Sekta ya elimu kwa muda mrefu imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali za ubora wa elimu inayotolewa kwa wanafunzi ambapo sababu mbalimbali zimekuwa zikihusishwa na kushuka kwa ubora wa elimu nchini.
Sababu kama uhaba wa walimu, miundombinu, vifaa vya kufundishia na kujifunzia, ongezeko la idadi ya wanafunzi shuleni limeongeza mlundikano wa wanafunzi darasani na kuibua changamoto ya uhaba wa madarasa ubora wa elimu inayotolewa.
Sababu nyingine ambayo imeibuliwa hivi karibuni ni elimu kusimamiwa na zaidi ya sekta moja ambapo huleta changamoto katika uwajibikaji wa watendaji wa sekta hiyo katika kutimiza majukumu yao ya kila siku.
Siku za hivi karibuni tumeshuhudia viongozi wa kisiasa kuingilia taaluma ya elimu na kutoa maagizo ambayo yanakinzana na maadili, matakwa ya kazi ya ualimu nchini. Mkanganyiko huo unatajwa kama sababu nyingine ya kushuka kwa ubora wa elimu ikizingatiwa kuwa sekta ya elimu haijasimama yenyewe kuendesha shughuli zake bila kuingiliwa na taasisi nyingine za uongozi.
Licha ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuwa msimamizi mkuu wa sera na sheria za elimu, wizara zingine kama Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto zinawajibika katika utekelezaji wa sera ya elimu nchini.
Mathalani, wizara ya TAMISEMI imepewa jukumu la kusimamia shule za msingi na sekondari ambapo inahusika na uboreshaji wa miundombinu na kuajiri walimu huku utekelezaji sera na mitaala umebaki wizara ya elimu.
Wasomi na wadau wa elimu nchini wameshauri kuwa utaratibu unaotumika wakati huu wa elimu kusimamiwa na zaidi ya wizara moja sio mzuri kwa mstakabali wa elimu nchini ikizingatiwa kuwa umesababisha mgongano mkubwa wa maslahi ya viongozi na walimu.
Hoja hiyo ilibuliwa na Mbunge wa Ulanga, Goodluck Mlinga bungeni Februari mwaka huu wakati akizungumzia kushuka kwa ubora wa elimu ambapo alibainisha kuwa usimamizi wa shule una mkanganyiko mkubwa kwa sababu mwalimu anawajibika kwa zaidi ya bosi mmoja.
“Leo hii mwalimu hana bosi. Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi, Afisa Utumishi, Waziri wote mabosi zake; huyo mfanyakazi ni wa namna gani, hata sisi tungeweza? Sisi tungeweza kila mtu awe bosi wetu, Spika awe bosi wetu, Rais awe bosi wetu, kwahiyo mnawachosha walimu”, alinukuliwa Mlinga akiwa bungeni.
Naye, Prof. Mwesiga Baregu ambaye ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) amesema kinachojitokeza katika elimu ya Tanzania ni mgongano wa maslahi ambayo yanachagizwa na wanasiasa kutumia ujinga na umasikini wa wananchi kama mtaji wa kujipatia nafasi za kisiasa na uongozi wa ngazi mbalimbali katika jami.
“Kilichobadilika katika nchi hii na kuturudisha nyuma kielimu ni kuwa Ujinga na Umasikini vilikuwa maadui lakini sasa Ujinga na Umasikini ni Mitaji ya Kisiasa”, amesema Prof. Baregu.
Mwalimu akifundisha wanafunzi darasani
Wasomi watoa neno
Fikra Pevu ilifanya mahojiano na wasomi wa taasisi za elimu ili kupata maoni yao kuhusu uwajibikaji wa sekta ya elimu kwa zaidi sekta moja na athari zake kwa ukuaji wa elimu nchini.
Mahadhiri wa Shule Kuu ya Elimu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dkt. Lulu Mahai amesema walimu wamefunzwa na wana uwezo wa kufundisha lakini changamoto inayowakabili ni usimamizi usioridhisha wa shughuli zao ambapo huingiliwa na viongozi wengine ambao hawana taaluma ya ualimu.
“Kama sasa hivi mwalimu wa shule ya msingi, sekondari yuko TAMISEMI lakini mtoto akiumwa yuko wizara ya Afya. Je wizara ya elimu inafanya nini katika hilo?”, ameuliza Dkt. Lulu.
Ameibainisha kuwa suluhisho ni kuwa na mgawanyo unaoleweka wa majukumu ya kikazi katika sekta ya elimu ili kuepusha mgongano wa maslahi ambao unawachanganya walimu na wanafunzi katika dhana nzima ya kufundisha na kujifunza.
“Mtoto ni sehemu ya jamii hawezi kukua akiwa kwenye wizara ya elimu peke yake bila wizara ya Afya kuwepo, bila TAMISEMI kuwepo lakini nakubaliana kwamba ni lazima tuwe na wizara ya elimu inayodeal (simamia) masuala ya elimu”, amesema Dkt. Lulu na kuongeza kuwa
“Ni lazima tufike mahali kutambua roles (majukumu) kuwe na descriptions (maelezo) nani anafanya nini saa ngapi, nani anaingia wapi na anaingilia nini lakini Mratibu wa Elimu lazima aitwe wizara ya elimu. Wizara ya elimu lazima ipewe nafasi ya kuifanya elimu ya Tanzania iitwe elimu ya Tanzania kama miaka iliyopita”.
Kwa upande wake, Mhadhiri wa UDSM, Dkt. Luka Mkonongwa amesema elimu ni suala mtambuka linahitaji ushirikiano wa wadau mbalimbali ili kutimiza sera na mipango iliyowekwa.
“Suala la sekta mbalimbali kuweza kushirikiana katika suala la elimu hilo halina ubishi lazima wote tuwe wadau wa elimu kwa nafasi zetu”, amesema Dkt. Mtonongwa.
Hata hivyo, amebainisha kuwa maamuzi muhimu ya kitaalama ikiwemo sera na utendaji wa walimu lazima ubaki mikononi mwa wataalamu wa elimu na sio viongozi wa kisiasa ambao wanataka kujinufaisha kisiasa.
“Kwenye maamuzi ya msingi, mabadiliko ya sera lazima wataalamu wahusike isitokee mtu kwasababu ya nafasi yake ya Uwaziri, Ubunge, Katibu Kata, Udiwani basi ajione yeye ana uwezo kufanya maamuzi kwenye elimu kuliko wataalamu wa elimu wenyewe”,amebainisha Dkt. Mkonongwa na kushauri kuwa,
“Sisi tunaelewa kwamba elimu ndio msingi wa taifa, ili elimu ilete matokeo tarajiwa tunaanza kwanza na mwalimu kumbuka nchi haiwezi kuendelea kuzidi uwezo wa kufikiri wa mwalimu katika nchi hiyo. Tukiwa na utaratibu unaoeleweka tutasonga mbele”.
Akitolea ufafanuzi suala hilo kwa niaba ya serikali, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako amesema ushirikiano wa sekta mbalimbali ni muhimu katika kukuza ubora wa elimu nchini lakini wizara yake itaendelea kutatua changamoto muhimu za utendaji ikiwemo uwajibikaji wa viongozi na walimu katika sekta ya elimu.
“Tunafanya juhudi mbalimbali ikiwemo kuimarisha mitaala ya elimu ili kuwawezesha wanafunzi kupata maaarifa sahihi. Pia tunajitahidi kuboresha utoaji wa elimu bora kwa kuajiri walimu wenye uwezo mzuri wa kufundisha na kuwapeleka kwenye maeneo ambayo hayana walimu wa kutosha”, amesema Prof. Joyce Ndalichako.