MBUNGE wa Kigoma Kaskazini na Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Zitto Kabwe, amesema sakata la ufisadi wa fedha za manunuzi ya Rada, kati ya Serikali ya Tanzania na kampuni moja ya BAE Systems ya Uingereza, litarudishwa bungeni kwa maelezo kwamba suala hilo bado ni bichi.
- Zitto Kabwe akihutubia Kirumba Mwanza
Amesema, suala hilo la paundi 29.5 ambazo ni sawa na sh. bilioni 80 za Kitanzania, zilizogundulika kutaka kuliwa kupitia manunuzi ya rada lazima lirudishwe Bungeni, ikiwa ni pamoja na kutaka kujua riba iliyokuwa ikitozwa na benki katika urejeshwaji wa fedha hizo hapa nchini kutoka nchini Uingereza, na ‘chenji’ halisi iliyobaki, ili fedha hizo zisitumbukie tena kwenye mikono ya watu aliowaita mafisadi.
Zitto ametoa kauli hiyo jana Jijini Mwanza, wakati alipokuwa akizungumza kwenye ufungaji wa kampeni za uchaguzi mdogo wa Kirumba, ambapo alisema kamwe Chadema hawatalinyamazia jambo hilo.
“Hili suala la ufisadi wa fedha za rada halijaisha, na mimi nasema bado ni bichi. Tunataka kujua riba iliyotozwa na benki na chenji yetu iliyobaki. Tunaishukuru sana Serikali ya Uingereza kwa kutoboa ufisadi huu uliofanywa na vigogo wa Serikali ya CCM.
“Mafisadi walitaka kuzila hizi hela. Sasa Chadema na mimi hapa nasema hii ngoma bado mbichi kabisaa, tunaurudisha mjadala bungeni ili moto ukawake huko. Bila hivyo fedha hizi zinaweza kutumbukia tena kwenye mikono ya mfisadi”, alisema Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini.
- Mzunguko wa sakata la rada
Zitto ambaye hivi karibuni alikaririwa na vyombo mbali mbali hapa nchini akioelezea nia yake ya kutaka kugombea urais mwaka 2015, alisema Bunge ndicho chombo pekee kinachoweza kuhoji na kutoa mapendekezo yake dhidi ya watu waliohusika katika ufisadi huo pamoja na matumizi ya fedha hizo Serikali ya Uingereza iliagiza zirudishwe nchini.
Kwa mujibu wa Zitto, bila Bunge kuhoji fedha hizo, mafisadi wa CCM wataendelea kutamba nazo mitaani ikiwa ni pamoja na kuzitumia kujineemesha baadhi ya vigogo ndani ya chama tawala na Serikalini.
Hata hivyo, Zitto ambaye pia amewahi kukaririwa na badhi ya vyombo vya habari hapa nchini akiahidi kutokugombea nfasi yoyote ndani ya chama chke hicho cha upinzani, alikwenda mbli zaidi na kusema kwamba, wapo baadhi ya vigogo wanazimezea mate fedha hizo za rada zilizorudishwa, hivyo lazima Bunge lihoji ili mabilioni hayo ya fedha yasitumiwe na wabunge wa CCM kujitengenezea madawati na kuchimba visima vya maji katika majimbo yao.
Kutokana na utata wa suala hilo, Serikali ya Tanzania kupitia kwa Waziri wake wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo imekuwa ikitoa kauli zinaoonekana dhahiri kukinzana, kuhusu fedha hizo za rada na ujio wake.
Desemba 6, mwaka jana, Waziri Mkulo alinukuliwa na vyombo mbalimbali vya habari akisema tayari fedha hizo zilikwishaingizwa kwenye akaunti ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Akaunti ya London, Uingereza, lakini Machi 4 mwaka huu, Waziri huyo alidai fedha hizo bado hazijalipwa.
Hata hivyo, Februari mwaka jana, Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Kassim Majaliwa alisema tayari Serikali imezielekeza fedha hizo kutatua kero kwenye mipango ya elimu nchini, mojawapo ni kutengeneza madawati.
“Vyombo hivyo vilini-misquote (vilininukuu vibaya). Lakini ukweli ndiyo huu ninaokuambia leo…fedha hizo bado hazijaingia”, alinukuliwa na vyombo vya hbari akisema Mkulo hivi karibuni.
Waziri Mkulo alisema sababu za fedha hizo kutoingia kwenye akaunti hadi sasa ni kutokamilishwa kwa taratibu za kifedha kati ya Serikali za Tanzania na Uingereza.
“Unajua kila Serikali ina taratibu zake za kifedha. Lakini naweza kusema tumefikia mahali pazuri tu. Ni kwamba kwa sasa process (mchakato) zimefikia katika kiwango cha hali ya juu”, alinukuliwa tena akisema.
Habari hii imeandikwa na Sitta Tumma, FikraPevu – Mwanza