Viwanda 17 vilivyobinafsishwa vimekufa, tunawezaje kufikia ndoto za kuwa na ‘Tanzania ya Viwanda’?

Jamii Africa

RIPOTI ya mwaka 2012 ya iliyokuwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) inasema kwamba, takriban viwanda na mashirika 17 ya umma yaliyobinafsishwa mwaka 1993 yamefungwa baada ya kushindwa kuzalisha.

Hali inaleta changamoto katika azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuifanya ‘Tanzania kuwa nchi ya Viwanda’ kutokana na ukweli kwamba ni vigumu kujenga viwanda vipya wakati vile vilivyokuwepo tu vimeshindwa kuendelezwa, licha ya kwamba tayari vilikuwa na miundombinu pamoja na mashine mbalimbali za kuzalishia.

FikraPevu inatambua kwamba, viwanda na mashirika hayo 17 vilikuwa kati ya viwanda 74 vilivyobinafsishwa katika harakati za kuvifufua na kuvinusuru ili viongeze uzalishaji baada ya kuendeshwa kwa hasara wakati vilipokuwa mikononi mwa umma.

Lakini badala ya kufufuliwa na kuongeza uzalishaji, viwanda hivyo vikafungwa na wawekezaji waliovinunua ama kuingia ubia.

FikraPevu imebaini kwamba, asilimia kubwa ya viwanda vilivyobinafsishwa ama kuuzwa moja kwa moja kwa nia ya kuvunusuru vimekufa, vimefungwa au vimebadilishwa matumizi yake, huku vingi kati ya hivyo viking’olewa mitambo na kugeuzwa maghala.

Kiwanda cha Mang'ula Mechanical and Machine Tools Limited (MMMT) cha Kilombero mkoani Morogoro, ambacho alikabidhiwa Mchungaji Getrude Rwakatare kupitia St. Mary’s International Schools Februari 2007 ni miongoni mwa viwanda vilivyobadilishwa matumizi ambapo kwa sasa kinatumika kama madarasa ya Shule ya St. Mary’s International, ambayo ni miongoni mwa msururu wa shule anazozimiliki.

Kwa mujibu wa ripoti ya POAC, mashine nyingi ziling’olewa kitambo, majengo yameharibika na mitambo mikubwa imetelekezwa ambapo inasemekana baadhi ya watu wamekuwa wakiuza vifaa mbalimbali kama vyuma chakavu.

Ingawa mwaka 2007 Kamati ya Bunge ya POAC ilishauri serikali ivunje mkataba huo baada ya Mchungaji Rwakatare kushindwa kukiendeleza kiwanda hicho kilichokuwa kikizalisha zana mbalimbali, hakuna kilichofanyika mpaka sasa huku ajira za Watanzania zikiwa zimepotea baada ya wafanyakazi kufukuzwa ama kuachishwa kazi.

“Asilimia 80 ya viwanda na miradi ya umma iliyobinafsishwa wamiliki wapya wamebadilisha matumizi yake bila ya kutoa taarifa serikalini na serikali imekaa kimya tu, mfano ni kiwanda cha kutotoresha vifaranga kilichopo Banana-Ukonga jijini Dar es Salaam ambacho kimegeuzwa baa na maduka,” amedokeza mwananchi mmoja aliyechangia kupitia mtandao wa Jamiiforums.

FikraPevu imebaini kwamba, baadhi ya kampuni na viwanda hivyo havikuwahi hata kufanya kazi tangu vilipobinafsishwa miaka zaidi ya 20 iliyopita kinyume na makubaliano hali iliyoifanya POAC kuishauri serikali kuvirudisha viwanda hivyo mikononi mwa umma.

Mitambo ambayo ilikuwa ikitumika kutengenezea Zana za Kilimo katika kiwanda cha ZZK Iyunga jijini Mbeya ikiwa imetelekezwa

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya POAC, orodha ya viwanda vilivyobinafsishwa na vikashindwa kuendelezwa na wawekezaji ni Mwanza Tanneries, ambacho kiliuzwa kwa Africa Trade Development Limited (Mwanza), Tanzania Bag Corporation Limited Mills kilichouzwa kwa TPM (Kilimanjaro) na Morogoro Ceramics Ware Ltd ambacho kiliuzwa kwa Hans Nails Ltd (Arusha).

Vingine ni Morogoro Shoes Co. Ltd kilichonunuliwa na Guled Shoe Co. Ltd (Morogoro), Zana za Kilimo (ZZK) Mbeya kilichouzwa kwa CMG Investments Ltd (Mbeya), Arusha Metal Industry kilichonunuliwa na Bwana Mfahamiko (Arusha) na Mbeya Ceramics Company (MBECECO) kilicho mikononi mwa Kyela Valley Food Ltd (Mbeya).

Aidha, viwanda vingine ni Nyanza Engineering and Foundry kilichonunuliwa na Nyanza Cooperative Union na Halmashauri ya Manispaa ya Mwanza (Mwanza), Kilimanjaro Textile Mill Ltd (Kiltex Dar) kilichouzwa kwa Iron and Steel Co. Ltd (Arusha), Musoma Textile Mills (Mutex) kilichonunuliwa na Kiltex Ar/METL (Mara) pamoja na Polysacks Co. Ltd ambacho kiliuzwa kwa Prebond Ltd (Dar es Salaam).

Katika orodha hiyo pia vilitajwa viwanda vya Tractor Manufacturing Co. Ltd that ambacho kilichukuliwa na Quality Group Ltd (Dar es Salaam), Steel Rolling Mills kilichonunuliwa na Unique Steel Rolling Ltd (Tanga), Rukwa RTC kilichouzwa kwa wazawa Rukwa (2000) Ltd (Rukwa), LRT Motors ambacho kiliuzwa kwa LRT (2000) Motors Co. Ltd/MEBO Co (Dar es Salaam), Ubungo Garments Ltd kilichonunuliwa na VMB Holdings Ltd (Dar es Salaam) na Moshi Hand Tools (Kilimanjaro).

Wakati POAC ilipopokea ripoti hiyo, viwanda 42 vilivyobinafsishwa vilikuwa vinafanya vizuri wakati vingine 15, japokuwa vilikuwa vinaendelea kufanya kazi, lakini vilikuwa katika hali mbaya sana.

Inaelezwa kwamba, Mwanza Tanneries Limited, ambacho kilichukuliwa na Tanzania Leather Association Industries (TLAI) na African Trade Development Ltd pia kilisimama uzalishaji muda mrefu ambapo mwekezaji hakufanya jitihada zozote kukiendeleza.

“Mitambo mingi ukiwemo mtambo wa kutibu ngozi (effluent treatment plant – ETP) imeibiwa na mitambo iliyosalia iko katika hali mbaya, eneo kubwa limegeuzwa kuwa gereji na ghala la kuhifadhia vifaa vya uchimbaji madini vinavyomilikiwa na kampuni ya Caspian Ltd,” ilieleza ripoti hiyo wakati huo.

Hata hivyo, katika maeneo mengine POAC ilishindwa hata kupata mikataba na nyaraka muhimu ambayo ilitumika wakati wa zoezi la ubinafsishaji wa mashirika na viwanda hivyo.

Ripoti hiyo inasema, POAC ilishindwa kupata mkataba uliosainiwa baina ya Serikali na kampuni ya Pure Bond Limited wakati wa uuzwaji wa kiwanda cha Morogoro Ceramics Limited mwaka 1993.

Inaelezwa kwamba kiwanda hicho kiliuzwa kwa Shs. 452 na mwekezaji akaruhusiwa kusafirisha mitambo kupeleka Nigeria.

“Kiwanda kimetelekezwa na hakuna shughuli yoyote inayofanyika pale kwa kuwa machine zote zilihamishwa,” ilisema ripoti hiyo.

Aidha, uchunguzi unaonyesha kwamba, baadhi ya wawekezaji walibadilisha shughuli za uzalishaji tofauti na zile za mwanzo ambazo zilitarajiwa kuendelezwa.

Kiwanda cha Ubungo Farm Implements (UFI) ni miongoni mwa viwanda hivyo vya umma ambavyo ‘vilipitiwa’ na zoezi la ubinafsishaji ambapo kilichukuliwa na kampuni ya Tanzania Steel Pipes mwaka 2004 inayomilikiwa na raia wa Ufilipino, Terence Loh, lakini badala ya kuzalisha zana za kilimo ili kuhakikisha wakulima wanapata zana bora za kutosha, sasa kinazalisha mabomba ya maji, mradi ambao taarifa zinasema uliletwa na vigogo wa serikali katika Awamu ya Tatu ili kuzalisha mabomba kwa ajili ya Mradi Mkubwa wa Maji wa Ziwa Victoria.

Aidha, kiwanda cha Polysacks Company Ltd (BAGCO LTD) nacho kiligeuzwa kuwa ghala la kuhifadhia chumvi iliyozalishwa na kiwanda cha Kensalt.

Viwanda ambavyo vimefanya vizuri baada ya kubinafsishwa ni pamoja na Kampuni ya Sigara (TCC), Tanzania Breweries Limited (TBL), Kiwanda cha Mabati cha Aluminium (ALAF), Kagera Sugar, Mtibwa Sugar, Kilombero Sugar, Twiga Cement, Tanga Cement na Mbeya Cement.

Ingawa watendaji wengi wa serikali wamekuwa wakitetea uamuzi wa ubinafsishaji, lakini wananchi wengi wanaona kwamba zoezi hilo halikuwa na nia njema kwani licha ya kupoteza ajira za Watanzania wengi, lakini pia hata uzalishaji wa bidhaa muhimu umeshindwa kufanyika.

“Hii inaonekana kama ilikuwa hujuma, kwa sababu wengi kati ya waliouziwa ama kuingia ubia wameshindwa kuendeleza viwanda hivyo, wamegeuza matumizi ama wameng’oa kabisa na mitambo,” anasema Juma Shekimweri, mkazi wa Vingunguti jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo, wengi wanalalamika kwamba, zoezi hilo la ubinafsishaji lilitumiwa vibaya na baadhi ya watendaji na wanaoitwa wawekezaji, ambao waliamua kujiuzia viwanda hivyo bila kuwa na uzoefu na utaalam wa shughuli zenyewe.

“Wengi walifanya njama tu na kuua viwanda vyetu ili wapate kamisheni na wafanyabiashara kutoka nje ambao walianza kuingiza bidhaa zile zile tulizokuwa tunazalisha, tena wakauza kwa bei nafuu,” anasema Wilson John, mkazi wa Temeke jijini Dar es Salaam.

“Wanasiasa wasio waadilifu walikwenda kwa siri nje kusaini mikataba feki ili kuingiza bidhaa zile zile ambazo viwanda vyetu vilizalisha na kuzipeleka nje, tukauziwa kwa bei ya juu na kuua viwanda vyetu… angalia tulikuwa na kiwanda cha kutengeneza magari cha Nyumbu, lakini kimekufa, kile General Tyre ndiyo kwanza kinataka kifufuliwe baada ya kuuawa na wajanja wachache,” anaeleza Sigfrid Muhumba.

Katika mahojiano na mwandishi wetu mapema mwaka huu, aliyekuwa Msajili wa Hazina, Lawrence Mafuru, alikiri kwamba viwanda vingi vilivyobinafsishwa vilikuwa havifanyi kazi iliyopangwa na vingine vilikiuka mikataba kwa kutokuzalisha kabisa.

Hata hivyo, akasema kwamba, baadhi ya wawekezaji walikuwa wakilalamika kuwa mitambo iliyokuwepo ilikuwa imepitwa na wakati na kwamba walihitaji fedha nyingi zaidi kununua mitambo mipya kama walitaka kuendelea kuzalisha bidhaa zile zile.

“Kuna malalamiko mengi, mashirika na viwanda vingi vilibinafsishwa na kila ukitazama mafaili unakuta wengi wanalalamika kwamba hawakuweza kuendeleza uzalishaji kwa vile mashine mbovu na vipuri vyake havipatikani, wengine wanasema ni bora kubadili uzalishaji, lakini wanakosea kwa sababu mikataba inawafunga,” alisema Mafuru.

Aidha, alisema kwamba, suala la kuruhusiwa kwa bidhaa mbalimbali kutoka nje zinazouzwa kwa bei nafuu kuliko bidhaa zinazozalishwa ndani nalo lilichangia viwanda vingi kushindwa kuendelea na uzalishaji, kwani viwanda vya ndani haviwezi kushindana na bidhaa hizo za nje.

FikraPevu inaona kwamba, ingawa serikali ilikwishaahidi kwamba ingevirejesha viwanda hivyo vilivyoshindwa kuzalisha mikononi mwake, lakini kasi hiyo bado ndogo hasa katika kipindi ambacho wengi wanategemea kuona ‘Tanzania ya Viwanda’.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *