WAFANYABIASHARA wadogowadogo, maarufu kwa jina la ‘machinga’ wanaendelea kuumizwa na utofauti wa kauli na maagizo yanayotolewa na viongozi wa serikali nchini kuhusu kuondolewa maeneo ya katikati ya miji na kupelekwa pembezoni.
Licha ya kauli ya Rais John Magufuli, katika ziara yake jijini Mwanza Agosti 11 mwaka huu, ya kutengua agizo lililokuwepo kwa baadhi ya mikoa kuwaondoa machinga katikati ya miji, baadhi ya mikoa haikutii kauli hiyo ukiwemo Mkoa wa Mwanza.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, mkoa wa Mwanza umetekeleza uondoshwaji wa machinga kwa nguvu. Uongozi wa mkoa huo wa Kanda ya Ziwa Viktoria, umetumia njia ya bomoabomoa iliyofanywa na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na mgambo.
Hatua hiyo inadaiwa imetokana na machinga kukaidi kuondoka kwa hiari, kwani walisimamia agizo la Rais Maguguli na sio masharti ya viongozi wa mkoa na wilaya.
Kitendo hiki cha kuondolewa kwa nguvu mwishoni mwa wiki, kimesababisha kupoteza mali zao huku vibanda vingine vikibomolewa bila utaratibu wowote.
Hali hii imewatia hofu machinga na kutoa malalamiko yao kuhusu kauli za viongozi wao zinavyowachanganya kutokana na kutofautiana juu ya hili.
Lakini, baada ya siku tatu tangu kuondolewa kwa wafanyabiashara wadogo wa Mwanza ndani ya maeneo ya Makoroboi, Liberty, Sahara, Mtaa wa Soko Kuu na Tanganyika, Rais Magufuli amewaagiza Waziri na Katibu Mkuu – Ofisi za Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kusitisha mara moja zoezi la kuwaondoa hadi mamlaka husika itakapoamua sehemu za kuwapeleka, huku ikiwashirikisha machinga wenyewe katika uamuzi huo.
Aidha, katika agizo lake, Rais Magufuli amewaonya wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi wanaowafukuza machinga bila kuwapa maeneo mengine yanayofikiwa kirahisi na wateja.
Ikumbukwe kwamba awali katika ziara yake, akiwa Mwanza, Agosti mwaka huu, Rais Magufuli, alitoa agizo kwa viongozi wote; mikoa, wilaya, manispaa na wakurugenzi miji na majiji, kutowapeleka machinga nje ya miji na badala yake kuweka mikakati ya kuwatengea maeneo ndani ya miji hiyo.
“Ni lazima tujenge mazingira ya watu wote; awe tajiri au masikini, kila mmoja anataka afanye biashara katikati ya mji, lakini pia unapofanya biashara ni lazima ufanye biashara yenye kuleta mapato…
Kila mmoja ana haki ya kuishi mahali pazuri, kila mmoja ana haki ya kufanya biashara mahali panapouza,” hii ni kati ya kauli zake dhidi ya kuondolewa mijini kwa wamachinga.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella, alinukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari akidai kuwa, machinga katika mkoa huo, wamekuwa wakifanya biashara zao bila kufuata kanuni na sheria zilizopo, hivyo ndicho kigezo cha kumpa mamlaka mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Mary Tesha kuhakikisha anasimamia zoezi la kuwaondoa wafanyabiashara hao.
Mkakati huu wa kuwaondoa machinga sio wa Mwanza pekee, bali umeshamili nchini kote unaojulikana kama mkakati wa ‘Safisha Jiji’ uliopitishwa na serikali, kwa lengo la wafanyabiashara hawa kupisha maeneo ya mjini na kutafutiwa maeneo mengine ya kwenda.
Matamko haya ya viongozi kutofautiana yanaleta maumivu kwa wafanyabiashara hawa kwani kila sehemu, kila kiongozi anatoa kauli jinsi anavyoamua. Utofauti huu unasababisha kuondolewa kwa nguvu machinga na baada ya agizo la raisi kutolewa, sasa wanarudi tena katika maeneo waliyofukuzwa.
Julai mwaka huu, Fikrapevu imeshuhudia baadhi ya machinga jijini Dar es salaam maeneo ya Kariakoo Mtaa wa Congo, Dar es Salaam, wakikamatwa kwa kulazimishwa kuhamia maeneo mapya ya kufanyia biashara na kutoka maeneo yaliyozoeleka kwa muda mrefu.
Wafanyabiasha wamekuwa wakipinga maagizo ya viongozi wao ya kuwataka kuhamia sehemu mpya wanazotengewa kwa kudai maeneo hayo hayana msisimko wa kibiashara na watu hawajayazoea, na hawatawafuata huko, hivyo itakuwa changamoto kwao kufanya biashara.
Hivyo basi, viongozi wanapaswa kuwa na kauli moja kabla ya kutoa uamuzi juu ya jambo husika ili kuondoa maumivu kwa wafanyabiashara hawa wanaotafuta maisha kwa njia halali.
Mbali na matamko hayo kuwaathiri machinga, pia serikali yenyewe inapata hasara kwani huingia gharama wakati wa utekelezaji wa matukio hayo ya kuwafukuza machinga.