Waziri afichua wizi mkubwa TRL, Marine Service

Jamii Africa

NAIBU Waziri wa Uchukuzi, Dk. Charles Tizeba (pichani), amefichua madudu mengi yanayofanywa na kampuni ya huduma za Meli (Marine Service), pamoja na Shirika la Reli nchini (TRL), ambapo amesema mashirika hayo yamekubuhu kwa wizi wa mafuta ya kuendeshea Meli na Treni.

Amesema, wizi huo mkubwa umekuwa ukifanywa na baadhi ya watumishi kwa kushirikiana na baadhi ya vigogo wa mashirika hayo wasiokuwa waaminifu, na kwamba hujuma hizo ndiyo chanzo kikuu cha mashirika hayo kufa na kushindwa kujiendesha kwa ushindani wa kibiashara baina yake na sekta binafsi.

Kufuatia tuhuma hizo za wizi wa mafuta ya Meli na Treni, Waziri Dk. Tizeba ameuagiza uongozi wa shirika la Marine Cervise kupitia kwa Kaimu Meneja wake, Projest Samson Kanja kumfukuza kazi mara moja Kepteni mmoja ambaye aliwahi kukamatwa na lita 2,000 za mafuta ya wizi katika Meli ya Mv. Victoria, inayofanya safari zake kutoka jijini Mwanza kwenda Bukoba mkoani Kagera.

Akizungumza jana kwa jazba, katika kikao cha pamoja na viongozi wa Marine Cervise ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku moja kutembelea na kukagua shughuli za mashirika hayo, Waziri Dk. Tizeba alisema, kamwe Serikali haiwezi kuvumilia hujuma za namna hiyo, kwani zimelenga kuichonganisha Serikali na wananchi wake.

Alisema, anazo taarifa sahihi kuhusu wizi huo wa mafuta ya meli na treni, na kwamba wizi huo umekuwa ukifanywa kwa siri na wahusika punde wanapokuwa safarini na vyombo vyao, hivyo kuagiza Kepteni mmoja (hakutajwa jina), aliyekamatwa na mafuta hayo ya wizi katika Mv. Victoria, afukuzwe kazi kuanzia sasa.

“Hapa Marine Cervise upo wizi mkubwa sana wa mafuta ya meli, na ushahidi upo!. Serikali inatoa fedha nyingi za kuendesha chombo hiki, lakini mnakihujumu bila huruma. Yaani mnamhujumu hadi marehemu?.

“Nataka kujua, na uniambie wewe Meneja wa Marine Cervise huyo Kepteni wa Mv. Victoria aliyekamatwa na lita 2,000 za mafuta ya meli bado yupo hapa?. Nakuuliza huyu mtu bado unaye?. Naagiza afukuzwe kazi mara moja. Aondoke akatafute kazi kwingine…umenisikia wewe Meneja?.”, alisema kwa kufoka Naibu Waziri huyo wa Uchukuzi, Dk. Tizeba.

Aidha, Waziri huyo aliyeambatana na Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana jijini Mwanza, Baraka Konisaga (DC), alilazimisha kupelekwa ndani ya meli ya Mv. Victoria iliyokuwa imepaki kwenye Gati lake, na kwamba alijionea madudu mengine makubwa ya viti vya meli hiyo kutokuwa katika standadi inayotakiwa.

Akiwa melini humo, Dk. Tizeba alijionea viti vya daraja la tatu vikiwa vimechomelewa kwa mbao na vyuma jambo lililoonekana kumkasirisha upya, ambapo alihoji sababu ya kampuni hiyo kushindwa kutengeneza viti vizuri kwa ajili ya wateja wao wanaosafiri umbali mrefu usiku kucha kutoka jijini Mwanza hadi mjini Bukoba mkoani Kagera.

“Hivi ninyi Marine Cervise unaona hivi ndiyo viti vya wateja wenu?. Yaani ni vyuma na mbao?. Mtu atapendaje huduma yenu mbovu kiasi hiki?. Nataka ndani ya wiki mbili meli yote iwe na viti vizuri na mazingira yanayomfurahisha mteja”, alisema.

Kuhusu Reli, Waziri Dk. Tizeba ambaye alikutana na wafanyakazi wa shirika hilo katika ofisi za makao makuu jijini hapa, licha ya kupokea malalamiko mengi kutoka kwa wafanyakazi hao, aliwarushia kombora zito la kuwatakawaache wizi wa mafuta ya treni.

“Kule Marine kuna wizi mkubwa wa mafuta ya meli. Na hapa Reli wizi wa namna huu upo tena mkubwa sana. Mnaiba mafuta mnapofika Imalampaka au Shinyanga.

“Taarifa hizi sahihi ninazo kutoka kwa baadhi ya wenzenu mnaoiba nao…sasa nataka hujuma hizi zife. Mimi na Bosi wangu Mwakyembe (Waziri wa Uchukuzi Dk. Harrison), tumekubaliana kulifufua upya shirika hili ili lisaidie wananchi wetu”, alisema.

Aidha, Waziri Tizeba aliuagiza uongozi wa shirika hilo kuhakikisha unaanza kupeleka treni ya abiria jijini Mwanza hadi Dar es Salaam kabla ya Septemba mwaka huu, na kwamba mikakati hiyo ifanywe na uongozi kwa kushirikiana na wafanyakazi wa shirika hilo, na si kutegemewa Serikali.

Alisema, mwaka huu Wizara yake hiyo ya Uchukuzi ilishatenga kwa shirika hilo la TRL nchini zaidi ya sh. bilioni 18.9 kwa ajili ya kulifufua, hivyo vichwa 18 vya treni vitakodishwa kutoka nchi ya Afrika Kusini, vichwa 13 vitanunuliwa vipya na 15 vitafufuliwa kwa ajili ya kufanyakazi zake katika kuhudumia Watanzania.

Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk. Charles Tizeba, akizungumza na wafanyakazi wa Reli nchini (Trau), mkoani Mwanza

3 Comments
  • Neno ufisadi halifurahishi kusikika katika masikio ya watanzania lakini sasa kila ukifungua habari unakutana na wizi wa mamilioni au mkataba usiokuwa sahihi kweli haipendezi

    Ni hivi majuzi tutumesikia habari mbaya ya utoaji wa liseni kwa wawindaji na hatimaye liseni hizo zinatumika kuwekeana mikataba ya mabilion ya uchimbaji wa madini ya urani huko Songea

    Mwandishi wa tukio hilo alieleza kuwa taratibu ziko wazi kwa wale wanaopewa liseni za uwindaji kuwa hazihusiani na madini yaliyopo aridhini wala mafuta

    Lakini mamlaka zinazohusika zimeliona hilo lakini sijui macho yao hayaoni au ni huo ufisadi.

    Juzi mheshimiwa aliyekuwa naibu katika ujenzi na sasa waziri katika wizara ya uchukuzi na kusimamia ipasavyo kamati aliyopewa kuhusu neno hilo ufisadi aliacha usingizi wake na kuamkia kituo cha usafiri pale Ubungo nafikiri kwa macho yake alijionea jinsi sheria na nauli iliyowekwa isivyofuatwa na baadhi ya watu wenye vyombo vya usafiri na hatimaye tunaambiwa wengine wamatozwa faini za hapo kwa hapo.

    Sasa wiki haijaisha tunasikia wizi mwingine wa mamilioni ya fedha kutokana na mafuta ya meli na treni na naibu waziri wa uchukuzi ameagiza wengine wafukuzwe kazi

    Kwa maoni yangu sioni kama haya ya kumfukuza kazi yanatosha . Kwanza serikali kupitia mkaguzi mkuu, Idara hii ya Ukaguzi inatakiwa sasa ipewe meno na hasa meno ya kutosha.

    Mheshimiwa Otouh antakiwa aandaye taarifa ya upotevu wa fedha hizo na hao watu wafikishwe mahakani hiyo iwe ndiyo kazi yake kusimama kama shahidi wa serikali

    Wakaguzi wa ndani wa wizara na idara pia wanatakiwa kusimamia ipasavyo malipo na sheria za ulipaji na ukusanyaji wa mapato ya idara ya wizara na taasisi zote za umma.

    Hakuna mkaguzi atakayeshindwa kusoma log book inayoonyesha mafuta yaliyoletwa toka ulaya , bohari kuu , yaliyoingia wizarani kwenye magari na mitambo , na matumizi yake

    Hizi ni hesabu za awali za utunzanzaji wa vitabu /bookeeping sasa mpaka mamilioni yanaibwa hao wakaguzi ni kama hawafanyi kazi yao ipasavyo au wanazibwa na uongozi wasifanye.

    Kwa hali hii hatutafika popote kila siku tutaendelea kusikia wizi wa mamilioni kama hatua za mfano kwa wanaohusika wawe ni mawaziri, wabunge makatibu , wakurugenzi wahasibu , nk hawatachukuliwa hatua tena ikiwa ni pamoja na kutaifisha mali zaozilizotokana na wizi huo

    Naomba tukumbuke enzi za waziri mkuu Sokoine na ile hali ya uhujumu uchumi jinsi watanzania walivyotupa vitu ambavyo vilitokana na fedha haramu. Leo hii mtu mabilioni bila kuwa na woga wa kuulizwa ameyapata na kama sii kuhujumu uchumi wa nchi au kwa neno la sasa Ufisadi

    Naomba mheshimiwa Rais Kikwete usaidie kurudisah ile hali na kama sheria ya uhujumu uchumi imefutika Tanzania basi hali iliyopo sasa inahitaji sheria hiyo irudishwe ili kudhibiti wimbi la wizi wa mamilioni unaoota kama uyoga kila kukicha

    Mungu ibariki Tanzania

  • Mkuu umezungumzia suala la mafuta bado la mataaluma ya reli(vyuma vya reli) vimekua vikiuzwa kwa wingi toka Kigoma, Singida ktk viwanda vya chuma chakavu hapa hapa Dar. na hapo tupia jicho mkuu.

  • Muda umefika Amiri Jeshi Mkuu kusimama kwa miguu miwili bila kulegeza mwendo. Umoja wetu unaiahitaji kulindwa na wanachi waulizwe juu ya wizi wa namna hii! Haiwezekani maana ipo siku utaulizwa haya yote yanayotokea uliyasimamia.

    Njia umeishaionyesha kwa uzalendo wa hali ya juu, upole wako na moyo wako mwema hakika elimu umeitoa ya kutosha.

    Basi, na asiyesikia la Mkuu lake guu uvunjika. Nashauri hawa wote wanaogundulika kwa makusudi kukwamisha juhudi zako wafutwe kazi na wapelekwe mahakamani na wafilisiwe tupo nyuma yako.

    Lakini kubwa zaidi kwa leo upendo wetu, umoja wetu ndio uliotufanya tufikie hapa na kuheshimika duniani. Haipo hata siku moja umfurahishe kila mtu. Ninachosema ni hiki hapa”kama tulinda vita ya kagera na makaburu kwa umoja wetu uleule kwa mshikamano wa wakulima na wafanyakazi basi taifa linangoja tamko lako tu la kununua meli kubwa kwa ajili ya safari za majini toka bara kwenda visiwani na ili linawezekana ni uamuzi na taarifa Watanzania wako nyuma yako tunasubiri”. Mwendo na mbinu zetu ni zilezile zilizomnyoa kaburu na nduli iddi amini.

    Meli ikipatikana utafutwe utaratibu wa kuiendesha na kuisimamia katika mtindo wa biashara au kwa jinsi taifa litakavyoona inafaa.
    Kitendo cha kuachia kila kitu mikononi mwa wa janja ndo kunaumiza nchi sasa ni lazima taifa liwe na mambo ya kujivunia na ya kupigia mfano. Na ikimbukwe kuwa kila kitu kinhitaji usimamizi na uongozi bora tu(Good leadership and governance) pamoja na misingi imara ya uwepo wake.

    Mungu ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *