Zahanati yafungwa baada ya Muuguzi wake kwenda likizo!

Jamii Africa

WAKATI baadhi ya hospitali zikiathiriwa na mgomo wa madaktari, mkoani Mwanza kumetokea kituko baada ya zahanati kusitisha huduma na kufungwa kwa kuwa tu muuguzi wake ameanza likizo.

Zahanati ya Kata ya Ngula Wilayani Kwimba mkoani Mwanza, ndiyo ambayo imefungwa na huduma kusimamishwa kutokana na kuwa na muuguzi mmoja tu ambaye amelazimika kuanza likizo yake ya mwaka na zahanati kufungwa.

Zahanati hiyo ambayo muuguzi wake ametajwa kwa jina moja la Magdalena, inahudumia vijiji vinne vya Nyamatale, Ngula, Ng’hulya pamoja na kijiji cha Ngogo, na kwamba zaidi ya watu 25,000 wanategemea kupata huduma katika zahanati hiyo ambayo kwa sasa imefungwa.

Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi, umegundua kwamba, zahanati hiyo imefungwa tangu Januari 26 mwaka huu, na kwamba hadi sasa Serikali kupitia Idara yake ya afya wilayani humo, haijapeleka muuguzi mwingine kwa ajili ya kwenda kutoa huduma kwa wananchi wanaohitaji kupata huduma za kitabibu.

Kwa mujibu wa uchunguzi huo, kwa sasa wananchi waliokuwa wakitegemea huduma katika zahanati hiyo wamekuwa wakilazimika kutembea umbali unaokadiriwa kuwa zaidi ya kilometa 30 hadi 50 kwenda kupata huduma katika maeneo mengine, huku baadhi yao wakishindwa kumudu safari hiyo ndefu, hivyo hujikuta wakiathirika.

Taarifa zisizo rasmi zinadai kwamba, wapo baadhi ya watu wamepoteza maisha yao kutokana na kukosa huduma kwa ukaribu, huku wengine wakilazimika kusafirishwa hadi hospitali ya wilaya iliyopo na umbali mrefu kutoka maeneo husika.

“Tulisikia kuna watu kama wawili hivi wamekufa baada ya kukuta kituo hakifanyi kazi kimefungwa. Tulisikia tu ila hatujui kama ni kweli maana ukweli watu wengi tunahangaika sana kutafuta huduma”, alisema mwana mama mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Mama Samwel.

Diwani wa Kata hiyo ya Ngula, Palu Mashagu (CUF), pamoja na Mkuu wa wilaya hiyo, Christopher Ryoba Kangoye (DC), wamethibitisha kufungwa kwa zahanati hiyo, ambapo Diwani Mashagu alisema: “Hili ni tatizo kubwa sana. Haiwezekani kituo kifungwe kutoa huduma kwa sababu ya Muuguzi wake kaenda likizo. Hivi tupo na Serikali ya aina gani hii?.”

Alisema, hiyo ni mara ya pili kufungwa kwa zahanati hiyo baada ya Muuguzi wake kwenda likizo nyumbani kwao, na kwamba hali kama hiyo ilijitokeza Machi mwaka jana 2011, ambapo wananchi hao waliathirika kwa kukosa huduma za matibabu baada ya huduma hiyo kufungwa hadi Aprili mwaka huo.

“Mwaka jana napo zahanati hii ilifungwa kwa tatizo hili hili la mtaalam kwenda likizo…ilikuja kufunguliwa mwezi wa nne. Nasema kwa niaba ya wananchi wangu wa kata ya Ngula hatutavumilia hali hii mbaya.

“Kwa nini Serikali isilete wauguzi wengine wengi?. Inakuwaje kituo kama hiki kinahudumia maelfu ya watu kiwe na mtaalamu mmoja tu?. Tunataka Serikali ilete haraka Muuguzi ili watu wangu wapate huduma”, alisema Diwani huyo wa Kata ya Ngula, Mashagu (CUF).

Kwa upande wake, Mkuu wa wilaya hiyo, Kangoye alikiri kufungwa kwa zahanati hiyo kwa sababu ya Muuguzi wake kwenda likizo, na kusisitiza kwamba kamwe Serikali haiwezi kumzuia mtumishi kwenda kupumuzika (likizo), kwani hiyo ni haki ya kila mtumishi.
“Ni kweli kuna taarifa kama hizo za kufungwa kwa zahanati hii. Lakini tatizo lililopo ni uhaba wa wataalamu katika wilaya yetu hii ya Kwimba!. Huwezi ukamzuia mtu asiende kupumuzika…na tunashindwa kupeleka wengine hapo maana gharama ni kubwa za kumhamisha.
Mkuu wa Wilaya ya Kwimba, Christopher Ryoba Kangoye (kulia), akiwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Zephania Wanga Masangu katika moja ya vikao vya Kiserikali
“Halafu hata kama tukimhamisha kwa mfano kutoka kule Mwamashimba kwenda Ngula, atamwacha nani hule Mwamashimba?. Na yeye akipata rikizo itakuwaje?. Mimi naona Serikali iajiri watumishi wengi zaidi wa sekta hii na zile nyingine ili kuondoa adha kama hizi kwa wananchi wetu”, alisema Mkuu huyo wa wilaya ya Kwimba.

Hata hivyo, Mganga Mkuu wa wilaya hiyo (DMO), aliyefahamika kwa jina moja la Dk. Bisulu alipoulizwa leo kwa simu alitofautiana na kauli ya Mkuu wa wilaya hiyo pamoja na diwani wa Kata ya Ngula kwa kusema: “Mimi nipo safarini, lakini mbona alishapelekwa Muuguzi mwingine?. Ngoja niulizie maana si kwamba bado imefungwa, nimeambiwa yupo mtu kapelekwa huko Ngula”.

Habari hii imeandikwa na Sitta Tumma – Mwanza

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *