Baadhi ya viongozi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wamewasili kwa mahojiano katika Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam kufuatia wito wa Jeshi la Polisi uliotolewa siku ya jana.
Kwa mujibu wa taarifa ya Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa CHADEMA, John Mrema ilisema kwamba walipokea barua kutoka kwa Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalam Dar es Salaam iliyoelekezwa kwa Mwanasheria, Makao Makuu ikiwataka viongozi waandamizi wa chama hicho kufika polisi kwa mahojiano jana saa 11 jioni.
Waliotakiwa kufika ni Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, Dkt. Vicent Mashinji ( Katibu Mkuu), Salum Mwalim (Naibu Katibu Mkuu Zanzibar), John Mnyika (Naibu Katibu Mkuu Bara). Wengine ni Halima Mdee (Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Taifa-BAWACHA), John Heche (Mbunge wa Tarime Vijijini) na Ester Matiko (Mweka Hazina wa Baraza la Wanawake Taifa- BAWACHA).
Lakini taarifa ilizopata Fikra Pevu zinasema waliofika polisi ni viongozi wanne tu ambao ni Halima Mdee, John Mnyika, John Heche na Ester Matiko ambapo baada ya kuhojiwa wameachiwa na watakakiwa kuripoti Februari 27 mwaka huu.
Aidha, wito huo unakuja siku nne tangu kutokea kwa kifo cha mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini ambaye aliuwawa akiwa ndani ya daladala eneo la Mkwajuni, Kinondoni jijini Dar es Salaam wakati polisi wakiwatawanya waaandamanaji na wafuasi wa CHADEMA waliokuwa wanakwenda ofisi za Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kinondoni kudai viapo vya mawakala wao.
Fikra Pevu ilitaka kujua sababu za viongozi wengine 3 kutokwenda polisi kwa mahojiano ambapo kiongozi mmoja wa ngazi ya juu wa CHADEMA amesema viongozi hao wamepata udhuru na jitihada za kuhakikisha wanaripoti polisi zinaendelea.
Amesema Katibu Mkuu, Dkt. Vicent Mashinji yuko safarini nchini Marekani kwa shughuli za kikazi ambapo Freeman Mbowe na Salum Mwalim nao wako safarini.
Inaelezwa kuwa sababu kubwa ya viongozi kuitwa kwa mahojiano ni kujibu mashtaka ya kufanya maandamano kinyume na sheria siku ya 16 Februari mwaka huu. Na wanashtakiwa chini ya kifungu cha 10 (2) na 10 (2A) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ambapo jalada lenye namba OB/IR/1467/2018 limefunguliwa.
Maandamano ya Chadema
Siku moja kabla ya kufanyika uchaguzi wa marudio katika jimbo la Kinondoni baada ya viongozi kufunga kampeni katika kata ya Mwananyamala, waliandamana kuelekea ofisi ya Mkurugenzi wa Kinondoni kudai viapo vya mawakala wa uchaguzi uliofanyika jumamosi ya 17 Februari 2018.
Lakini walipofika eneo la Mkwajuni Kinondoni walidhibitiwa na polisi. Polisi walilazimika kutumia silaha na kuwatawanya wafuasi wa CHADEMA ambapo kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa risasi moja ilimpata mtu (Akwilina) aliyekuwa kwenye daladala.
Akwilina alifariki na kupelekwa hospitali ya Mwananyamala na tayari Jeshi la Polisi linawashikilia askari 3 kwa kusababisha kifo cha marehemu.
Bajeti ya Mazishi
Kufuatia kifo cha mwanafunzi huyo, serikali kupitia waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako imesikitishwa na mauaji hayo na iliahidi kubeba gharama zote za mazishi.
Siku moja baadaye, Familia ya marehemu Akwilina imewasilisha serikalini bajeti ya milioni 80 kwa ajili ya shughuli ya mazishi na kuaga mwili wa marehemu 22 Februari, 2018 jijini Dar es Salaam na kisha kusafirishwa hadi wilaya ya Rombo, Kilimanjaro ambako marehemu atapumzishwa.
Msemaji wa familia, Festo Kavishe amesema wamefikia uamuzi wa kutengeneza bajeti hiyo kutokana na serikali kuwataka wawasilishe bajeti yao kwa wizara ya Elimu.
Katika hatua nyingine familia hiyo imetahadharisha watu wanaochangisha fedha kwa njia ya mtandao kwa ajili ya rambirambi za msiba kuacha kufanya hivyo na ikiwa wana nia hiyo wawasiliane na familia hiyo.