Wanafunzi hawa wanafanyishwa vibarua

Albano Midelo

Wanafunzi wa shule ya msingi Ndingine mwambao mwa ziwa Nyasa wilayani Mbinga mkoani Ruvuma wakifanyishwa kazi ya  kusomba tofali muda wa masomo.

LICHA ya serikali kupiga marufuku walimu  kuwafanyisha vibarua wanafunzi wakati wa masomo,bado baadhi ya shule hasa katika maeneo ya vijijini,zinaendelea na tabia hiyo hali ambayo inachangia kuzorotesha elimu nchini.

Uongozi wa shule ya msingi Ndingine iliyopo kata ya Ngumbo mwambao mwa ziwa Nyasa wilayani Mbinga mkoani Ruvuma bado unaendelea kuwafanyisha vibarua wanafunzi licha ya  afisa elimu wa wilaya hiyo kupiga marufuku jambo hilo.

Uchunguzi ambao umefanywa na mwandishi wa habari hizi katika kijiji cha Ngumbo hivi karibuni ulibaini wanafunzi baadhi wakiondolewa madarasani tena majira ya asubuhi na kwenda kufanyishwa kibarua cha kubeba tofali za kuchoma kutoka kwenye tanuli lililokuwa mtoni hadi mahali ambapo nyumba inajengwa umbali wa kilometa tatu.

Wanafunzi wa darasa la  tatu na la sita kutoka shule hiyo walishuhudiwa wakisomba tofali hadi nne kichwani huku wakilalamika kuwa wanafanya kazi ambayo hawanufaiki nayo licha ya kuambulia maumivu kutokana na mzigo na umbali.

Baadhi ya wanafunzi wanasoma darasa la sita walipohojiwa ,walidai kuwa mwalimu amewaambia huo ni mradi wao ambao utawawezesha kupata fedha kwa ajili ya sherehe za mahafali ya kumaliza elimu ya msingi hapo mwakani watakapomaliza darasa la saba.

Hata hivyo wanafunzi wa darasa la tatu walilalamika kuwa wao wamelazimishwa na mwalimu kwa kuwa hawapati chochote na kwamba fedha zote wanachukua walimu,ingawa tofali zinachangia kuchafua sare zao za shule ambazo wakirudi nyumbani inawalamu wazazi kununua sabuni ili kufua nguo zao.

Miongoni mwa wazazi waliohojiwa kuhusiana na watoto wao kuendelea kufanyiwa kazi za vibarua,waliomba serikali ya wilaya kuwachukulia hatua walimu wa kata za Ngumbo na Liwundi kwa kuwa wamezoea kuwafanyisha kazi wanafunzi wao licha ya wazazi na walezi kukataa.

“Sisi wazazi kwenye vikao tulishakubaliana  tutachangia shilingi 2000 kila mzazi ,walimu waache tabia ya kuwafanyisha kazi watoto wetu badala yake waendelea na kusoma lakini walimu bado wanaendelea kuwafanyisha kazi mbalimbali wanafunzi kama vile kuchota maji ya walimu,kubeba tofali,kukata matete,kubeba kuni  pamoja na kazi nyingine nyingi’’,alisema Martha Nchimbi mkazi wa Mkili.

Hata hivyo mwalimu mkuu wa shule ya msingi Ndingine Aidan Mbilinyi alipohojiwa kuhusiana na kuwafanyisha kazi  za vibarua wanafunzi alidai kuwa katika shule yake wanafunzi hawafanyishwi vibarua badala yake wazazi wanachangia kila mwaka shilingi 2000 kwa ajili ya sherehe za mahafali ya darasa la saba .

Katika kikao cha walimu wakuu wote wa wilaya ya Mbinga ambacho kiliitishwa na  idara ya elimu chini ya mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga Septemba 23 mwaka huu pamoja na mambo mengine waliazimia  kuacha kuwafanyisha vibarua wanafunzi vikiwemo kusomba tofali na kuvuna kahawa.

Afisa elimu wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga David Mkali amekemea tabia  ya walimu  wakuu kuendelea kuwafanyisha kazi wanafunzi na kusisitiza kuwa kuanzia sasa atachukua hatua za kinidhamu kwa walimu wakuu wote ikiwa ni pamoja na kuwashusha vyeo vyao.

“Maazimio yalipitishwa tangu mwezi Septemba mwaka huu  marufuku wanafunzi kufanyishwa  vibarua,shule zibuni miradi ya kujitegemea itakayowawezesha kupata fedha,pia walimu kuwapatia wanafunzi maarifa ya kujitegemea kwa mfano kulima bustani baada  ya  saa za masomo’’,alisisitiza.

Mkali aliyataja mambo ambayo yamechangia kushuka kwa elimu na ufaulu kwa wanafunzi wa shule za msingi wilayani Mbinga kuwa ni pamoja na wanafunzi kufanyishwa vibarua,utoro na ulevi kwa baadhi ya walimu,walimu kutofundisha siku zote 195 zilizopangwa na wizara,walimu wakuu kutofuatilia ufundishaji,ukaguzi wa maandalio na kazi za watoto.

Takwimu   zilizokusanywa katika shule 321 katika Halmashauri ya wilaya ya Mbinga kuanzia darasa la tatu hadi la saba zinaonesha kuwa  wanafunzi 15,128 kati ya 116,966 hawajui kusoma,kuandika na kuhesabu.

7 Comments
  • Hali hii ni yakawida sana especially maeneo ya huko vijijini, viongozi wapo lakini they dont care, watoto wao wanasoma ulaya, issue ni kwa watoto wa walala hoi na wanyonge. it’s so sad! afisa elime awajibishwe.

  • Jamani jamani wa Tanzania kwa hali hi tutafika kweli? maafisa limu mkowapi? daaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaa!

  • This is what we call Bongo bhaaaaaaaaaaana! wanafunzi wakifeli nanai wakulaumiwa? je ni mwalimu au mwanafunzi? au ni mzaziiiiiiiiiii!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *