Wakulima nchini wamelalamikia mrundikano wa kodi zinazotozwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kudai kuwa unakwamisha sekta ya kilimo kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa viwanda.
Malalamiko hayo yametolewa leo na wadau mbalimbali wa sekta binafsi mbele ya Rais John Magufuli wakati wa kikao cha 11 cha Baraza la Taifa la Biashara kilichofanyika Ikulu, jijini Dar es Salaam ili kujadili changamoto za uwekezaji na mazingira ya kufanyia biashara nchini.
Akizungumza katika kikao hicho, Rais John Magufuli amesema serikali inakabiliwa na changamoto mbalimbali lakini inataka kusikia kutoka kwa wakulima na wafanyabiashara ili kufikia muafaka na kuharakisha maendeleo ya viwanda nchini.
“Tuambizane ukweli wapi tunaenda, wapi tumetoka na wapi tunaelekea. Sisi upande wa serikali tuna changamoto zetu zipo tu nyingi. Lakini upande wenu nyinyi wafanyabiashara mna changamoto zenu”, amesema na kuongeza kuwa,
“Tujue tatizo nini, serikali ifanye nini? Ili tusolve problem (tutatue tatizo) maana kila mwaka tunakuja tunazungumza hayohayo ni lazima tufike mahali tusolve problem (tutatue tatizo)”.
Wawakilishi hao kutoka mikoa mbalimbali wamesema changamoto kubwa wanayokabiliana nayo kwenye uzalishaji na biashara ya mazao ya kilimo ni mrundikano wa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) na ushuru uliowekwa na serikali.
Mwenyekiti wa Sekta Binafsi Tanzania, Reginald Mengi akizungumza wakati wa kikao cha Baraza la Taifa la Biashara, Ikulu jijini Dar es Salaam leo.
Mfanyabiashara wa zao la Pamba kutoka Shinyanga, Fredy Shukuru amesema kodi zinazotozwa kwenye bidhaa za pamba ikiwemo mafuta na mashudu yanayosafirishwa nje ya nchi ni kubwa kuliko thamani ya uzalishaji.
“Nilikuwa nakuomba Mhe. Rais utusaidie kuangalia kwenye maeneo ya VAT kwenye baadhi ya products (bidhaa) zinazotokana na pamba. Mbegu tunayoipata kwenye pamba tunatoa mafuta na mashudu tunauza nje ya nchi yana ushindani mkubwa wa VAT na kusababisha bei inakuwa kubwa”.
Amesema ili kuwapatia wakulima na wafanyabiashara nafuu ni vema kodi hizo zikaondolewa au kuchanganywa pamoja ili kuondoa usumbufu unaojitokeza wa wakulima kulipa kodi zaidi ya moja kwenye zao moja.
“Hizi kodi zilizopo kwenye viwanda ni nyingi sana zinakaribia 41 ziondolewe au zichanganywe pamoja zipunguze leseni”, amesema Shukuru.
Kwa upande wake, Mkulima na Mfanyabiashara wa mbao kutoka mkoa wa Njombe Benard Mnyuka, amesema matumizi ya mashine za EFD (Electronic Fiscal Device ) kwa biashara ndogo ya mazao bado ni tatizo ambalo limesababisha biashara nyingi kufa.
“Suala la kodi hasa mbao, unakuta mkulima ana heka zake mbili anapotaka kuuza anakutana na vikwazo kwamba anatakiwa awe na mashine ya EFD. Kwahiyo wakulima wetu wanalalamika sana kuhusu hili suala”, amesema Mnyuka na kuongeza kuwa,
“Akishatoka kwa mkulima, anaelekea tena kwa mnunuzi naye anatakiwa awe na mashine anaenda kwa mwenye gari naye anapofika Iringa anaambiwa naye awe na mashine ya EFD. Kwahiyo wafanyabiashara wetu wamekuwa na matatizo makubwa sana “.
Wakulima wa Alizeti kutoka mkoa wa Singida nao wameweka wazi usumbufu wanaoupata ambapo wamelalamikia ongezeko la ushuru wanaotozwa kwenye mashudu na mafuta ya kula.
Mzalishaji wa mafuta ya kula ya alizeti kutoka mkoa wa Singida Yusuph Amir amesema, “Mkoa wa Singida tunakabiliwa na changamoto ya VAT kwenye mafuta na mashudu ya Alizeti. Alizeti tunanunua kwa wakulima ambao hawana risiti, sasa hiyo VAT inatushinda sisi kuilipa. Na wakati mwingine unakuta viwanda mfano Singida viko 120 lakini tuliosajiliwa VAT labda 3 sasa na hiyo VAT asilimia 18 ya ndoo moja ni sawa na elfu na kitu.”
Amebainisha kuwa ni vema serikali ikaondoa ushuru wa mashudu na kubakiza kodi ili kumpunguzia mkulima mzigo wa kodi nyingi ambazo haziendani na hali ya uzalishaji na biashara ya zao hilo.
“Tunaomba utuondolee ushuru wa mashudu na Alizeti hii tunayoinunua kutoka kwa wakulima kwasababu Alizeti hiyo hiyo umenunua kwa wakulima asubuhi umeisaga halafu jioni unaambiwa ulipie ushuru sh. 2000 kwenye gunia hiyo faida itatoka wapi tunashindwa hadi tumefunga viwanda”, amesema Amir na kuongeza kuwa,
“Mhe. Rais tunakuomba wewe na serikali yako uongeze kodi kwenye mafuta yanayoagizwa nje yanauzwa kwa bei ya chini kwahiyo mafuta yetu yanayozalishwa nchini yanashindwa kushindana na bei za sokoni”.
Mkulima wa Mkonge kutoka Morogoro, Damian Luhinda amesema changamoto inayowakabili kwenye zao la Mkonge ni gharama kubwa za uzalishaji viwandani ambazo huambatana na kodi kubwa ya serikali na matokeo yake huathiri mfumo mzima wa uzalishaji wa zao tangu likiwa shambani.
Naye, Mwekezaji wa kiwanda cha kukoboa Kahawa kilichopo Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Danstan Komba amesema wakulima wanalima Kahawa kwa wingi lakini wanakosa magunia ya kuhifadhia zao hilo kabla halijapelekwa kiwandani kwaajili ya usindikaji. “Changamoto yangu ni kuchelewa kwa magunia ya kuhifadhia Kahawa ambayo yanaagizwa nje ya nchi”.
Awali akichangia katika mazungumzo hayo, Mwenyekiti wa Sekta Binafsi Tanzania, Reginald Mengi alisema serikali inapaswa kutengeneza mazingira wezeshi kwa wakulima ili kuchochea uzalishaji wa bidhaa za viwandani.
“Pamoja na matokeo ya ukuaji wa uchumi wetu wa asilimia 6.8, tuko mbali kufikia uchumi wa kati ifikapo 2025. Biashara nyingi zinafungwa kutokana na kodi nyingi ambazo ni kandamizi, kodi hizi zinadidimiza ukuaji wa biashara”.
Kikao cha Baraza la Taifa la Biashara, kikiongozwa na rais John Magufuli Ikuli jijini Dar es Salaam leo.
Kauli ya Serikali
Akitolea majibu ya wakulima, Rais Magufuli amesema serikali inapitia kodi zinazotozwa na TRA ili kuwapatia wakulima na wafanyabiashara nafuu ya uzalishaji wa bidhaa ikiwemo mafuta ya kula yanayotokana na zao la Alizeti.
Naye Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema serikali imesikia changamoto zote za wakulima na wafanyabiashara na watazifanyia kazi ili kuhakikisha tija inapatikana kwa pande zote ikiwemo sekta binafsi na ya umma.
“Hayo mliyotuambia tumeyachukua na tutayafanyia kazi. Mambo yote mliyochangia hapa Mawaziri wenzangu na Makatibu tunapoelekea kwenye kipindi cha bajeti tutayatolea majibu. Lengo letu ni kuona uwekezaji wenu unaleta tija kwenu na katika nchi”, amesema Waziri Mkuu.