Wanaharakati waitaka serikali kufuta adhabu ya kifo

Jamii Africa

Kituo cha Sheria na  Haki za binadamu (LHRC) wameitaka serikali kuifanyia marekebisho Sheria ya Kuzuia Ugaidi ya mwaka 2002 ambayo inatoa adhabu ya kifo kwa makosa ya mauaji, uhaini na ugaidi.

Hatua hiyo inakuja siku chache baada ya Rais John Magufuli kutangaza uamuzi wake wa kupinga adhabu ya kifo ambapo alisema kuwa anapatwa na kigugumizi kusaini hukumu za wafungwa ambao wamehukumiwa kunyongwa baada ya kukutwa na makosa mbalimbali.

“Sisi wanasiasa tunaogopa kunyonga, natambua kuwa sasa orodha ya watu ambao wanatakiwa kunyongwa ni kubwa sana ila mimi naomba hiyo orodha msiniletee kwasababu najua ugumu wake ulivyo,” alinukuliwa Rais John Magufuli.

Akizungumza na waandishi wa habari, leo jijini Dar es salaam, Naibu Mkurugenzi Mtendaji  wa LHRC, Ana Henga amesema kuwa adhabu hiyo ni ya kikatili ambayo inakinzana na misingi ya utu na misingi ya haki za binadamu kama ilivyoainishwa katika matamko na mikataba mbalimbali ya Kimaifa ambayo Tanzania imeridhia kuyatekeleza.

“Serikali irekebishe sheria ya kanuni na sheria ya adhabu ya ugaidi yenye kutoa adhabu ya kifo kwa makosa ya mauaji, uhaini na ugaidi” amesema Henga na kuongeza kuwa

“Serikali itekeleze pendekezo la mpango wa kujitathmini wa nchi wanachama wa umoja wa Mataifa(universal periodic review) mwaka 2016 kwa kuridhia mkataba wa nyongeza wa haki za kiraia na kisiasa na kutangaza rasmi sasa kuwa haitekelezi adhabu ya kifo”.

Sheria ya Kanuni za Adhabu, Sura ya 16 ya sheria za Tanzania, kifungu 197 kinaeleza kuwa mtu yeyote atakayepatikana na hatia ya kuua atahukumiwa adhabu ya kifo.

Pia serikali imetakiwa kuondoa adhabu ya kifo na kuweka adhabu mbadala kwenye makosa yote ya jinai ambayo washitakiwa wanahukumiwa kunyongwa. Nia ya Rais ni nzuri na anastahili pongezi kwa uamuzi wake lakini ili uamuzi wake uwe na maana achukue hatua ya kupeleka mapendekezo bungeni ili sheria zote zinazotoa adhabu ya kifo zibadilishwe.

“Serikali ibadilishe sheria na kuondoa adhabu ya kifo na kuweka adhabu mbadala kwenye makosa ya jinai. Kwa vile utekelezaji wa sheria hii una mkera Rais basi awe kinara katika kuitisha mabadiliko haya ili yeye na Majaji waondolewe mzigo wakutekeleza adhabu hii mbaya na kutweza utu wa mtu”, amesema Henga

Adhabu ya kifo inakiuka tamko la Kimataifa la Haki za Binadamu la mwaka 1948 ambalo linatamka kuwa kila mtu ana haki ya kuishi bila kujali hali aliyonayo, na nchi wahisani zinahimizwa kutekeleza mkataba huo.

Takwimu za ripoti ya Haki za Binadamu ya mwaka 2016 zinaonyesha kuwa hadi kufikia 2015 watu 472 walihukumiwa adhabu ya kunyongwa ambapo wanaume walikuwa 452 na wanawake 20. Tanzania ni miongoni mwa nchi chache duniani ambazo zinatambua adhabu ya kifo katika sheria zake. Nchi nyingine China, Marekani na Korea.

Kitanzi kinachotumika kunyongea watu

Utekelezaji wa adhabu ya kifo duniani

Kulingana na ripoti ya shirika la Amnesty International ya mwaka 2017 inakadiriwa kuwa watu 1,032 walinyongwa katika nchi 23 mwaka 2016 na idadi hiyo imepungua ikilinganishwa mwaka 2015 ambapo walinyongwa watu 1,634 katika nchi 25 duniani kote.

Adhabu hiyo ilitekelezwa zaidi katika nchi za China, Saudi Arabia, Iraq na Pakistan. China inabaki katika nafasi ya juu miongoni mwa nchi zinazotekeleza adhabu ya kifo na inaelezwa kuwa taarifa za watu kunyongwa nchini humo huwa ni za siri. Kutokana na ukweli huo idadi ya watu wanaonyongwa katika nchi hiyo ni kubwa zaidi kuliko ile inayotajwa katika ripoti za mashirika ya haki za binadamu.

Ukiondoa China asilimia 87% ya watu wote walionyongwa mwaka 2016 walitokea kwenye nchi nne za Iran, Saudi Arabia, Iraq na Pakistan.

Kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2006, Marekani haikuwa miongoni mwa nchi 5 zenye idadi kubwa ya watu wanaonyongwa, ilishuka hadi katika nafasi ya 7 nyuma ya Misri. Walinyongwa watu 20 pekee ambapo ni idadi ndogo tangu mwaka 1991.

Kwa mwaka 2016, nchi 23 zilitekeleza hukumu ya kifo. Idadi hiyo imepungua katika miaka 20 iliyopita ambapo nchi 40 zilikuwa zinatekeleza adhabu hiyo mwaka 1997.

Mwaka 2016, nchi za Belarus, Botswana, Nigeria na Parestina zilirejea tena kutoa adhabu ya kifo baada ya kutokuitekeleza kwa muda mrefu. Lakini nchi za Chad, India, Jordan, Oman na Dubai ambazo zilitekeleza adhabu ya kifo mwaka 2015 ilipofikia mwaka 2016 hazikuripotiwa kutekeleza adhabu hiyo.

Nchi 141 duniani sawa na robo tatu ya nchi zote zimeachana na adhabu ya kifo na kufuta kabisa sheria zinazohusu kifo.

 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *