Walimu wapya wa sekondari Mwanza wazua kizaazaa ofisi za Jiji

Jamii Africa

WALIMU wapya wa Shule za Sekondari Jijini Mwanza, wamelazimika kuacha kufundisha wanafunzi darasani kwa siku nzima, kisha kwenda kupiga kambi katika ofisi za jiji hilo, kwa lengo la kushinikiza kulipwa mishahara yao ya Februari mwaka huu.

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa

Tukio hilo la aina yake, lilitokea jana ambapo walimu hao wa Sekondari walifika kwenye ofisi hizo za jiji wakilalamikia kitendo walichodai kupigwa danadana na maofisa wa jiji hilo juu ya kulipwa haki zao hizo, jambo lililowalazimu kukataa kuondoka hadi wapewe fedha zao hizo za mshahara.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa jazba, walimu hao walilalamikia manyanyaso waliyodai kufanyiwa na ofisi ya Utumishi pamoja na Idara ya Sekondari jiji, ambapo walisema, mishahara iliyoidhinishwa na Serikali kwa ajili ya kulipwa walimu wenye Digrii na Diploma zimekatwa kisha kulipwa fedha kidogo tofauti na maelekezo ya Serikali.

Walisema, Serikali imeidhinisha mishahara ya walimu wenye digrii kulipwa sh. 469,200 kwa mwezi, lakini siku hiyo majira ya jioni walikuwa wakilipwa na jiji sh. 404,600 huku sh. 64,600 wakikatwa kila mwalimu wa daraja hilo bila maelezo yoyote, jambo walilodai huenda ni vitendo vya kifisadi vilivyoanza kufanywa dhidi ya fedha zao.

Mbali na walimu hao wenye digrii kulalamikia kukatwa fedha zao hizo bila sababu zozote, walimu wenye elimu ya Diploma nao waliungana na wenzao kulalamikia kukatwa mishahara yao kinyume na utaratibu, na kwamba walipaswa kupewa mshahara wa sh. 325,700 lakini walikuwa wakilipwa kila mwalimu wa Diploma kiasi cha sh. 290,600, hivyo sh. 35,100 walikuwa wakikatwa kwa kila mmoja wao.

Walikwenda mbali zaidi na kusema, kwa kiwango hicho kidogo cha fedha baadhi ya walimu watashindwa kupanga hata nyumba za kuishi, badala yake watalazimika kuishi kwenye nyumba za kulala wageni (Guest House), na kwamba wamelazimika kuchukuwa fedha hizo ndogo kwa sababu ya ugumu wa maisha tangu waliporipoti jijini hapa.

Mwalimu Rehema Said Lukindo, Sostenes Ndoshi, Henry Enock pamoja pamoja na mwenyekiti wa kamati ndogo ya kufuatilia fedha za walimu hao, aliyejitambulisha kwa jina moja la Wanga, ni miongoni mwa walimu waliolalamikia hali hiyo, huku wakitishia kuacha kazi hiyo ya ualimu na kujiunga na kazi nyingine.

“Leo tumeshinda hapa jiji tukifuatilia kulipwa mishahara yetu, na hata darasani leo hatujaingia kabisaa!. Lakini cha ajabu tunapewa fedha kidogo tofauti na mishahara yetu halisi iliyoidhinishwa na Serikali.

“Kwa mfano, mwalimu wa digrii anapaswa alipwe mshahara wa sh. 469,200 lakini leo hii analipwa na jiji sh. 404,600. Hizi fedha nyingine wanazikata na kuzipeleka wapi?.

“Kwa nini tunyanyasike hivi?. Hakianani mimi nikipata kazi nyingine hata ya kuanzia 700,000 nitaacha ualimu kabisa, maana huu ni ufisadi wa wazi. Mwalimu ataishije kwa mshahara mdogo kama huu?. Na tumeambiwa hapa jiji bila kugoma hatupati haki zetu”, alilalamika mwalimu Rehema Lukindo kisha kuungwa mkono na walimu wenzake.

Hata hivyo, walimu hao walisema, hadi waanze kazi Januari Mosi mwaka huu, Serikali kupitia jiji la Mwanza haijawalipa fedha zao za nauli na mizigo, tofauti na ilivyoelezwa na Serikali kwamba jumla ya sh. bilioni 6.2 zilishapelekwa jijini Mwanza kwa lengo la kulipa madai ya walimu hao ya fedha za nauli na mizigo wakati wakienda kuripoti na kuanza kazi rasmi.

Walisema, kwa mtindo huo walimu wameanza kukata tamaa ya kufundisha wanafunzi darasani, na kwamba kamwe kiwango cha elimu nchini kitazidi kushuka kila kukicha kwani walimu wameshaanza kukata tamaa ya kujituma katika kazi zao.

“Kama hali ndiyo hii inatukatisha tamaa kabisa walimu kuingia na kushika chaki darasani kufundisha!. Na hata kiwango cha elimu kitazidi kudorola zaidi, maana mwalimu akiingia darasani hawazi tena kufundisha vizuri, bali atakuwa akiwaza ukata wa maisha na ataishije”, alisema mwalimu Sostenes Ndoshi ambaye pia aliungwa mkono na walimu wenzake kwa kauli yake hiyo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Jiji la Mwanza, Wilson Kabwe alipozungumza leo na mwandishi wa habari hizi akiwa nchini Uganda, alikiri walimu hao kukatwa mishahara yao, ambapo aliwashangaa pia walimu hao kulalamikia makato ya fedha zao hizo.

“Hawa walimu ni watumishi wa Serikali, na lazima wakatwe kodi ya Serikali. Hatuwezi kuwalipa mshahara wote kama wanavyotaka wao…tukifanya hivyo watakuwa hawalipi kodi. Nawashangaa sana maana pale jiji kuna wataalamu sana wa mahesabu, hawawezi kumpunja mtu haki yake”, alisema Mkurugenzi Kabwe kwa njia ya simu yake ya kiganjani kutoka nchini Uganda.
Habari hii imeandikwa na Sitta Tumma – Mwanza.

1 Comment
  • tatizo la watanzania ni kutokuthamini hali ya mtz mwenzake yaani kila aliyejuu kila kitu ni chake labda watabadilikaga sikumoja..

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *