Katavi: Wanafunzi wa madarasa mawili tofauti watumia chumba kimoja, ubao mmoja, wengine chini ya mti

Jamii Africa

WANAFUNZI wa madarasa mawili tofauti katika Shule ya Msingi Kawanzige katika Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi wanalazimika kutumia chumba kimoja na ubao mmoja kwa wakati mmoja kufundishiwa huku wengine wakisomea chini ya miti kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa, FikraPevu inaripoti.

Uchunguzi wa FikraPevu unaonyesha kwamba, wanafunzi wanaotumia chumba kimoja ni wa darasa la sita na darasa la tatu.

Shule  hiyo yenye wanafunzi 917 ilianzishwa mwaka  2008 na ilikuwa na walimu wa kujitolea hadi mwaka 2011 ilipopata walimu wa kuajiriwa, ambapo ina madarasa ya kuanzia la awali hadi la saba.

Mwalimu wa Shule ya Msingi Kawanzige Manispaa ya Mpanda akifundisha madarasa mawili tofauti darasa la sita lenye wanafunzi 71 na darasa la tatu lenye wanafunzi 183 wakisoma kwa wakati mmoja wengine wakiwa wamekaa chini, kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa na upungufu wa madawati.

Mwalimu Mkuu Msaidizi wa shule hiyo, Ajaye Patrick, aliiambia FikraPevu ilipotembelea shuleni hapo kwamba, shule hiyo licha ya kuwa na matokeo mazuri ya ufaulu wa mitihani ya kumaliza darasa la saba kwa vipindi vya miaka miwili mfululizo, lakini bado inakabiliwa na changamoto nyingi hususan uhaba wa vyumba vya madarasa.

Mwaka 2015, kwa mujibu wa mwalimu Patrick, shule hiyo ilishika nafasi ya kiwilaya na mwaka 2016 ilishika nafasi ya tatu.

“Uhaba wa vyumba vya madarasa unawalazimu wanafunzi wa madarasa mawili tofauti kusomea chumba kimoja kwa wakati mmoja huku wakitumia ubao mmoja pia,” alisema Mwalimu Patrick.

Wanafunzi wa darasa la sita ambao wako 71 na darasa la tatu lenye  wanafunzi 183 husoma kwa wakati mmoja kwa kutumia chumba kimoja cha darasa, jambo linaloleta ugumu kwa kujifunza na kufundisha.

Pia darasa la nne lenye wanafunzi 97 na darasa la tano lenye wanafunzi 72 nao wanalazimika kusomea chumba kimoja.

Mwalimu Patrick alisema, hali hiyo inawapa ugumu wanafunzi hao pamoja na walimu wanaofundisha, kwani vipindi vyao huenda kwa wakati mmoja hivyo kukosekana kwa umakini kwa wanafunzi na walimu.

Aidha, alisema baadhi ya wanafunzi wanalazimika kusomea chini ya miti na pindi mvua zinaponyesha hulazimika kusimamisha vipindi na wanafunzi hao hukimbilia majumbani kwa vile kwenye vyumba vingine wenzao huwa wanaendelea na vipindi.

Changamoto nyingine aliitaja kuwa ukosefu wa nyumba za walimu ambapo licha ya shule hiyo kuwa na walimu 12, lakini hakuna hata nyumba moja ya walimu huku wote wakiwa wanaishi nyumba za kupanga hapo kijijini na wengine katika kijiji cha jirani cha Kakese kilichoko umbali wa kilometa nne kutoka shuleni hapo.

Mwanafunzi John Maganga anayesoma darasa la tano shuleni hapo, alieleza kwamba wamekuwa wakifundishwa ndani ya chumba kimoja madarasa mawili tofauti kwa wakati mmoja.

Alisema walimu wao hutumia ubao mmoja ambapo wakati mmoja anaandika ubaoni kwa ajili ya darasa lake, mwingine hutoa kazi za vitabuni kwa darasa linalomhusu.

Diwani wa Kata hiyo, Maganga Salaganda, alieleza kuwa pamoja na shule hiyo kuwa na changamoto hizo, walimu wamekuwa wakiendelea kufanya kazi kwa moyo mkubwa na ndiyo maana shule imekuwa ikifanya vizuri.

“Nguvu ya serikali pamoja na wananchi inahitajika sana ili kuboresha miundombinu ya shule na kutatua changamoto zilizopo ambazo zimekuwa kero kubwa kwa wanafunzi na walimu,” alisema diwani huyo.

 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *