Wakaazi wa wilaya ya Kilwa mkoa wa Lindi wanategemea zao la korosho kama zao kuu la biashara na kusahau mazao mengine yanayoweza kubadili maisha yao kiuchumi. Sababu kuu ni kukosa mafunzo na teknolojia inayowawezesha kulima mazao mbalimbali kulingana na mahitaji ya soko.
Biubwa Ibrahim Maingo, mkazi wa Kilwa ametumia changamoto za wakulima wa wilaya hiyo na kuwa fursa kwa kuwajengea uwezo wakulima kugeukia mazao mengine ili kujikwamua kiuchumi.
Biubwa ambaye ni mzaliwa wa Kilwa lakini amekuwa akiishi Dar es Salaam aliamua kurudi nyumbani na kuungana na wakulima wengine ambao walikuwa na hali ya kuleta mabadiliko ya kiuchumi katika wilaya hiyo.
“Umasikini niliokutana nao haukuniridhisha na isitoshe mimi ni mzaliwa wa Kilwa na wakati huo nilikuwa naishi Dar es salaam sikuona vema kukaa mjini lakini niliamua kurudi kijijini na kupanga mikakati ya kuwainua wananchi wa vijiji mbalimbali vya wilaya ya Kilwa kupitia sekta ya kilimo.
Hatua ya kwanza ilikuwa kufanya utafiti wa kilimo katika wilaya hiyo na kuunda mfumo binafsi wa vikundi vya wakulima ili kuwapatia mafunzo na teknolojia ya kilimo cha kisasa.
Baada ya kuwa na taarifa za kutosha alianzisha programu ya kutoa mafunzo kwa wananchi wa kata zote za Kilwa kwa sababu anaamini kuwa huwezi kutekeleza sera yoyote ya kilimo bila kuwaelimisha wakulima na kuonyesha mafanikio watakayoyapata katika sera husika.
Ili kuhakikisha anafanikiwa kubadili maisha ya wakulima, alitumia muda wa miaka miwili kubadilisha mawazo, mitazamo na itikadi ambazo watu wa Kilwa walikuwanazo za kutegemea zao moja la korosho, licha ya kuwa na ardhi kubwa ambayo inaweza kutumiwa kulima mazao ya bishara na kuondokana na umaskini.
Biubwa anasema alizunguka vijiji 27 vya kata zote nne na kutoa mafunzo ya kilimo cha kibiashara kwa wanachi akishirikiana na viongozi wa vijiji. Ingawa alipata upinzani toka kwa watu mbalimbali na viongozi wa serikali kuwa mradi wake hautafanikiwa kwa sababu viongozi wametumia njia nyingi kuinua kilimo lakini wameshindwa kuleta mabadiliko ya kweli.
“Changamoto hizi hazikunizuia kutimiza nia yangu ya kuwakomboa wananchi na nilitumia miaka miwili ya kubadili mawazo ya watu ambao wakati wote waliamini kuwa mwanamke hawezi kuishawishi jamii na kuleta mabadiliko”, amesema Biubwa.
Anasema aliwajengea uwezo wa kujiamini na kuunda vikundi 275 vya ujasiliamali ambapo kila kikundi kina mtaji wake ambao unatokana na michango ya wanachama. Vikundi hivyo vinasimamiwa na taasisi ya Amsha inayojihusisha na ujasiriamali vijijini.
Biubwa akishirikiana na wakulima walianza kutekeleza maadhimio yao kivitendo kwa kutafuta ardhi ya kulima bila kutegemea ufadhili wa serikali. Kwa kuwa wanachama wa vikundi hivyo walikuwa na ardhi kubwa ambayo haijalimwa walifyeka na kusafisha mapori.
Wakulima maelezo ya njia bora za kulimo katika shamba darasa
Mtaji wa kuendeshea mradi wa kilimo ulipatikana kwa kuuza miti na kuchoma mkaa katika mashamba ya wakulima na fedha zilizopatikana zilitumika kununua pembejeo za kilimo.
“Wakulima wana fedha katika ardhi yao na kulikuwa hamna haja kukopa katika taasisi nyingine, tulifanikiwa kukusanya zaidi ya milioni 48 na kuanza kulima mazao ya ufuta,mtama,mahindi na mihogo”, anafafanua.
Anaeleza kuwa amewarithisha wakulima dhana ya kuona kila kitu kinawezekana na umuhimu wa kutumia rasilimali zinazowazunguka kutengeneza utajiri bila kutegemea msaada kutoka kwa serikali. Wakulima hao walianza kulima hekali 1 na sasa wana zaidi ya hekali 2,000 ambazo wanalima mazao mbalimbali ya chakula na biashara.
“Sisi kama AMSHA hutupokei fedha yoyote kutoka serikalini wala kwa wafadhili lakini tunachojali ni ushirikiano, umoja na uaminifu kwa kila mwanachama katika kukuza kilimo chenye tija kwa kila mtu”, amesema Biubwa.
Baada ya awamu ya kwanza ya mradi huo, vikundi 50 kati ya 275 vilivyokuwa na mtaji wa milioni 48 vimefanikiwa kutengeneza faida ya milioni 191 kutokana uuzaji wa mazao ya ufuta na mtama kwenye viwanda vya ushindikaji kikiwemo cha kiwanda cha Bia Tanzania(TBL).
Mafanikio haya yamechangiwa zaidi na mafunzo ambayo yanaendelea kutolewa kwa wakulima hao kutoka kwa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo ya Naliendele iliyopo Mtwara ambao wanatoa mafunzo ya kuchagua mazao ya kulima kulingana na aina ya udongo unaopatika sehemu husika.
Pia wanashirikiana kwa karibu na Shule ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam(UDSM)ambayo hutoa mafunzo ya kupata soko la uhakika la mazao yanayozalishwa na wakulima wa Kilwa. Wakulima hao wameingia mkataba na kampuni ya ALIGRAM kuzalisha ufuta ambapo kampuni hiyo itatoa pembejeo muhimu kwa wakulima ili kuzalisha zao hilo na kujipatia kipato cha familia.
Kutokana na faida inayopatikana katika kilimo, AMSHA imeandaa mradi mwingine wa kuwawezesha wakulima kujenga nyumba bora za bei nafuu. Mradi huu unalenga kuboresha mazingira na makazi ya wakulima ili wawe na sehemu nzuri ya kuhifadhi mazao na kupata haki ya makazi bora.
Biubwa anatoa wito kwa serikali na wadau wanaohusika na kilimo nchini kutekeleza sera za kilimo kwa vitendo kwa kutoa mafunzo, teknolojia na soko kwa wakulima ili wafaidike na kilimo cha bishara.