Vyoo shuleni mpaka harambee?

Jamii Africa

HAKUNA eneo muhimu katika makazi ya watu au kwenye jumuiko la wananchi, kama choo.

Hili ni eneo maalum, lenye kubeba afya ya binadamu katika mazingira bora. Hata hivyo, ni eneo linalosahaulika mno. Iwe nyumbani, iwe sokoni, iwe kwenye vituo vya basi, maeneo yenye vyoo ni vurugu. Hayana usafi wa kutosha, idadi kubwa ya watu hawajali maeneo hayo.

Hali ni hiyohiyo shuleni. Shule nyingi zinashindwa kuwa na vyoo vya kutosha, achilia mbali usafi wake. Pamoja na umuhimu wake, siyo uongozi wa shule, walimu, wanafunzi wenyewe na hata serikali, haitoi kipaumbele kwenye maeneo ya vyoo shuleni.

Hali hii ni tofauti kabisa na suala la madawati, vyumba vya walimu, madarasa, maabara na hata sare za shule.

Akizungumza na FikraPevu, Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako anasema siyo kweli kwamba serikali haitoa kipaumbele kwa vyoo shuleni.

“Serikali inafanya kazi kwa vipaumbele na kutegemea rasilimali zilizopo, kwa kuwa vyoo vipo mashuleni, hata kama havina ubora zaidi, lakini siyo kwamba hatuvipi umuhimu wa kuwepo wala kuvifuatilia, tutafika tu huko,” anasema.

Prof. Ndalichako anasema serikali ya sasa iliona kuna uhaba mkubwa wa madawati, ikaamua kuanza na changamoto hiyo, ikaendelea na suala zima la kuwepo walimu wa kutosha na wenye elimu ya uhakika na tunapambana bado na majengo.

Waziri Ndalichako ameahidi kuanza kupambana na ubora wa vyoo shuleni na vyuoni, kwani ni maeneo muhimu yanayotakiwa kuwa safi na kwamba vyoo viwepo vya kutosha kwa mujibu wa mahitaji na sera ya taifa. Mapema mwaka jana, 2016, serikali ya awamu ya tano, chini ya uongozi wa Rais John Magufuli ilianzisha harambee ya kuchangia madawati katika shule za msingi nchini.

 Watu mbalimbali; wahisani, mashirika na kampuni zilijitokeza kuchangia na kufanikiwa kwa kiasi kikubwa kutimiza lengo la kuhakikisha hakuna wanafunzi wanaokaa sakafuni au juu ya mawe.

Kutokana na harambee ya kuchangia madawati, iliyohimizwa mno na serikali, hivi sasa taswira ya vyumba vingi  vya madarasa, inavutia. Madawati yapo ya kutosha.

Pamoja na kwamba tathmini ya mafanikio ya wingi wa madawati bado inaendelea kukusanywa  nchi nzima, kuna kila dalili kwamba lengo limevukwa. Shule nyingi sasa zina madawati ya kutosha, huku zingine zikikosa vyumba vya kuyahifadhi.

Haya ni mafanikio makubwa ambayo yatasaidia wanafunzi kusoma katika mazingira yenye “kuchochea” uelewa na umakini darasani.

(Rais Magufuli amesifu harambee na michango iliyofanikisha kupatikana kwa madawati. Lakini vipi kwa upande wa vyoo? Tumejisahau. Hali bado ni mbaya. Vyoo vimeendelea kuwa tatizo kubwa  katika  shule zetu nchini, hususan katika  shule za msingi, ambapo  tatizo hili limeendeea kuwa sugu.

Ni vigumu kung'amua tatizo hili bila ya kufanya uchunguzi, kwani wengi wanapotazama vyoo vya shule, wanaona  majengo, lakini kumbe “nyuma ya pazia,” vyoo vingi vimejaa, havina maji, havisafishwi ipasavyo na havifai kwa matumizi ya wanafunzi wala walimu wao.

Yapo maswali mengi ya kujiuliza; je,  idadi ya matundu yaliyomo, inaendana na wingi  wa wanafunzi? Je, vyoo hivi ni rafiki kwa wanafunzi wenye ulemavu? Hali ikoje ndani ya vyoo hivyo?

 Ukweli ni kuwa matundu ya vyoo yaliyopo katika shule nyingi ni machache sana na  hayatoshelezi idadi ya wanafunzi waliopo na  sio  rafiki kwa watumiaji wake, hasa wasichana, ambao mara nyingi wamekuwa wakikatisha masomo yao, hasa wakiwa wakiwa hedhi kutokana na mazingira mabovu, uhaba wa  maji na  vifaa vya kunawia mikono  kama vile sabuni.

Vyoo vingi vya wavulana na wasichana vinatumia jengo moja, huku vikiwa havina milango,  vingine  vimejengwa kwa nyasi na vingine  mashimo  yake yamefunikwa  kwa  magogo, hasa maeneo ya vijijini.

Ni kutokana na uhaba wa vyoo, shule nyingine zina tundu moja la choo, linalotumiwa kwa pamoja; wanafunzi wavulana na wasichana a hata walimu wao.

Baadhi ya shule hazina vyoo kabisa, hali inayosababisha wanafunzi kujisaidia vichakani, hali inayoweza kuhatarisha afya zao kutokana na magonjwa mbalimbali ya milipuko yanayosababishwa na uchafu kama vile kipindupindu, homa ya matumbo, minyoo na kuhara.

Hali hii imesababisha  kwa kiasi kikubwa  kushuka kwa kiwango cha taaluma nchini. Wanafunzi  wengi wamegeuka watoro sugu, huku wengine wakiamua kusitisha masomo yao kutokana na ukosefu wa vyoo.

Wanafunzi wengine hukosa vipindi kwa kupoteza muda mwingi kutokana na ama kusubiriana chooni kunakosababishwa na uchache wa matundu ya vyoo au kuamua kwenda nyumbani, kama ni jirani au vichakani.

Hali hii imesababisha matokeo mabovu ya mtihani wa darasa la saba kwa shule nyingi nchini  zenye tatizo la vyoo.

Sera ya elimu ya mwaka 2005, inataka kila tundu moja  la choo kutumiwa na wanafunzi wa kike 20 na wa kiume 25,  lakini  takwimu za idadi ya matundu ya vyoo katika shule za msingi mwaka 2014, zinaonesha hali ni mbaya  katika mikoa ya Tabora, Simiyu, Geita na Dar es Salaam.

Katika wilaya ya Kaliua mkoani Tabora,  wastani wa wanafunzi kwa tundu moja ni wavulana 257 na wasichana 228.

Wilaya ya Itimila mkoani Simiyu; wavulana 130 hutumia tundu moja la choo, huku wasichana 137 nao wakitumia tundu moja. Wilaya ya Geita mkoani Geita, wastani ni wavulana 114 kwa tundu moja na wasichana 110.

Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu ni wastani wa wavulana 133 kwa tundu moja na wasichana 149.

Katika Mkoa wa Dar es Salaa, Wilaya ya Kinondoni wastani ni wavulana 115 kwa tundu moja na wasichana 111,  ilihali wilayani Temeke wastani ni wavulana 102 kwa tundu moja na wavulana 92.

Zipo baadhi ya  halmashauri zilizojitahidi kutimiza lengo la sera ya elimu la wastani wa wanafunzi 20 hadi 25 kwa tundu moja kama vile halmashauri ya wilaya ya Rombo na Mwanga mkoani Kilimanjaro pamoja na halmashauri ya wilaya ya Hanang mkoani Manyara.

Kuanza kwa sera mpya ya elimu bure tangu Januari mwaka huu, 2016, hali ya vyoo inaelezwa kuwa mbaya Zaidi kutokana na kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi walioandikishwa darasa la kwanza.

Takwimu zinaonesha kuwa idadi ya wanafunzi walioandikishwa mwaka huu, imeongezeka kutoka wanafunzi 1,282,100 – mwaka uliopita, hadi kufikia wanafunzi 1,896,584 sawa na ongezeko la asilimia 84.5. Zaidi ya wanafunzi wameandikishwa.

Pamoja na uzuri wa kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi katika shule zetu, ni vyema suala la miundombinu ya vyoo, likapewa umuhimu mkubwa ili kujenga afya bora za wanafunzi na hata walimu.

Kuruhusu uhaba mkubwa wa vyoo kunaweza kusababisha mkwamo kwa nia nzuri ya serikali ya kuhakikisha idadi ya watoto wasiojua kusoma, kuandika na kuhesabu inapungua.

Je, tujiulize, tunahitaji harambee nyingine kukabili uhaba wa vyoo au tunasubiri hadi Rais Magufuli alisemee hili, ndipo watendaji wa shule, halmashauri na mkoa wachukue hatua za “zimamoto?”

Hapana tubadilike.

 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *