Daniel Samson
Utunzaji wa mazingira ni wajibu wa kila mwananchi ili kuhakikisha shughuli za kibinadamu zinaratibiwa vizuri na kuifanya dunia kuwa sehemu nzuri ya kuishi. Utunzaji wa mazingira ni pamoja na kupanda miti na kuhifadhi uoto wa asili uliopo katika maeneo mbalimbali nchini.
Kwa kutambua hilo, serikali kupitia Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, January Makamba amesema ili kupunguza matukio ya ukataji wa miti kwa ajili kutengeneza mkaa, serikali inaendelea na mikakati ya kuwaelimisha wananchi juu ya matumizi ya teknolojia ya nishati mbadala ambayo ni rahisi na yenye uhakika.
Akiongea katika kipindi cha Njoo Tuongee kinachorushwa na kituo cha runinga cha Star TV nchini kwa ushirikiano wa shirika la Twaweza na JamiiForums amesema, “Moja ya mambo ambayo yanaweza kusaidia kupunguza uharibifu wa mazingira ni matumizi ya teknolojia hasa ya nishati ya jua au teknolojia ya kusambaza gesi ya kupikia kwa urahisi ni kupunguza ukataji wa miti”.
Tanzania ni miongoni mwa nchi za Afrika ambazo zinashika kasi katika ukataji wa miti kwa ajili ya mkaa unaotumika maeneo mbalimbali ya uzalishaji na nyumbani. Hali hiyo inatishia nchi kuwa jangwa na kuathiri mfumo mzima wa hali ya hewa ikiwemo upatikanaji wa mvua kwa ajili ya shughuli za kilimo na mifugo.
Takwimu za Shirika la Uangalizi wa Misitu Duniani (Global Forest Watch-2016) zinaonyesha kuwa kuanzia mwaka 2001 hadi 2016 Tanzania imepoteza hekali 1,999,704 za miti na hali hiyo isipodhibitiwa ukataji wa miti utaongezeka kwa kasi.
Waziri Makamba ameeleza kuwa teknolojia ya nishati mbadala ni njia sahihi ya kupunguza tatizo la ukataji miti kwasababu imefanyiwa utafiti na kuonyesha matokeo chanya katika maeneo mbalimbali duniani.
“Teknolojia ni jawabu la uhifadhi wa mazingira, huo ni mwanzo tu wa utafiti wa utumiaji na usambazaji wa teknolojia”, amesema Waziri Makamba.
Ili kuhakikisha suala la mazingira linapata nguvu ya kisheria, serikali inaifanyia marekebisho Sera ya Mazingira ya mwaka 1997 ambayo imepitwa na wakati. Katika Sera mpya wataweka vichocheo vya teknolojia ya utunzaji wa mazingira ili kuhakikisha kila mwananchi anakuwa sehemu ya kutunza mazingira kwa maendeleo endelevu.
“Sera tuliyonayo ya Mazingira ni ya mwaka 1997 imepitwa na wakati na sera hiyo haitaji hata mabadiliko ya tabia nchi. Katika sera mpya tunayoandika tunaweka vichocheo vya matumizi ya teknolojia rafiki katika uzalishaji viwandani na nishati ambazo tunatumia kupikia na kwa matumizi mengineyo”.
“Kwa kushirikiana na wenzetu Wizara ya Fedha kuona kwa kiasi gani tunaweza kurahisisha uingizaji, uagizwaji na uhamishaji wa teknolojia ambazo tayari wenzetu wanazitumia ili ziweze kutumika na hapa vilevile. Lakini kuwezesha tafiti kwenye vyuo vyetu na taasisi za elimu ya juu wazingatie teknolojia rafiki kwa mazingira”, anaeleza Waziri Makamba.
Hali Halisi ya Ukataji wa Miti
Kulingana na Benki ya Dunia (WB) inaelezwa kuwa ardhi yenye misitu nchini Tanzania inapungua kila mwaka. Mathalani mwaka 1990 ardhi yenye misitu ilikuwa asilimia 63 ya ardhi yote lakini kutokana na ongezeko la watu na shughuli za kibinadamu ardhi hiyo imepungua hadi kufikia asilimia 52 mwaka 2015.
Takwimu hizo zinaiweka Tanzania katika nafsi ya juu katika nchi za Afrika kwa matumizi ya mkaa na kuni ambazo hukatwa kwa matumizi mbalimbali ya nyumbani na viwandani.
“Kwa Tanzania matumizi ya mkaa kwa mwaka ni tani milioni 1, usambazaji wa mbao kwa mwaka zinazohitajika kufikia mahitaji hayo ni milioni 30 ujazo wa mita. Katika baadhi ya maeneo nchi, hasa maeneo ya mijini, uzalishaji wa mkaa unasababisha uharibifu wa ardhi yenye miti”, inaeleza ripoti ya Benki ya Dunia.
Nishati ambazo zinatumika katika maeneo ya vijijini na mijini kwa kupikia ni gesi, mkaa, kuni, mafuta ya taa na umeme. Lakini mkaa unaongoza kutumiwa kuliko nishati nyingine huku Dar es Salaam ikiongoza kwa maeneo ya mijini.
Mkaa huo ambao huzalishwa katika misitu iliyopo pembezoni mwa nchi husafirishwa hadi mjini ambako idadi kubwa ya watu wenye kipato cha juu wanaishi. Watu ambao wameelimika bado wako katika kundi la watu ambao wanatumia zaidi mkaa katika shughuli zao ikilinganishwa na watu masikini wasio soma ambao wao wanatumia zaidi kuni.
Kutokana na athari za ukataji wa miti katika maeneo mbalimbali duniani, Tanzania tunapaswa kuchukua tahadhari na kujikita katika matumizi ya nishati mbadala ikiwemo gesi ambayo inapatikana kwa wingi nchini.