Utata wa vijana wanaoacha fursa za uzalishaji vijijini na kwenda mjini

Jamii Africa

Ripoti ya shirika la Chakula Dunia (FA0-2017) imeeleza kuwa ili Tanzania na nchi nyingine za Afrika zikamilishe Malengo Endelevu ya 2030 wanashauri kuzigeukia jamii za watu wanaoishi vijijini kwa kuboresha mfumo wa uzalishaji mazao ya kilimo.

Rai ya FAO inatokana na ukweli kuwa  shughuli nyingi za kilimo zinafanywa na wananchi wanaoishi vijijini ambao wanapaswa kujengewa uwezo wa kiujuzi na teknolojia ili kuongeza uzalishaji wa mazao na kukuza uchumi wa kaya.

Ikiwa Tanzania itafanikiwa kufanya mapinduzi ya kilimo vijijini ni dhahiri itachochea maendeleo ya viwanda na kutengeneza ajira nyingi kwa vijan.

 

Lakini ipo changamoto kubwa…

Licha ya kuwepo kwa mikakati ya kuzikwamua jamii za watu waishio vijijini kutoka kwenye umasikini lakini zinakwamishwa na ongezeko kubwa la idadi ya watu hasa vijana.  

Kulingana na ripoti ya FAO inaeleza kuwa kati ya mwaka 2015 na 2030, idadi jumuishi ya wakazi wa Afrika na Asia inatarajiwa kuongezeka kutoka bilioni 5.6 hadi zaidi ya bilioni 6.6.

Inabainisha kuwa katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara, idadi ya vijana walio na umri wa miaka kati ya 15 na 24 inatarajiwa kuongezeka kwa zaidi ya bilioni 90 ifikapo 2030, na idadi hiyo itakuwa maeneo ya vijijini.

Ongezeko  la vijana linaweza kutengeneza changamoto kubwa ya ukosefu wa ajira kwa karne zijazo. Kwasababu kuna uzalishaji mdogo kwenye sekta ya kilimo na viwanda, vijana wengi watapambana kutafuta ajira; matokeo yake na wale wanaokimbia kutoka vijijini kwenda mjini wataongeza na kuzidisha umasikini katika maeneo hayo.

                                                                      Wakulima wakipalilia maharage

 

Nini kifanyike?

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, FAO inashauri kuwa, ikiwa wananchi waishio vijijini wanataka kuondokana na umasikini ni muhimu kubaki katika maeneo yao kuliko kwenda mjini. Maamuzi hayo lazima yaende sambamba na mabadiliko ya sera zinazosimamia kilimo na kuongeza uwekezaji wa teknolojia utakaowawezesha vijana kulima kilimo cha kisasa.

Wakulima wa vijijini hawana soko la uhakika la mazao yao na mfumo thabiti wa uzalishaji unaounganishwa na ukuaji wa viwanda vya uzalishaji wa bidhaa za kilimo.

Mshauri na Mtaalamu wa maswala ya Biashara na Maendeleo kutoka taasisi ya Small Starter, John-Paul Iwouha ameshauri kuwa, licha ya  maendeleo ya viwanda katika bara la Afrika kwenda taratibu, mabadiliko vijijini yanaweza kufanyika kwa kuinua mfumo wa uzalishaji chakula ili kufikia mahitaji ya wakazi waishio mjini

Amesema, “Lengo ni kuboresha mfumo wa chakula na kutengeneza fursa mpya za uchumi kwenye shughuli za kilimo ikiwemo kilimo cha biashara, uchakataji, usindikaji, usambazaji na utunzaji. Kuongezeka kwa mahitaji ya soko la vyakula kutoka mjini inatarajiwa kuwa kichocheo kikubwa cha mabadiliko vijijini”.

Hata hivyo, fursa hiyo kwa wananchi wa vijijini bado ina changamoto ikizingatiwa kuwa itahusisha kuwatoa wakulima kwenye kilimo cha jembe la mkono hadi kwenye mashamba makubwa (large plantation) ambapo kuna uwezekano wa wakulima hao kuwekwa pembeni.

Iwouha amesema ili kuhakikisha mabadiliko hayo yanamnufaisha kila mwananchi, watunga sera na serikali wanapaswa kuelewa utendaji jumuishi wa jamii na uchumi wa miji, majiji na maeneo ya vijijini na jinsi unavyoweza kuimarisha mfumo wa uzalishaji chakula bila kuwaathiri wakulima wadogo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *