Walinzi mgodini wafanya unyama, wamng’oa mtu meno

Jamii Africa

WALINZI wa kampuni ya uchimbaji madini ya Tancan Mining Limited inayoendesha shughuli zake katika mgodi wa dhahabu wa Buckreef Wilayani Geita Mkoani Geita, wamempiga na kumvunja meno mawili, Agustino Kapiku (22), mkazi wa kijiji cha Mnekezi wilayani humo.

Agustino Kapiku (22), akiwa amefungwa bandeji katika shavu aliloshonwa baada ya meno yake mwaili kuvunjwa kwa kipigo na walinzi wa mgodi wa Buckreef, Geita jana. (Picha na Sitta Tumma).

Tukio hilo limetokea baada ya walinzi wanne wakiwa na silaha aina ya marungu na bunduki moja, kumkuta Kapiku akifukuza ndege kwenye shamba la mpunga lililopo jirani na mgodi huo kisha kuanza kumshambulia kwa madai kwamba ameingia ndani ya eneo la mgodi huo bila kibali maalumu.

Akizungumza leo na FikraPevu kwa shida hospitali ya wilaya ya Geita alipolazwa, Kapiku alisema akiwa katika shamba hilo la mpunga akifukuza ndege wasile mazao yake, alivamiwa na walinzi hao kisha kuanza kupigwa bila sababu zozote jambo ambalo lililosababisha kumvunja meno yake.

Alisema, baada ya walinzi hao kugundua wamemuumiza vibaya walianza kumburuza chini kwa lengo la kumtupa mtoni, na kwamba alikuwa akipiga mwano na kelele akisaidaiwa na  watu waliokuwepo jirani wakivuna mpunga, na ndipo walipomtelekeza na kukimbia.

“Nilipigwa sana na walinzi wa mgodi huu wa Buckreef bila sababu zozote. Walinikuta ninafukuza ndege kwenye shamba langu la mpunga ndipo wakaanza kunishambulia na kunivunja meno mawili”, alisema Kapiku huku akitokwa machozi.

Alisema, baada ya kupigwa na kujeruhiwa vibaya na walinzi hao, baadaye aliokotwa na wasamaria wema ambao walimbiza hadi kwenye Kituo kidogo cha Polisi cha Buckreef, kwa ajili ya kupewa huduma ya kwanza.

Akisimulia zaidi alisema: “Nimetoa taarifa polisi juu ya kipigo, na nimepewa PF3 ambapo baadaye nilipelekwa katika kituo cha Afya cha Katoro Geita kwa gari la kampuni hiyo.

“Lakini waliponifikisha kwenye kituo hicho cha afya Katoro walinipa sh. 14,000 na kisha wakakaondoka hadi nilipokuja kuchukuliwa na shemeji yangu na kunileta hapa hospitali ya Wilaya jioni”.

Akithibitisha jana kuwepo kwa tukio hilo, mkuu wa kitengo cha tiba ya meno katika hospitali ya Wilaya ya Geita, Dk. Baraka Sinde aLIsema kuwa Kapiku alivunjika meno mawili ya taya la juu, ambapo ameshonwa nyuzi kadhaa kwenye shavu lake la kulia.

“Ni kweli huyu majeruhi amevunjwa meno yake mawili…kwa kutumia utaalamu wetu tulilazimika kumshona. Lakini vipande vya meno vilivyobaki tulivitoa baada ya uvimbe kupungua”, alisema Dk. Sinde.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Geita, Leonard Paul (RPC), amethibitisha kuwepo kwa tukio hilo, na kwamba jeshi lake bado linafanya uchunguzi kwa ajili ya kubaini chanzo cha tukio hilo, hivyo baada ya uchunguzi huo atalitolea ufafanuzi wa kina na hatua zote za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watuhumiwa.

Naye Ofisa Uhusiano wa kampuni hiyo ya Buckreef, Anna Haule alithibitisha kutokea kwa tukio hilo, na kusema kwamba: “Kampuni inafuatilia kwa karibu kuhusu huduma ya matibabu anayopatiwa majeruhi huyu”.

Matukio ya wananchi wanaoishi karibu na maeneo ya migodi kupigwa ovyo pamoja na kuuawa kwa kupigwa risasi na askari polisi na walinzi wa migodi hiyo ya wawekezaji, imeonekana kuanza kushamiri nchini.

Hivi karibuni watu wawili wakazi wa wilaya ya Tarime mkoani Mara, waliripotiwa kuuawa kwa kupigwa risasi na askari polisi wanaolinda mgodi wa North Mara-Nyamongo, ambapo pia mwaka jana watu watano waliripotiwa kuuawa na polisi huko North Mara.

Mbali na hayo, hivi karibuni iliripotiwa mwanafunzi mmoja alipigwa risasi na walinzi wa mgodi wa GGM uliopo Geita, ambapo tukio lililofuata wiki iliyopita mtu mwingine tena alijeruhiwa kwa risasi na walinzi hao wa GGM, ukiachilia mbali na tukio hili la jana.

Kwa maana hiyo, upo ulazima sasa Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kuhakikisha inakomesha unyama huo wanaofanyiwa Watanzania katika nchi yao, na kwamba wahusika wote wa matukio hayo hapana shaka wachukuliwe hatua kali za kisheria.

Habari hii imeandikwa na Sitta Tumma – FikraPevu, Mwanza.

2 Comments
  • Wanamwaga damu ya wenye nchi kisha wanapora rasilimali yao!!polisi wapo mijini wanalinda maduka ya wahindi na benki zilipohifadhiwa pesa zao hizo za damu! Watawala wetu wapo ndani ya 5stars hotels wakisubiri mgao wao mara baada ya zoezi la kuua raia na kuwapora dhahabu na almasi zao,litakapo kamilika, yaani rasilimali ile tuliyodhani kuwa ni zawadi toka kwa mungu,imegeuka na kuwa laana kuu!!inyonyayo na kukausha damu ya watanzania wale masikini,ikiwafanya waishi kwa hofu kuu,wao na vizazi vyao,umeuficha wapi uso wako Ee Mungu?,wapi ulipozitupia hasira zako?

  • jamani watanzania tumgeukie Mungu wetu,u wapi ubinadamu wetu? Tazama watu wasio na hatia wanvyoteseka na rasilimali za nchi yao.mbona tahusikii wanaoiba wanyama,epa n.k hawauawi?mtoto wa miaka 22 itaiba nini jamani!jifunzeni kwanza kabla kuchukua hatua.askari wetu wamekuwa wadudu wanaotisha miongoni mwa jamii yetu.matukio mengi ya umwagaji damu yanawahusu wao

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *