Serikali imeshauriwa kuharakisha upitishaji na utekelezaji wa mkakati wa kitaifa wa kuzuia unyanyasaji na mauaji ya wazee nchini utakaosaidia kuundwa kwa Baraza la Wazee na kujenga jamii inayoheshimu haki za watu wachache.
Kwa mujibu wa Sensa ya watu na Makazi ya mwaka 2012 idadi ya wazee imefikia milioni 2.5 ambayo ni sawa na asilimia 5.6 ya wananchi wote. Lakini idadi hiyo inaongezeka kila mwaka na kutishia usalama wao ikiwa hatua mathubuti hazitachukuliwa.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Wazee Morogoro (MOREPEO), Samson Msemembo amesema katika kuelekea kilele cha maadhimisho ya haki za binadamu, jamii na serikali inapaswa kuwaangalia wazee na kuwatoa katika hali duni inayowakabili.
Amesema wazee wanakabiliwa na umaskini, unyanyasaji, mauaji na kukosa huduma muhimu za matibabu na usalama ambazo zinawaweka katika hatari ya kutothaminiwa na jamii inayowazunguka.
“Tunapoadhimisha kilele cha siku ya haki za binadamu kimataifa, wazee nchini bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo kuendelea kuwepo kwa unyanyasaji na mauaji ya wazee kwa imani za kishirikina na uwakilishi hafifu wa wazee katika vyombo mbalimbali vya kutoa maamuzi”, amesema mzee Msemembo.
Ameshauri serikali kutunga na kuboresha sera na sheria zitakazo wahakikishia usalama na maslai yao katika jamii.
“Tunapaza sauti setu kuiomba serikali kuharakisha upitishaji na utekelezaji wa mkakati wa kitaifa wa kuzuia unyanyasaji na mauaji ya wazee kwa imani za kishirikina”, amesema mzee Msemembo na kuongeza kuwa, “kukamilisha kutungwa kwa sheria ya wazee ili kuyapa uzito masuala ya wazee na kuanzisha mabaraza ya wazee nchi nzima, ili kujenga mfumo imara wa uwakilishi”.
Kulingana na Shirika la HelpAge International Tanzania linaeleza kuwa asilimia 96 ya wazee hawana uhakika wa kipato na kuwaweka katika hatari ya kuishi katika umaskini na kushambuliwa na magonjwa ya mara kwa mara.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Wazee Morogoro (MOREPEO), Samson Msemembo (katikati) akiwa na Katibu Mkuu Mtendaji wa Mtandao wa Mashirika ya Wazee Tanzania, Wilson Karuwesa (kushoto) na mwananchi kutoka Kibaha, Getrude Msangule, mapema leo jijini Dar es Salaam, wakati wakitoa tamko la kuelekea siku ya Haki za binadamu duniani.
Kwa upande wake, mzee Elisha Mwamkinga kutoka shirika la The Good Samaritan Social Services Tanzania (GSSST) ambaye amekuwa akipigania haki za wazee nchini amesema kila mtu ni mzee mtarajiwa na ameitaka jamii kutengeneza mfumo mzuri wa upatikanaji wa huduma za afya ili kuwaondolea usumbufu wanaoupata katika vituo vya afya.
Amebainisha kuwa wanaendelea kupingania mabadiliko ya kisheria na sera lakini hazitafanikiwa ikiwa afya za wazee hazitaangaliwa na kupewa kipaombele.
“Serikali iendelee kuboresha huduma za afya kwa wazee ikiwemo upatikanaji wa dawa za magonjwa yanayowasumbua wazee”, amesema mzee Mwamkinga.
Naye Getrude Msangule, ambaye ni mwananchi kutoka Kibaha ameitaka serikali kuridhia na kutekeleza mikataba ya kimataifa ya haki za wazee ambayo inawapa nguvu wazee kutambulika na kuthaminiwa katika jamii.
Maazimio ya kimataifa ya Haki za Binadamu
Azimio la Ulimwengu la Haki za Binadamu la mwaka 1948 na Tangazo la Kiulimwengu la Haki za Binadamu (Universal Declaration of Human Rights) ambalo kimsingi ndiyo dira kuu ya utekelezwaji wa masuala ya Haki za binadamu; Maazimio haya yametaja haki za msingi za binadamu kama vile haki ya kutobaguliwa kwa rangi, kabila, umri, jinsia, asili, dini ama hali yoyote ile.
Serikali imeridhia pia Mkataba wa Afrika wa haki za Binadamu na watu (ACHPR) pamoja na Itifaki ya Kusimamia Haki za wazee na mikataba mingine ambayo inazungumzia kulinda na kutetea haki za wazee. Pia Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, ibara ya 12(2) na ibara ya 14 ambazo zinaelezea juu ya wazee kupewa heshima na hifadhi kutoka kwa jamii wanamoishi.
Hali ya Wazee Tanzania
Kulingana na takwimu za shirika la HelpAge Tanzania linaeleza kuwa wazee walio wengi wanaishi katika hali duni na isiyokuwa na uhakika wa kipato. Wazee wanaopata pensheni ni asilimia 4 tu ya wazee wote na familia zinazimilikiwa na wazee, umaskini wake uko juu kwa asilimia 24.4 zaidi ya wastani wa umaskini wa nchi.
Sababu kubwa ya hali hiyo ni kukosa mfumo na mipango madhubuti inayoongoza upatikanaji wa haki za wazee, ikiwemo huduma za msingi za kibinadamu.