Wimbi la watoto kutoweka Bukoba latisha wananchi; Mwingine atoweka

Jamii Africa

MATUKIO ya kupotea kwa watoto yameibuka tena katika wilaya ya Bukoba mkoani Kagera,baada ya mwanafunzi wa darasa la tatu Renatha Felician(10) shule ya msingi Mwenge kupotea katika mazingira ya kutatanisha.

Mwanafunzi huyo amepotea mwezi mmoja uliopita na kwa mujibu wa mlezi wake Leokadia Thomas juhudi za kumpata zimeshindikana ambapo alipotea wakati amekwenda mtoni kuchota maji.

Mlezi huyo amefungua faili namba BU/RB/5940 katika kituo cha polisi Bukoba,huku wilaya hiyo ikigubikwa na matukio mengi ya kupotea kwa watoto yanayohusishwa na imani za ushirikina.

Kwa mujibu wa maelezo ya mlezi huyo mkazi wa kijiji cha Kyaitoke kata ya Butulage ambaye ni bibi yake mwanafunzi huyo alipotea Octoba 8, na kudai baadhi ya watoto wa vijiji jirani wamepotea kwa njia ya kuwarubuni kwa kuwapa lifti kwenye magari.

“Ni mfupi mweupe tumeulizia hata kwa ndugu hakuna aliyemwona wanaiba watoto wa kike kwa kuwapa lifti kwenye magari na wengi wamepotea kwa njia hiyo”alisema Leokadia.

Pia miezi michache iliyopita mwanafunzi wa darasa la tatu shule ya msingi Kabalenzi Twinayesu Emmanuel alipotea katika mazingira ya kutatanisha na baadaye kugundulika ameuwawa huku baadhi ya viungo vya mwili wake vikiwa vimenyofolewa.

Katika tukio hilo mtuhumiwa mmoja aliyedaiwa kujihusisha na mtandao wa mauaji ya watoto na unyofoaji wa viungo alikamatwa na matukio ya aina hiyo yameendelea kujenga hofu kubwa miongoni mwa wazazi na watoto.

Matukio mengine yanayohusishwa na imani za ushirikina katika wilaya hiyo ni lile la kupotea kwa Anard Ezekiel(3)katika kijiji cha Karonge katika mazingira ya kutatanisha ambapo baada ya miezi kadhaa mtoto huyo hakuwahi kupatikana.

 

Na Phineas Bashaya

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *