Wananchi wanapotaka waganga watatue shida zao

Sifa Lubasi

MWAKA jana Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Betty Mkwasa alikumbwa na zomeazomea ya wananchi wa Wilaya hiyo baada ya kupiga marufuku waganga wa kutoa uchawi kufanya kazi zao ndani ya Wilaya hiyo.

Wananchi hao walikuwa wakitaka waganga hao waruhusiwe kufanya kazi ya kutoa uchawi ndani ya Wilaya hiyo huku DC huyo akiwa hakubaliani na maamuzi hayo.

Kwa mujibu wa mkuu huyo wa Wilaya  alisema kamwe hatakubali kubadilisha uamuzi huo kwani anataka wananchi waachane na mambo ya kishirikina na wafuate shughuli za maendeleo.

Kwa muda mrefu Dodoma umekuwa ni miongoni mwa mikoa ambayo inavamiwa na waganga wa kutoa uchawi maarufu kama lambalamba lakini tatizo hilo linaonekana kupungua kutokana na juhudi mbalimbali zinazofanywa katika kuhakikisha waganga hao wanaondoka.

lambalamba

Waganga wa kutoa uchawi maarufu kama lambalamba wakiwa nje wa kituo kikuu cha polisi mkoani Dodoma baada ya kukamatwa.

Juhudi hizo ni pamoja na kuelimisha wananchi ili kuweza kuachana na imani potofu.
Pia kuna juhudi zilizofanywa na Mkuu wa Mkoa ili kufukuza waganga hao, juhudi ambazo mara kadhaa zilikuwa zikigonga ukuta kutokana na wananchi kutaka waganga hao watatue shida zao.
Katika eneo la Gawaye Manispaa ya Dodoma wananchi walikuwa wakishindwa kwenda kwenye shughuli za uzalishaji mali na kupanga foleni kwa waganga kwa lengo la kutatuliwa matatizo yao.
Hilo pia lilisababisha kuzorotesha uchumi kwenye ngazi ya kaya.

Mmoja wa watu wanaofanya kazi ya lambalamba, Majuto Mohamed anasema wamekuwa wakizunguka Vijiji mbalimbali vya mkoa wa Dodoma kwa nia ya kutoa pepo wabaya kwenye nyumba.

“Kama kuna Fisi au nyoka tunamtoa baada ya kufanya kazi yetu  na huwa tunafanya hivyo baada ya  wananchi au viongozi wa vijiji au vitongoji  kukubaliana” anasema.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dk. Rehema Nchimbi anasema waganga hao hawastahili kuwemo katika jamii kwani wamekuwa wakitapeli wananchi fedha zao kwa madai ya kutoa uchawi huku wakifanya unyanyasaji mkubwa wa kijinsia kwa wanawake.

Anasema licha ya kupita kila Kaya kukusanya fedha za kutoa uchawi pia wamekuwa wakichagua wanawake kila kijiji wanapofika kuweka kambi ili kuwapikia na hata kulala nao.

Anasema aliwahi kupata malalamiko kuwa baadhi ya vijiji ambapo lambalamba hao kabla ya kuinga ndani lazima wanawake waliovua nguo wawe mlangoni ambapo huwaruka kisha kuingia ndani.

Dk Nchimbi anasema huo ni udhalilishaji mkubwa kwa wanawake na jamii inatakiwa kukemea vitendo hivyo kwa nguvu zote.

Mkuu wa Wilaya ya Chamwino Fatma Ally anasema lambalamba hao wamekuwa wakitumia uelewa mdogo walionao wananchi li kuwarubuni na kisha kuwatapeli.

Anasema miongoni mwa Wilaya zilizoathirika na tatizo la lambalamba katika mkoa wa Dodoma ni Chamwino kutokana na baadhi ya viongozi wa vijiji kuwaruhusu kufanya kazi hizo.

Godfrey Wambali ni mwanasheria kutoka Ofisi ya Mwanasheria wa Serikali kanda ya kati Dodoma anasema kuna sheria inayozungumzia vitendo vya uchawi.

Wambali anasema Sheria ya uchawi (Witch craft Act ) namba 12 ya mwaka 1998 , kwenye kifungu cha 3 cha sheria hiyo kinaongelea vitendo hivyo ambavyo ni makosa.

Anasema mtu yoyote kutumia kauli yake vitendo na kujifanya ana nguvu za uchawi, anayefanya , anayetumia au kujifanya ana vifaa vya uchawi, kusambaza kwa watu wengine kushawishi watu wengine kujiunga na uchawi,kutishi kutumia uchawi wote wanakuwa wamefanya makosa chini ya kifungu hicho cha sheria.

Pia anasema kifungu cha tano cha sheria hiyo kinaongelea adhabu ambapo mtu yoyote anayetenda vitendo vilivyotajwa katika sheria hiyo , kusababisha kifo, ugonjwa, majeraha,msiba au balaa lolote katika jamii au jumuia ya watu fulani kwa mtu pekee mnyama au kusababisha uharibifu wa mali yoyote na kutaja kuwa mtu mchawi anastahili kupata adhabu isiyopungua miaka saba.

Mwanasheria huyo anasema mtu ambaye anafanya makosa yaliyopo ndani ya sheria hiyo pasipo kujua adhabu yake ni faini ya Sh. 100,000 au kifungo kisichopungua miaka mitano

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Kamishna Msaidizi  Mwandamizi wa Polisi (SACP) David Misime anasema lambalamba ni tatizo kubwa katika Mkoa wa Dodoma kutokana na watu kadhaa kukamatwa wakijihusisha na vitendo hivyo.

Anasema watu hao walikuwa wakijihusisha na vitendo vya kishirikina kwa kujifanya wanaagua na kufichua wachawi katika Vijiji mbalimbali.

Waliokamatwa walikuwa wakitoka mikoa ya Mtwara,Lindi, Dar es Salaam.

Anasema mbinu walizokuwa wakitumia watu hao ni pamoja na kuwaita watu wachawi na kuchukua fedha zao kwa nguvu .

Anawataka wananchi kuacha kushabikia vitendo hivyo kwani ni njia waliobuni watu hao kwa lengo la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, kudhalilisha na kujenga chuki ndani ya jamii kutokana na kuwaita wengine wachawi.

Mwenyekiti  Chama cha Waganga wa Tiba za Asili na Wakunga wa Jadi (CHAWATIATA) Mkoa wa Dodoma Issa Mohamed Mdoe anasema chama kinawatambua waganga wa kutoa uchawi maarufu kama lambalamba ni wahuni kwani hakuna mganga anayeunda kikundi, kazi ya waganga ni mtu na wateja wake.

“Lambalamba ni vijana wasio na kazi maalum ambao wameunda kikundi na kujifanya ni waganga na hivyo kuwapa usumbufu wananchi na kujifanya  wanatoa uchawi”.

Anasema chama kimekuwa kikifanya juhudi mbalimbali kuhakikisha uhuni huo unakoma ikiwemo kupita kata kwa kata na vijiji  kuelimisha wananchi wasikubali kurubuniwa  na kuchukuliwa fedha zao kwa madai kuwa watatolewa uchawi huo ni  utapeli kwani hakuna uchawi unaotolewa

“Vitu wanatega wenyewe na asubuhi wanasema wamekuta nyumba Fulani ina uchawi” anasema

“Chawatiata inasikitika kwa sababu baadhi ya viongozi  wa vijiji na kata walikuwa wakishirikiana na lambalamba kwa kupewa fedha kidogo na kuruhusu wafanye shughuli zao jambo ambalo ni uvunjifu wa amani kwani hakuna mtu mwenye haki ya kuingia eneo la mtu mwingine bila ridhaa yake” alisema

Mratibu wa Ukimwi Mkoa wa Dodoma Audry Njelekela, alisema zipo changamoto za kupambana na VVU na ukatili wa kijinsia katika mikoa ya Dodoma .

Anasema amewahi kusikia tatizo la waganga wa kutoa uchawi kutumia wembe mmoja kunyoa zaidi ya watu watatu lakini kinachotakiwa ni wananchi kuachana na imani za kishirikina ili wawe salama.

Anasema kinachotakiwa ni elimu zaidi ili wananchi waweze kuelimika na kuchana na imani hizo.

Ally Biringi ni chifu wa Wagogo akiwa mkazi wa Makulu Dodoma anasema kazi ya lambalamba haiwezi kukubalika katika eneo lolote.

Anasema waganga hao ni matapeli  ambapo wakati mwingine wamekuwa wakitaja  mtu au watu wanaozuia mvua zamani mambo hayo yalikuwa hayapo kabisa.

“Leo lambalamba na uwezo wa kuingia nyumbani kwa watu anatoa uchawi  kisha anataka hela  hapo wananchi wanaona kama wanasaidiwa kumbe wanatapeliwa” anasema

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *