Wananchi Tunduru watozwa sh. 50 kugharamia ujenzi wa vyoo shuleni

Jamii Africa

Mazingira bora ya kufundishia na kujifunzia katika shule ni kichocheo kwa wanafunzi kufanya vizuri katika masomo yao na kupata ujuzi na maarifa yatakayowasaidia kutatua changamoto zilizopo katika jamii.

Uwepo wa vyoo katika shule ni sehemu muhimu kwa wanafunzi kujisitiri ili kulinda afya na kuwawezesha kufuatilia masomo wanayofundishwa.

Kwa tambua hilo, Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru imewekeza nguvu kubwa katika ujenzi wa vyoo vya kisasa katika shule za msingi vyenye huduma ya maji na vifaa vya usafi kwa wanafunzi.

Halmashauri hiyo ina jumla ya shule za msingi 150 zilizopo katika vijiji 157 zikiwa na wanafunzi  62,139 ambapo wavulana ni 31,303 na wasichana ni 30,836. Kwa muktadha huo kila shule ina wastani wa wanafunzi 414.

Kutokana na ongezeko la wanafunzi katika shule limesababisha mahitaji ya vyoo yaongezeke pia. Ili kukabiliana na changamoto hiyo, Halmashauri kupitia makusanyo yake ya ndani katika kipindi cha mwaka 2016/2017 ilitenga fedha katika bajeti ya uboreshaji wa matundu ya vyoo.

Milioni 38.8 zilitumika katika ujenzi wa matundu ya vyoo katika shule za msingi Wilayani Tunduru na miradi hii ya ujenzi wa vyoo ipo katika hatua mbali mbali. Vilevile kupitia fedha za ruzuku ya miradi ya maendeleo, milioni 21 zilielekezwa pia katika ujenzi wa matundu ya vyoo hivyo kupunguza changamoto hii kwa kiasi kikubwa.

 

 

Uwiano wa Wanafunzi na Vyoo

 Changamoto iliyobaki ni uwiano usioridhisha wa matundu ya vyoo na idadi ya wanafunzi. Katika shule nyingi za Wilaya hiyo vyoo vya kisasa vimejengwa lakini matundu ya vyoo hayakidhi mahitaji ya wanafunzi.

Kwa mujibu wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya 2014 inaelekeza kuwa wasichana 20 watumie tundu 1 la choo na wavulana 25 watumie tundu 1 katika shule za msingi ili kuhakikisha kunakuwa na uwiano mzuri wa wanafunzi na vyoo.

Mathalani, shule ya msingi Tunduru Mchanganyiko iliyopo kata ya Mlingoti Mashariki ina wanafunzi1,367 ambao wanatumia matundu ya vyoo 10 pekee, ambapo kwa wastani mwanafunzi 137 hutumia tundu 1 la choo.

Mahitaji ya wavulana na wasichana kwenye huduma ya vyoo hutofautiana. Shule hiyo ya Tunduru Mchanganyiko ina wasichana 655 ambao hutumia matundu 6. Ili idadi hiyo ya wasichana ikidhi uwiano wa 1:20 inatakiwa wasichana hao wapate matundu 33 ambapo kwa sasa wana matundu 6.  Kwa muktadha huo wasichana hao wanahitaji matundu 27  ya ziada ili kukidhi mahitaji yote ya vyoo.

Wavulana katika shule hiyo wako 712 ambao hutumia matundu 4, lakini kulingana na sera ya Elimu walipaswa kuwa na matundu 28 na hivyo wanahitaji matundu mengine 24 ili kukidhi mahitaji yote ya wavulana. Kwa ujumla shule ya Tunduru Mchanganyiko  ina upungufu wa matundu 41 ya vyoo kati ya matundu 51 yanayopaswa kuwepo shuleni hapo.

Takwimu za Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto  zinaonyesha kuwa asilimia 60 hadi 80 ya magonjwa yote ambayo watu hutibiwa hospitalini  yanasababishwa na kutozingatia kanuni za usafi ikiwemo matumizi yasiyo sahihi ya vyoo.

Hali hiyo haitofauti na shule msingi Umoja iliyopo kata ya Nanjoka ambayo  ina wanafunzi 553 ambapo wavulana ni 265 na wasichana ni 288. Wavulana wanatumia matundu 4 ya vyoo, hivyo wana upungu wa matundu 6, ambapo wasichana ni matundu 8. Kwa ujumla shule hiyo ina upungufu wa matundu 14 ya vyoo ili kukidhi maelekezo ya Sera.

Upungufu wa matundu ya vyoo katika shule za Tunduru Mchanganyiko na Umoja unaweza kuakisi hali halisi iliyopo katika shule mbalimbali nchini ambapo shule nyingine  hazina vyoo kabisa, ziko ambazo zina vyoo vichache ambavyo havikidhi mahitaji ya wanafunzi na maelekezo ya Sera  na kuhatarisha afya za wanafunzi hasa wa kike ambao hupata hedhi kila mwezi.

Katika uchunguzi uliofanywa na Programu ya SWASH Mapping Survey (2009) katika shule za msingi na sekondari katika Wilaya 16 za Tanzania ulibaini kuwa hali ya maji, usafi na afya katika shule za msingi haiku katika hali nzuri.

Ripoti ya Programu ya SWASH inaeleza kuwa ni asilimia 11 tu ya shule zote zilizochunguzwa zilikidhi kiwango cha taifa cha wasichana 20 na wavulana 25 kutumia tundu 1 la choo. Asilimia 20 ya shule zote ambao zina wanafunzi zaidi ya 100 hutumia tundu moja la choo na asilimia 6 ya shule hizo hazina vyoo kabisa.

 

Mkakati wa Halmashauri

Taarifa iliyotolewa na Afisa Elimu Shule za Msingi Wilaya ya Tunduru, Jafari Abrahaman kupitia Kitengo cha Habari na Mawasiliano inaeleza kuwa Halmashauri hiyo inaendelea na mikakati ya kumaliza tatizo la uhaba wa vyoo katika shule zote ili kuwawezesha wanafunzi kufikia ndoto zao.

“Katika bajeti ya mwaka wa fedha 2017/2018 jumla ya milioni 30 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa matundu ya vyoo katika shule za msingi”, inaeleza ripoti hiyo.

Pia Halmashauri ya Tunduru imeandaa mpango mkakati wa kumaliza tatizo la miundombinu ya elimu kwa kutumia mazao ya biashara yanayozalishwa katika wilaya yake.

“Kwa msimu wa zao la korosho mwaka 2017/2018 wakulima watachangia shilingi 50 kwa kila kilo moja ya korosho na fedha zitakazopatikana zitaelekezwa katika kuboresha miundombinu ya shule ikiwa ni pamoja na ujenzi wa vyoo vya kisasa”.

 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *