Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe amesema chama chake kitaendelea kuikosoa serikali pale inapokosea na kutetea maslahi ya taifa.
Akizungumza leo na vyombo vya habari katika Makao Makuu ya chama hicho jijini Dar es salaam, Zitto amesema chama chake hakitakuwa jukwaa la kuisifia serikali na chama tawala na kama kuna wanachama hawakubaliani na msimamo wa chama waondoke.
“Wanaodhani kuwa chama hiki kitakuwa jukwaa la kusifia chama tawala na serikali hili sio jukwaa sahihi kwao. Wajitathmini kama wataendelea na uanachama au wajivue kama wenzao walivyofanya”
“Ni wajibu wetu kama chama cha upinzani kutanguliza maslahi mapana ya taifa na kuikosoa serikali pale inapokosea”, amesema Zitto
Kauli ya Zitto inakuja siku chache baada ya aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Samson Mwigamba na wenzake kukihama chama hicho na kukimbilia Chama Cha Mapinduzi (CCM). Mwigamba alidai kuwa viongozi wa chama hicho wanakiuka misingi waliyojiwekea na kuwa anaenda CCM kwasababu ameridhishwa na utendaji wa Rais John Magufuli.
Hata hivyo Zitto amepinga madai hayo na kusema chama chake kiko imara na kitaendelea kusimamia misingi ya uzalendo, kudai usawa wa kiuchumi kwa raia wote, kupinga ubaguzi kwa misingi ya rangi, dini na walioondoka wameshindwa kukubaliana na misimamo ya ACT Wazalendo.
“Baadhi ya wanachama wetu wameondoka na kujiunga na vyama vingine na miongoni mwa masuala yalioelezwa ni pamoja na chama chetu kutofuata misingi ya chama chetu tuliyokubaliana. Wale wanaoona utawala wa sasa ni mzuri wakaamua kujiunga nao wasiwakwaze wanachama wanaoona utawala wa sasa haufai kwani unaua uchumi na kuminya haki za watu”, amesema Zitto.
Zitto ameeleza kuwa wataendelea kushirikiana na wanachama walioondoka kwasababu wana mchango katika kukiimarisha chama hicho hata kama wana mawazo tofauti na wanachama waliopo katika chama.
Kwa upande wake, Kaimu Mwenyekiti wa chama hicho, Maganja Jeremia aliyechukua nafasi ya Anna Mghwira amesema uongozi wa chama upo na kilichotokea ni mapito tu katika siasa na wataendelea kusonga mbele kutetea misingi ya chama na taifa.
Akizungumzia makubaliano ya serikali na Kampuni ya Barrick kuipa Tanzania fidia ya bilioni 700 na kugawana faida 50 kwa 50 licha ya serikali kumiliki hisa za asilimia 16, amesema suala hilo haliwezekani na serikali inapaswa kuwaambia ukweli wananchi juu ya mchakato mzima wa upatikanaji wa mapato katika sekta ya madini.
“Tanzania changamoto zake ni mbili tu kwenye sekta ya madini, umiliki na mfumo wa kodi ya kimataifa. Mfumo wa kodi ya kimataifa unayaruhusu makampuni kufungua makampuni dada kwenye nchi zenye kodi ndogo (tax haven)” amesema Zitto na kuongeza kuwa,
“Hapana sivyo, huwezi kuwa na hisa ya 16% ukapata faida ya 50% haiwezekani, haipo kokote duniani lakini unaweza kama ukimfanya muwekezaji kuwa mkandarasi sababu utamlipa fee yake na wala sio jambo la ajabu tunafanya hivyo kwenye sekta ya mafuta. Tuna mfumo maalumu wa kugawana faida”
Acacia ambayo ni kampuni tanzu ya Kampuni ya Dhahabu ya Barrick jana ilikataa kuilipa Tanzania fidia ya bilioni 700 ambazo Barrick ilikubali kuilipa Tanzania wakati wakiendelea na mazungumzo ya kutengeneza mfumo sahihi wa kugawana mapato yanayotokana na sekta ya madini.