kauli ya ‘uchochezi’ dhidi ya Rais katika moja ya mikutano ya kisiasa iliyofanyika katika jimbo lake mapema mwaka huu.
Pia viongozi 7 waandamizi wa chama cha upinzania CHADEMA wakiongozwa na Mwenyekiti wao, Freeman Mbowe wiki hii walifikishwa Mahakamani kwa kosa la kuandamana bila kibali mnamo Februari 17, 2018 wakati wakienda kwa Msimamizi wa Jimbo la Kinondoni kudai hati za viapo za mawakala wao.
Katika maandamano hayo alifariki mwanafunzi mmoja wa Chuo Cha Taifa Cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akiline kwa kupigwa risasi wakati polisi wakiwatawanya wafuasi wa CHADEMA.
Kutokana na maandamano hayo, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi aliiandikia CHADEMA barua ya kujieleza kwanini wasipewe adhabu kutokana na kukiuka sheria inayowakataza kuandamana bila kibali na kusababisha taharuki katika jamii.
Kimsingi Msajili ni mlezi wa vyama vya siasa ambaye wakati wote anapaswa kuwa mtetezi na mlinzi wa vyama hivyo dhidi ya hatari yoyote ile inayonuia kuvidhoofisha visitimize majukumu yake.
Sambamba na hilo tayari, Serikali imeanza mchakato wa kuifanyia marekebisho sheria ya vyama vya siasa ya mwaka 2002, ambapo katika Rasimu iliyotolewa kipengele kimojawapo kinazuia kufanyika kwa mikutano ya kisiasa isipokuwa tu wakati wa uchaguzi.
Matukio haya yanaweza kuashiria kuwa mfumo wa vyama vingi nchini Tanzania unapitia kipindi kigumu na kama hatua muhimu hazitachukuliwa kuturejesha katika misingi tuliyojiwekea, uwezekano wa vyama vingi kupotea ni mkubwa. Na kitachofuata ni kurudi kwenye utawala wa kiimla unaongozwa na viongozi wanaofuata nadharia za ‘kidikekta’.
Tunahitaji mjadala wa kitaifa, kutathmini ni wapi tumekosea au ni mfumo upi wa uongozi unatufaa watanzania kwa siku zijazo.