WABUNGE wa Mikoa ya Kanda ya Ziwa, wameitaka Serikali kuivunja mara moja Bodi ya Pamba nchini (TCB), kwa madai ya kushindwa kuwanufaisha wakulima wa hali ya chini, badala yake Bodi hiyo imekuwa na mikakati ya kuyaneemesha makampuni na wafanyabiashara wakubwa.
Mbali na kutaka Bodi hiyo iliyopo chini ya uenyekiti wake, Dk. Festus Limbu ivunjwe, pia wabunge hao wameitaka Serikali kuvunja mkataba baina yake na kampuni ya nje ya nchi ya KYUTON, iliyopewa tenda ya kuzalisha mbegu bora za pamba hapa nchini, na kwamba kazi hiyo yapewe makampuni na mashirika ya wazawa, na si Wazungu.
Wakizungumza kwa jazba jana kwenye Mkutano Mkuu wa Tisa wa sekta ndogo ya pamba, uliofanyika kwenye ukumbi wa BoT jijini Mwanza, wabunge hao walieleza kukasilishwa na utendaji mbovu wa Bodi hiyo, kwa kushindwa kuwanufaisha wakulima kupitia zao hilo tangu miaka 50 ya uhuru.
Walisema, inashangaza Bodi hiyo chini ya mwenyekiti wake, Dk. Limbu na Mbunge wa jimbo la Magu mkoani hapa (CCM), kuamuru wakulima kuuziwa kilo moja ya mbegu za pamba kwa sh. 1,000 huku Bodi hiyo ikiamuru pia kununua kilo moja ya pamba kwa sh. 800 pekee.
Mbunge wa Kishapu mkoani Shinyanga, Suleiman Nchambi (CCM), ndiye aliyeanza kutupa makombora hayo mazito kwa uongozi wa Bodi hiyo, akitaka ivunjwe kwa madai kwamba imepoteza sifa ya kusimamia sekta hiyo kwa manufaa ya Watanzania, kwani tangu nchi ipate uhuru wakulima wamekuwa wakinyanyasika sana, huku Bodi hiyo ikishindwa kuwapatia mbegu bora na suluhisho la maendeleo yao.
“Hivi tunawezaje kuanza kutoa elimu kwa wananchi wetu kuhusu mkanganyiko huu wa bei ya mbegu na kilo ya pamba?. Yaani kilo ya mbegu muuze 1,000 lakini kilo ya pamba mmnunulie mkulima kwa sh. 800?. Hivi hiyo mnaona ni sawa?.
“Mheshimiwa mwenyekiti, sisi tunaona hii Bodi imepoteza sifa ivunjwe mara moja. Maana haiwasaidii wananchi na wakulimawa hali ya chini.
“Hatukubali, tunakataa na tutaenda Bungeni kukataa suala hili. Bahati nzuri wewe mwenyekiti ni mbunge mwenzangu, tutakutana kwenye vikao vya kamati na mlango wa Bunge kukataa haya madudu”, alisema mbunge huyo wa Kishapu, Nchambi, kisha kushangiliwa na wajumbe karibu wote wa mkutano huo.
Kuhusu mkataba wa kampuni hiyo ya KYUTON iliyopewa kuzalisha mbegu bora za pamba, mbunge huyo wa Kishapu, mbunge wa jimbo la Nzega mkoani Tabora, Dk. Hamis Kigwangalla (CCM), na mbunge wa Meatu mkoani Shinyanga, Meshack Opulukwa (Chadema), walisema kwa nyakati tofauti wakati wakichangia kwamba, mkataba huo ni wa ovyo hovyo, hivyo uvunjwe mara moja.
Katika hilo, Dk. Kigwangalla ambaye alionekana kuwachanganya baadhi ya wajumbe kutokana na Bastola yake kuonekana mara kwa mara wakati akisimama kuchangia, alisema: Huu mkataba tunao na ni wa ovyo sana. Hatuwezi kukubali nchi yetu iendeshwe kwa namna hii maana mkataba unazuia mtu mwingine kuwekeza kwenye kazi hii ya uzalishaji wa mbegu za pamba”.
Alisema, kutokana na ukweli kwamba wakulima wa pamba wamenyanyasika na kupunjwa tangu mwaka 1961, wakati umefika sasa Serikali iweke utaratibu mzuri wa kuwanufaisha wananchi wake kupitia zao hili na si vinginevyo, na kwamba mkataba huo hawakubaliani nao na wanataka uvunjwe.
Naye mbunge wa Jimbo la Mwibara Wilayani Bunda Mkoani Mara, Kangi Lugola alisimama na kuwatahadharisha wajumbe wa mkutano huo kwamba huenda mkutano huo ukavunjika na usifikie kikomo chake, kutokana na kuonekana wazi ajenda ya kuwanufaisha wakulima haipo katika mikakati ya Bodi hiyo.
“Mheshimiwa mwenyekiti, natoa angalizo inawezekana mkutano huu ukavunjika. Maana hapa hatuoni mikakati thabiti ya kuwasaidia wananchi wetu iliyowekwa na Bodi, badala ya kutaka kuanza kuwanufaisha matajiri na makampuni ya nje”, alisema.
Kwa upande wake, Mkuu wa mkoa wa Morogoro, Joel Bendera pamoja na Mkuu wa wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, Benson Mpesya waliishambulia vikali Bodi hiyo, huku wakiitaka wawakamate wamiliki wa makampuni yaliyosambaza mbegu zilizooza kwa wananchi msimu uliopita, na kwamba madudu yanayofanyika viongozi wa Bodi hiyo hawawezi kukwepa kuwajibika.
Naye mbunge wa jimbo la Busega wilaya mpya ya Busega mkoa mpya wa Simiyu, Dk. Titus Kamani alisisitiza umuhimu wa Serikali kuanzisha viwanda japo vitano vya kutengeneza nyuzi, na kwamba uwepo wa viwanda hivyo utachochea maradufu soko la pamba hapa nchini.
Kwa mujibu wa mbunge huyo wa Busega, Dk. Kamani inashangaza sana kuona Tanzania inakosa viwanda kama hivyo vya kutengeneza nyuzi wakati inazalisha pamba kwa wingi, na kusema wakati umefika sasa Serikali na sekta binafsi zianze kujenga viwanda hivyo, ili iweze kuuza bidhaa hiyo nje ya nchi kwa faida ya Watanzania wenyewe.
Habari hii imeandaliwa na Sitta Tumma – FikraPevu Mwanza.
Kiasi nachanganyikiwa,makampuni yanayonunua pamba bila shaka ni ya watu binafsi,na ukweli usiopingika ni kuwa yapo pale kwa masilahi binafsi.si kwa lengo la kuwanufaisha wakulima wa pamba , na siajabu baadhi ya viongozi wa bodi wakawa na hisa ndani ya makampuni hayo au kwa namna moja au nyingine wanamiliki makampuni hayo.Nawaomba wakulima wawe na msimamo mmoja,wasikubali kuburuzwa na matajiri hawa.Wazo la serikali kuanzisha viwanda vya kusokota nyuzi ni la msingi sana kama yenyewe haiwezi ,ielekeze vyombo vyake kama Takukuru kuwa chunguza wajumbe wa bodi na endapo wamo walio na masilahi katika makampuni hayo waondolewe kwa faida ya wakulima na pia iangalie uwezekano wa ,kiwanda kama cha Tabora kikabidhiwe kwa bodi baada ya kuweka utaratibu mzuri wa kutohujumiwa kama Nyanza ilivyohujumiwa.Tatizo kubwa tulilonalo ni utashi wa Serikali pia sina hakika kama kuna dhamira ya kweli ya kuwainua wakulima wa Pamba kwani Jumuia ya wakulima wa pamba ni kubwa sana jumuia hii ikisitisha ulimaji wa Pamba na wakajikita katika mazao mengine kitakua kilio kikubwa sana kwa nchi hii ,si kwa serikali hii tu na hata hayo makampuni ,Jambo hili nakumbuka kama liliwahi kutokea .Nawakumbusha matajiri na Serikali kwa ujumla ,uwepo wa wakulima wa pamba ndio uwepo wao na pato la taifa pia.Nasikitika kusema pamba kama pamba hailiwi kama mpunga au viazi vitamu, Mpunga unahifadhika na viazi utatengeneza matobolwa au michembe ,hapo ndipo utumwa wa mkulima wa pamba unapoijia.Wakulima wa pamba msijinyanyapae .Tafuteni mbinu ya kjikomboa.