Shirika la Taifa La Hifadhi ya Jamii (NSSF) Wilaya ya Ilala linaendelea na uchunguzi wa wanachama ambao wamefungua madai ya kulipwa mafao baada ya kuachishwa kazi na waajiri ili kubaini wanachama wenye sifa za kupata mafao hayo
Hali hiyo ilijitokeza leo katika ofisi za shirika hilo zilizopo Wilaya ya Ilala ambapo wanachama wa NNSF walijitokeza kufuatilia mafao yao baada ya kujaza fomu za madai lakini hawakupata majibu ya kuridhisha ikizingatiwa kuwa wamekuwa wakifuatilia madai hayo muda mrefu bila mafanikio.
Akijibu malalamiko ya wanachama hao, Afisa anayeshughulikia madai ya wanachama ambaye jina lake tunalihifadhi amesema shirika linaendelea kufanya uchunguzi ili kujiridhisha kama kweli maombi yaliwasilishwa ni ya wanachama walioachishwa kazi na waajiri wao.
Amesema kumekuwa na maombi mengi ya wanachama ambao wataka walipwe mafao yao huku wengine wakiwa bado wako kazini au wameacha kazi kwa hiari yao wenyewe. Kutokana wanafuatilia kwa karibu kubaini wanachama wenye sifa ya kupata mafao yao na ikibainika kuwa kuna wanachama waliacha kazi kwa hiari au bado wako kazini hawatapata mafao yao mpaka wafikishe miaka 55.
“Tunaendelea na uchunguzi kwahiyo muwe na subira mtapata mafao kwa wakati”, amesema Afisa huyo wakati akimjibu mmoja wa wateja ambaye alifungua madai septemba mwaka huu baada ya kuachishwa kazi na mwajiri wake.
Kulingana na Sheria ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya mwaka 2012 inaeleza kuwa mwanachama mwenye haki ya kupata mafao ni yule aliyefikisha miaka 55. Sifa nyingine ni mwanachamaaliyeachishwa kazi na mwajiri wake na anapaswa kusubiri kipindi cha miezi 6 ndipo afungue madai ya kulipwa mafao.
Mwanachama wa shirika hilo wilaya ya Ilala, Issa (jina la pili tumelihifadhi) alimuuliza Afisa huyo ni lini uchunguzi huo utakamilika alijibiwa kuwa wanapaswa kuwa nasubira kwasababu haijulikani utakamilika lini. Majibu hayo yaliibua jazba na minong’ono ya wanachama waliokuwepo ofisini hapo huku wengine wakilalamika kuwa wamezungushwa kwa mwaka mmoja bila kupewa mafao yao.
Juma Ulasa (jina pili sio lake), mwanachama wa NSSF anasema alikuwa anafanya kazi katika kampuni ya ujenzi inayomilikiwa na raia wa China yenye makao yake Mikocheni, Dar es Salaam, lakini baada ya kutoelewana na bosi wake alifukuzwa kazi mwezi Agosti mwaka jana.
Anasema alifungua madai ya kulipwa fedha zake wilaya ya Kinondoni na akaambiwa asubiri kwa muda miezi sita huku madai yake yakishughulikiwa. Baada ya miezi sita aliwasiliana tena na ofisi hiyo na aliongezewa muda wa miezi 3 ya kusubiri wakati madai yake yakishughulikiwa.
Miezi mitatu ilipoisha, alipata jibu kuwa mwajiri wake ameamisha mafao yake wilaya ya Ilala na anapaswa kufungua madai mengine huko, “Nilifungua madai mengine Ilala septemba, 2017 baada ya kuzungushwa kwa mwaka mmoja”, amesema Juma ambaye siku ya leo amerudi tena kufuatilia mchakato wa madai yake.
Naye Judith Lukas (jina pili sio lake) ambaye anafuatilia fao la uzazi anasema alifungua madai oktoba mwaka huu akiwa mjamzito lakini sasa umepita miezi miwili tangu ajifungue mtoto wa kiume na hajapata mafao yake.
“Nina mtoto mdogo ambaye ana miezi miwili, nazunguka naye kufuata malipo yangu lakini bado wananizungusha, labda leo watanipa maana wamesema hundi iko tayari”, amesema Judith ambaye analalamikia utaratibu wa ofisi hiyo ambao hautoi majibu ya uhakika kwa wanachama wake.
Mfanyakazi wa NSSF Wilaya ya Kinondoni ambaye anahusika na huduma kwa wateja amesema wanachama wa shirika hilo wanatakiwa kutambua kuwa utaratibu umebadilika na sheria zinatakiwa zifuatwe na kuachana utaratibu wa zamani ambapo wale waliochishwa kazi walikuwa wanapata mafao yao ndani ya wiki tatu.
Ameongeza kuwa kwa sasa wanalipa wanachama ambao walifungua madai kabla ya mwezi June mwaka huu na wakikamilisha wataendelea na wanachama wengine.
Inaelezwa kuwa malalamiko ya wanachama wa mashirika ya hifadhi ya jamii ni matokeo ya kutopata elimu sahihi ya mabadiliko ya sheria na kutambua umuhimu wa mafao hayo kutunza hadi watakapofikisha umri wa miaka 55 ili fedha hizo ziwasaidie wakiwa na umri mkubwa.
Mabadiliko ya Sheria
Ili kuboresha utendaji wa mifuko ya hifadhi ya jamii, serikali inakusudia kuifanyia marekebisho sheria hiyo ambapo imekuja na mswada mpya ambao utapelekwa bungeni ili ujadiliwe na kupitishwa. Mabadiliko hayo ni pamoja na kuiunganisha mifuko yote ya jamii na kubaki na miwili itakayoweza kuwahudumia wananchi kwa ufanisi. Mabadiliko mengine ni kukatwa kodi kwenye mafao ya wastaafu.
Hata hivyo, mabadiliko hayo yameibua mijadala baina ya wananchi na wanasiasa ambapo kumekuwa na mitazamo tofauti juu ya utendaji wa mifuko ya jamii ambayo imeanza kuwekeza fedha zake kwenye sekta ya viwanda kufuatia agizo la rais John Magufuli kuitaka mifuko hiyo kushiriki katika kujenga uchumi wa viwanda.
Zitto Kabwe, Mbunge wa Kigoma Mjini amesema, “sheria ya sasa ya pensheni kwa watumishi wa umma kifungu cha 7 kinazuia kodi ya Mapato kukatwa kwa mlipwa pensheni kwa mafao yeyote atakayolipwa. Muswada wa sheria mpya kifungu cha 47(3) kinaelekeza mstaafu kukatwa kodi kwenye pensheni yake,
“Kwanza mtumishi kwenye uhai wake wote akifanya kazi alikuwa analipwa PAYE mpaka 30% ya mshahara wake kwa mwezi. Sheria mpya inataka akistaafu wakati anaipwa kiinua mgongo alipe tena 30% kodi ya Mapato kwa kipato ambacho ameshakilipia kodi wakati anafanya kazi”.
Zitto amabye ni mjumbe wa kamati ya Bunge ya huduma za jamii amesema muswada huo utawaumiza wananchi na amewataka wabunge kutokuupitisha kabla ya kujidhirisha ikizingatiwa kuwa watumishi wanaostafu watalazimika kodi mara mbili.
Kwa upande wake, Wakili Albert Msando amesema mabadiliko ya sheria hiyo hasa kifungu cha 47 (3) hakikusudii kumkata kodi mtumishi wa umma lakini ni hatua muhimu ya kuboresha utendaji wa mifuko ya jamii.