Wavamizi watishia kuliangamiza Bonde la Wami Ruvu

Jamii Africa

Sera ya maji ya mwaka 2002 inabainisha kuwa Matatizo mengine katika kusimamia na kuendeleza rasilimali za maji hapa nchini yapo katika maeneo ya utunzaji wa rasilimali za maji katika Mabonde ya kimataifa, masuala ya sheria na mfumo wa kitaasisi wa kusimamia kikamilifu rasilimali za maji nchini.

 Tanzania ina mabonde 9 ya maji ambayo hujumuisha ziwa Tanganyika, Nyasa, Victoria, Rukwa pamoja na mito mbalimbali ambayo ni vyanzo vikuu vya maji yanayotumika kwa shughuli za kibinadamu ikiwemo umwagiliaji na mifugo.

Shughuli za binadamu zisizozingatia sheria ikiwemo kulima na kuchimba mchanga kando ya mito zimekuwa zikihatarisha uhai wa mabonde hayo.

 Mathalani  Bonde la Wami Ruvu linatishiwa na uharibifu wa kingo za mto Wami kutokana na baadhi ya watu kuvamia maeneo hayo na kuanzisha kilimo cha umwagiliaji bila kuzingatia taratibu. 

Omary Ramadhan, mkazi wa Pongwe Kiona kijiji kilicho karibu na mto Wami anasema wamepata taarifa kuwa kuna watu wanalima kando kando ya mto bila kibali cha uongozi wa kijiji.

“Mwenyekiti na wajumbe walienda katika maeneo hayo na kukuta vijana wanalima kando ya mto, wamekatazwa kuendelea na shughuli zao kwasababu ni kosa”, amesema Omary.

Omary ambaye ni mkulima anakiri kuwa mto huo ni chanzo kikubwa cha maji katika Wilaya ya Bagamoyo lakini unakabiliwa na uharibifu wa mazingira ikiwemo wafugaji wa kimasai kuchunga mifugo yao kwenye chanzo hicho.

Kulingana na Takwimu za Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Bonde la Wami Ruvu linajumuisha mito mikuu miwili ambayo ni Wami wenye kilometa za mraba 400,000 na Ruvu kilometa za mraba 17,700. Pamoja na mito ya ukanda wa Pwani iliyopo Kusini mwa Dar es salaam. 

Bonde hili kwa ujumla lina ukubwa kilometa za mraba 72,930 pia lina maeneo ya tambarare na safu ndefu za milima. Linazungukwa na aina nne za milima; Milima ya Uluguru iliyopo Kusini Mashariki, Milima ya Nguru na Rubeho iliyopo Magharibi ya Kilosa, Milima ya Ukaguru iliyopo Kaskazini mwa Wami.

Sheria ya Mazingira hairuhusu shughuli zozote za kibinadamu jirani na vyanzo vya maji ndani ya mita 60 kuanzia chanzo cha maji kilipo ikiwemo mito na mtu akikaidi atafungwa ama atalipa faini isiyopungua Sh. milioni 10.

Bonde la Wami Ruvu ni chanzo kikubwa cha uzalishaji wa maji katika mitambo ya Ruvu Chini na Ruvu Juu ambayo inahudumia mikoa ya Dar es Salaam na Pwani. 

Licha ya kuzalisha maji ya uhakika lakini hayatoshelezi mahitaji ya wakazi wa mikoa hiyo kwasababu ya mabadiliko ya tabia nchi na kuongezeka kwa shughuli za binadamu.


Mkakati wa serikali

Wizara ya Maji na Umwagiliaji kupitia Bonde la Wami Ruvu inakusudia kutangaza  eneo hilo kuwa hifadhi ya vyanzo vikuu vya maji nchini ili kulinda na kutunza mazingira na kutoa huduma ya uhakika ya maji kwa wananchi.

Ofisa kutoka Bonde hilo, Grace Chitanda wakati akiongea na Wanahabari waliotembelea bonde hilo amesema wameaanza mipango ya uhifadhi huo katika eneo la Makotopola  mkoani Dodoma na wanatarajia kuendelea katika maeneo mengine.

Amesema uhifadhi huo wa vyanzo vya maji  utasaidia kurejesha hali ya uoto wa asili katika vyanzo hivyo na hivyo kuwa kivutio.

Aidha amesema kwa mkoa wa Morogoro wanatarajia kutangaza kuwa hifadhi katika Bwawa la Mindu na maeneo mengine oevu yenye vyanzo vikuu vya maji.

Amebainisha kuwa shughuli za kibinadamu zinazofanywa kwenye vyanzo vya maji mara nyingi zimekuwa zikichangia kwa kiasi kikubwa kuharibu na hatimaye hata kukausha vyanzo vya maji na hivyo uhifadhi huo utasaidia kuleta maana.

Pia wanaendelea kuwachukulia hatua za kisheria watu wanaovamia katika vyanzo hivyo na kuendesha shughuli za kilimo.

Kauli ya Katibu Mkuu

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Prof. Kitila Mkumbo, wakati akiongea katika kipindi cha runinga cha ‘Njoo Tuongee’ amesema serikali inaendelea kutekeleza Sera na sheria za maji ambapo wanato elimu kwa wananchi kuhifadhi vyanzo vya maji ili viwe na matumizi endelevu.

Hata hivyo, amesema wanashirikiana na sekta binafsi kubuni miradi ya maji itakayokidhi mahitaji ya wananchi wrote wa Tanzania.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *