KAMATI ya Saa 72 ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imeilima faini Yanga ya jumla ya Shs. 5 milioni kutokana na vitendo visivyo vya kiungwana michezoni, ikiwemo kutumia milango isiyo rasmi uwanjani, kugoma kuingia vyumbani na kugoma kusalimiana na wachezaji wa timu pinzani.
Taarifa ambayo FikraPevu imeipata kutoka TFF imeeleza kwamba, mbali ya Yanga, timu za Mbeya City, Mbao FC na Maji Maji nazo zimelimwa faini kwa vitendo kama hivyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Yanga imepigwa faini ya Shs. 1,000,000 (milioni moja) kutokana na timu hiyo kutoingia vyumbani wakati wa mechi namba 206 dhidi ya Toto African iliyochezwa Mei 9, 2017 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ambayo Yanga ilishinda 1-0.
Taarifa hiyo imesema, adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 14(48) ya Ligi Kuu ambapo uamuzi huo umezingatia pia kuwa Yanga imekuwa ikirudia kosa hilo mara kwa mara.
Katika mechi namba 231 ambayo Yanga ilishinda 2-1 dhidi ya Mbeya City Mei 13, 2017, timu zote mbili hazikupita kwenye mlango rasmi wakati wa kuingia uwanjani kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Yanga na Mbeya City
Hatua hiyo imefanya TFF kuzipiga faini ya Shs. 500,000 kila moja, uamuzi ambao pia umezingatia Kanuni ya 14(48).
Aidha, kwa kuzingatia kanuni hiyo hiyo, klabu ya Yanga pia imepigwa faini ya Sha. 1,000,000 (milioni moja) kwa kutoingia vyumbani kwenye mechi hiyo.
Katika taarifa hiyo ya TFF, imeelezwa pia kwamba, Yanga imepigwa jumla ya Shs. 3 milioni kwa vitendo visivyo vya kiungwana ilivyovionyesha kwenye mechi ya kufunga pazia la Ligi Kuu dhidi ya Mbao FC jijini Mwanza ambapo mabingwa hao walifungwa bao 1-0.
Katika mechi hiyo iliyochezwa Uwanja wa CCM Kirumba Mei 20, 2017, Yanga imepigwa faini ya Shs. 1,000,000 kwa kupita mlango usio rasmi.
“Pia Yanga imepigwa faini ya sh. 1.5 milioni kwa kutoingia vyumbani. Adhabu hiyo imezingatia Kanuni ya 14(8) ya Ligi Kuu. Vilevile klabu hiyo imepigwa faini ya Sha. 500,000 kutokana na kuonyesha vitendo vinavyoashiria ushirikiana. Adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 42(1) ya Ligi Kuu,” imesema taarifa hiyo ambayo FikraPevu inayo.
Katika mchezo huo, imeelezwa kwamba, mashabiki wa Yanga walivunja uzio wa ndani wa upande wa Magharibi wakati wakiingia uwanjani kusherehekea ubingwa wa timu hiyo, hivyo, klabu ya Yanga imeagizwa kulipa gharama za uharibifu huo uliofanywa na washabiki wake, uamuzi ambao umezingatia Kanuni ya 42(3) ya Ligi Kuu.
Nayo klabu ya Mbao FC imepigwa faini ya Shs. 500,000 kutokana na mashabiki wake kuingia uwanjani kushangilia baada ya timu yao kupata ushindi.
Wakati Yanga ikilimwa faini la kuamriwa kugharamia uharibifu, wachezaji wake Deus Kaseke, Simon Msuva na Obrey Chirwa wamesimamishwa kucheza mechi za Ligi Kuu wakati wakisubiri suala lao la kumsukuma na kumwangusha Mwamuzi Ludovic Charles kusikilizwa na kutolewa uamuzi na Kamati ya Nidhamu ya TFF.
Simon Msuva
“Walifanya kitendo hicho katika mechi hiyo dhidi ya Mbao FC iliyofanyika Mei 20, 2017 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijni Mwanza. Uamuzi wa Kamati umezingatia Kanuni ya 9(5) ya Ligi Kuu,” imeongeza taarifa hiyo.
TFF imesema kuwa, Mwamuzi Ludovic Charles amepewa onyo kali kwa kutodhibiti vizuri mchezo huo, uamuzi ambao umezingatia Kanuni ya 38(5) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti wa Waamuzi.
Kwa upande mwingine, TFF imeilima faini ya Shs. 1,000,000 timu ya Maji Maji baada ya kugoma kuingia uwanjani wakati wa mapumziko katika mchezo wake namba 225 na JKT Ruvu uliofanyika kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga Mei 13, 2017 ambao Maji Maji walishinda kwa bao 1-0.
Mbao FC imepigwa faini pia ya Shs. 500,000 kutokana na timu hiyo kutoingia vyumbani wakati wa mechi namba 230 baina yake na Kagera Sugar iliyochezwa Mei 13, 2017 katika Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba. Kagera ilishinda 2-0.
Wakati huo huo, Rais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), Gianni Infantino, ameipongeza klabu ya Yanga kwa kutwaa ubingwa Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu wa 2016/17.
Yanga imetwaa Kombe hilo ikiwa ni mara tatu mfululizo na katika salamu za pongezi, Rais Gianni Infantino amesema ubingwa huo wa Yanga ni kielelezo cha ushirikiano baina ya wachezaji, kocha, utawala, matabibu pamoja na mashabiki.
Katika pongezi zake, Rais Infantino ameishukuru Young Africans na shirikisho la mpira wa miguu la nchi kwa kusadia kupeleka ujumbe chanya kwa jamii kuhusiana na mpira wa miguu.