Watoto 330,000 waongezeka kila mwaka shule za msingi

Jamii Africa

WAKATI shule tayari zimekwishafunguliwa, inaelezwa kwamba jumla ya madarasa 8,392 yanahitajika kwa mwaka ili kukidhi ongezeko la wanafunzi.

Hali hiyo inatokana na kuwepo kwa ongezeko la wastani wa watoto 333,169 kila mwaka walio na umri wa kuanza darasa la kwanza kuliko idadi ya kawaida, hali inayochangiwa na ongezeko la uzazi nchini Tanzania.

Takwimu zinaonyesha kwamba, uandikishaji wa watoto katika shule za awali na msingi umeongezeka kwa kiasi kikubwa kuanzia mwaka 2005, ambapo idadi inaonyesha wanafunzi walioandikishwa kwa mwaka 2014 walikuwa karibu milioni moja kutoka 638,591 mwaka 2005.

Inaelezwa kwamba, idadi ya wanafunzi walioandikishwa shule za msingi nayo imeongezeka kutoka 7,541,208 mwaka 2005 hadi karibu milioni tisa mwaka 2014.

Kwa mujibu wa Sensa ya Taifa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, watoto waliokuwa na umri wa kati ya miaka 2-6 wako 1,665,843 zaidi ya wale wenye umri kati ya miaka 10-14, hivyo wanapoanza shule katika kipindi cha sasa miaka mitano ijayo watahitaji vyumba vingi zaidi vya madarasa kuliko vilivyopo.

Inaelezwa kwamba, hali hiyo, ikichangiwa na Utekelezaji wa Malengo ya Elimu ya Msingi kama yanavyoainishwa kwenye Malengo Endelevu ya Dunia yaliyopitishwa na wanachama wa Umoja wa Mataifa Septemba 22, 2015, inaipa wakati mgumu zaidi serikali hata katika upangaji wa bajeti za elimu na afya kutokana na ongezeko hilo kubwa la watoto.

Taasisi ya Kutetea masuala ya Idadi ya Watu na Uzazi wa Mpango (TCDAA) inaeleza kwamba, ikiwa wastani halisi wa chumba cha darasa ni watoto 40, basi ongezeko la watoto 333,169 pekee linahitaji vyumba 8,392 kwa mwaka, ambavyo hata hivyo, haviwezi kupunguza idadi ya watoto ambao wanakosa elimu ya msingi na wengine hawana madarasa kwa sasa.

Dk. Joel Silas Lincoln kutoka Idara ya Uchumi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam anasema Tanzania ya leo ina idadi ya watu wenye umri mdogo kuliko miaka ya nyuma. Asilimia 54 ya Watanzania wana umri wa chini ya miaka 20.

“Muundo wa idadi ya watu nchini unamaanisha kwamba nchi inaweza kunufaika na faida itokanayo na ongezeko la idadi ya watu kama ilivyokuwa kwa nchi za kusini-mashariki mwa bara la Asia.

“Tangu miaka ya 1970, asilimia 25-33 ya ukuaji wa uchumi katika nchi hizo imekuwa ikihusishwa na muundo wa idadi ya watu, kutokana na kuwa na idadi kubwa ya watu wanaofanya kazi kuliko wategemezi – badiliko ambalo lilisababishwa na upatikanaji wa huduma ya uzazi wa mpango,” anabainisha Dk. Joel.

Katika taifa ambalo uwezo wa mwanamke kuzaa ni watoto watano huku wanaotumia njia za uzazi wa mpango wakiwa asilimia 27 tu, hali hiyo ni changamoto kubwa kwa serikali na jamii kwa ujumla.

 

Tatizo likoje?

Ongezeko la watoto wengi kwa sasa linatokana na sababu nyingi, kubwa ikiwa kutokuwepo kwa elimu ya kutosha na matumizi sahihi ya uzazi wa mpango pamoja na mimba za utotoni.

Mimba za utotoni zinachangiwa na sababu mbalimbali zikiwemo umaskini na mila na desturi ambazo zimeshuhudia watoto wengi wa kike wakiozeshwa wangali wadogo.

Aidha, taarifa zinasema kwamba, watoto wa kike walio wengi wanapata ujauzito wakiwa na umri wa kati ya miaka 15 na 19, umri ambao wengi wao wanakuwa bado shuleni, hivyo kukatisha masomo kutokana na mimba hizo zisizotarajiwa.

Idadi ya wanafunzi wa kike wanaopata ujauzito bado ni kubwa nchini Tanzania ingawa takwimu zinaonyesha kwamba inapungua kwa kiasi fulani, hali ambayo inachangia kuwepo kwa ongezeko la watoto ambao wanakuwa tegemezi kwa kaya, familia na taifa kwa ujumla.

Shirika laUmoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) linaeleza kwamba, Utafiti wa Idadi ya watu na Afya Tanzania 2010, uligundua baadhi ya mabadiliko muhimu ambapo kiwango cha kupata ujauzito kwa wasichana wa umri wa miaka 15-19 kilishuka kwa asilimia 12 kati ya mwaka 2004 na 2010.

Hata hivyo, UNICEF inasema kwamba, karibu msichana mmoja kati ya wasichana 20 nchini Tanzania huanza kuzaa akiwa na umri wa miaka 15, na uwiano huo huongezeka kwa kasi hadi msichana mmoja katika wasichana wanne miongoni mwa wasichana wa umri wa miaka 17 na zaidi ya msichana mmoja katika wasichana watatu miongoni mwa wasichana wa umri wa miaka 18.

“Wasichana wa vijijini wana uwezekano wa karibu mara mbili ya wale wa mijini wa kupata watoto kabla hawajafikia umri wa miaka 19. Zaidi ya nusu ya wasichana ambao hawakupata elimu hupata watoto au mimba kabla ya kufikisha umri wa miaka 19, ikilinganishwa na kama asilimia 25 kwa wasichana waliomaliza elimu ya msingi na chini ya asilimia tano kwa wasichana waliohitimu elimu ya sekondari,” imeeleza UNICEF.

Imebainishwa kuwa wanafunzi wanaoongoza kupata ujauzito katika sehemu mbalimbali nchini ni wa shule za msingi ambao hawana uelewa wowote wa elimu ya uzazi wa mpango wala elimu ya mahusiano, hivyo wanapojiingiza kwenye uhusiano bila kutambua wengi hujikuta wakiambulia mimba ambazo mara nyingi huwa hazina mlezi.

Vile vile, katika matukio mengine, baadhi ya wazazi na walezi hushirikiana na watoto wao walio chini ya umri wa miaka 18 kutoa mimba hata kwa kutumia njia za kienyeji ambapo licha ya kutokuwepo takwimu za madhara ya waliofanya hivyo lakini wanafunzi wanaotoa mimba ili kuendelea na masomo inaongezeka kila siku.

Kukosekana kwa elimu ya uzazi wa mpango kuanzia ngazi za chini ndiyo chanzo kikubwa cha watoto kujiingiza katika uhusiano wa kimapenzi mapema, kama UNICEF inavyoeleza.

“Asilimia tisa ya wanawake na asilimia 10 ya wanaume wa umri wa miaka 15-24 walieleza kuwa walianza kujamiiana kwa mara ya kwanza wakiwa na umri wa chini ya miaka 15. Asilimia hamsini ya wanawake na asilimia 43 ya wanaume wa umri wa miaka 18-24 walieleza kwamba walianza ngono kabla ya umri wa miaka 18.”

Watoto wachanga waliozaliwa na mama wa umri mdogo wanakabiliwa na hatari kubwa zaidi ya kupoteza maisha kuliko wale waliozaliwa na mama wa umri mkubwa. Miongoni mwa kila vichanga 1,000 vinavyozaliwa na mama wa umri wa chini ya miaka 20, vichanga 41 hupoteza maisha ndani ya mwezi mmoja baada ya kuzaliwa.

Hata hivyo, mama anapokuwa na umri wa miaka 20 hadi 29, idadi ya vifo vya vichanga hupungua hadi kufikia vifo 22 kwa kila vichanga 1,000 vilivyozaliwa hai.

Mama wenye umri mdogo wanaelezwa pia kwamba huhatarisha afya zao wenyewe.

Duniani kote, mimba ni chanzo kikubwa cha vifo vya wanawake vijana wa umri wa miaka 15 hadi 19, zikisababisha takribani vifo 70,000 kila mwaka.

 

Zamani ilikuwaje?

Bi. Mwajuma Kassim (62), mkazi wa Tandika jijini Dar es Salaam, anasema kwamba, maadili yamepungua katika jamii kwa sasa ambapo vijana wengi wamekuwa wakianza masuala ya ngono wakiwa wadogo.

Hali hiyo, anasema, inachangiwa na mabadiliko ya sayansi na teknolojia, ambapo hata kama mzazi atakuwa na msimamo wa kumwelekeza mwanawe misingi mizuri, bado mtoto huyo atajifunza mambo hayo kwenye video ama makundi rika.

“Zipo mila za zamani ambazo zilikuwa zinasaidia sana kujenga maadili kwa watoto kuliko hivi sasa, kulikuwa na adhabu zilizokuwa zikitolewa kwa wasichana wanaokuwa na mimba,” anasema Bi. Mwajuma.

Aidha, anaongeza kwamba, zamani hata suala la mtoto kumchungulia mtu mzima akioga ama kujisaidia lilikuwa ni kosa kubwa, achilia mbali mtoto kuzungumzia suala la ngono hadharani.

“Tuliambiwa kwamba ukimchungulia mtu mzima utapofuka macho, hii maana yake ililenga kuhimiza maadili, lakini leo hii ambapo kuna mitandao ya kijamii wanayoweza kuitazama hata kwa kutumia simu za mkononi, watoto wanajifunza mambo mengi ambayo hata wazazi wao hawayajui,” anasema.

 

Nini kifanyike?

Serikali kwa kushirikiana na asasi zisizo za kiserikali inapaswa kuhakikisha kuwa elimu inatolewa kwa watoa huduma wa ya afya ya uzazi ikiwemo uzazi wa mpango na pia jamii ielimishwe zaidi kuhusu faida na umuhimu wa kupanga uzazi.

Bajeti ya Wizara ya Afya inapaswa kutoa kipaumbele kwa elimu na huduma za uzazi wa mpango ili wananchi wote, hasa wa vijijini, waweze kupata huduma hizo kwa wakati na kwa usahihi.

Kwa mfano, katika mwaka wa fedha 2011/12 Serikali ya Tanzania ilitenga shilingi bilioni 1.2 kwa ajili ya dawa za uzazi wa mpango, lakini hadi kufikia Juni 2012 haikuwa imetoa chochote.

Kwa mujibu wa Shirika la Maendeleo ya Watu Tanzania (HDT), katika kipindi cha 2010/11, fedha zilizotakiwa ili kufikia malengo ya asilimia 60 ya matumizi ya dawa za uzazi wa mpango ifikikapo 2015 zilikuwa shilingi billioni 19, lakini Serikali ilipanga kutoa shilingi billion 3, sawa ma asilimia 16 tu ya mahitaji.

Mikakati kadhaa imewekwa kufikia malengo hayo ambayo ni pamoja na kuongeza matumizi ya njia za kisasa za uzazi wa mpango ili yafikie asilimia 60, ambapo kwa sasa ni asilimia 27 tu ya wanawake walioolewa ndio wanaotumia njia hizo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *