Mahitaji ya maziwa, nyama ya ng’ombe yaongezeka;  takwimu zakwamisha wafugaji kunafaika na soko la Afrika

Jamii Africa

Familia nyingi za watu walio vijijini ni za wafugaji wa wanyama kama ng’ombe, kuku, mbuzi, kondoo lakini zinaishi katika umasikini uliokithiri licha ya kuwa na rasilimali muhimu ya kutengeneza utajiri. Kwa muktadha huo ongezeko la mahitaji ya bidhaa ya wanyama linaweza kutengeneza fursa mbalimbali kwa wafugaji  ikiwa watapata taarifa na teknolojia ya kisasa ya ufugaji.

Lakini ukosefu wa takwimu za soko ni kikwazo kwa wafugaji kufaidika kwasababu maamuzi ya sera na uwekezaji hutegemea mfumo mzuri wa upatikanaji wa taarifa za mifugo na changamoto zilizopo kwenye sekta hiyo. Ukosefu wa taarifa na takwimu umejikita katika mambo matatu ambayo ni:

Kwanza, taarifa za maisha ya watu wanaojihusisha na ufugaji hazipo kwenye ngazi ya taifa, kwasababu ufugaji unawakilishwa kwa sehemu ndogo kwenye utendaji wa takwimu.

Taarifa hizo zinahitajiki siyo tu kwaajili ya kufahamu kaya zinazofuga mifugo na vikwazo vya uzalishaji bali kupima mchango wa mifugo kwa maisha yao na zaidi kufahamu faida wanayoipata kwenye uwekezaji wa mifugo na utashi wao wa kuwekeza kwenye mifugo.

Hizi ni taarifa muhimu kwa watunga sera na wawekezaji ambao wanadhamiria kuinua maisha ya wafugaji kwa kuwapatia faida kutoka kwenye mifugo. 

Pili, hata kama takwimu za wafugaji zimekusanywa, hazitoshelezi kuwarasimisha wafugaji kufuga kwa ajili ya biashara. Mfumo wa takwimu uliopo umeyatenga makundi madogo ya wafugaji ambayo hayawezi kujiendesha kibiashara. Kuna utofauti mkubwa miongoni mwa wafugaji ambapo wengi wangejikita kwenye uzalishaji wa nyama na wachache kwenye bidhaa za maziwa.

Hakuna mfumo thabiti wa kujikita kwenye aina moja ya ufugaji, na sababu kubwa ni kuwa takwimu hazionyeshi mgawanyiko wa majukumu katika sekta ya ufugaji.

   

Tatu, takwimu zilizopo za kaya zinazojihusisha na ufugaji wa kibiashara  hazitoshelezi kubaini vikwazo vya uzalishaji, teknolojia na soko. Kwa mfano takwimu zilizopo Tanzania zinaonyesha kuwa magonjwa ya wanyama na uhaba wa malisho ni kikwazo kikubwa kwenye uzalishaji wa bidhaa za wanyama. Ukosefu wa takwimu unazuia wataalamu wa mifugo kutengeneza sera na mipango ya kuendeleza sekta hiyo.

 

Fursa kwa wafugaji wa Tanzania

Licha ya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi tatu barani Afrika zilizo na idadi kubwa ya mifugo, bado wafugaji hawajafaidika na rasilimali hiyo muhimu kwa ukuaji wa uchumi wa kaya na taifa. Mahitaji ya maziwa na nyama ya ng’ombe yanaongezeka kwa kasi na ikiwa wafugaji watapata takwimu sahihi wanaweza kufaidika na soko lililopo Afrika.

Uchunguzi wa Shirika la Chakula Duniani (FAO) wa mwaka 2014 kuhusu teknolojia na data za ufugaji za Afrika unaeleza kuwa mahitaji ya bidhaa za wanyama katika nchi za Afrika yanaongezeka kwa kasi kuliko maeneo mengine duniani. Bidhaa hizo ni nyama na maziwa ya ng’ombe.

Ripoti ya uchunguzi huo inaeleza kuwa maziwa ni protini inayotumiwa sana na wakazi wa Afrika kwasababu inapatikana na kuuzika kirahisi, lakini pia inaweza kutumika kidogokidogo. Inakadiriwa kuwa Afrika ilitumia tani milioni 32.4 za maziwa kati ya mwaka 2005 hadi 2007 na idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka hadi tani milioni 50.2 ifikapo 2050 ambapo itakuza soko la maziwa kwa tani milioni 83.

Nyama ya kuku na ng’ombe ndio inayotumiwa sana – ambapo tani milioni 7.6 zilitumika mwaka 2005/2007 ikifuatiwa na nyama ya nguruwe na kondooo. Hadi kufikia mwaka 2050 matumizi hayo yataongezeka kwa tani milioni 8.9 huku soko la nyama ya kuku likifikia tani milioni 11.8 na ng’ombe tani milioni 13.6. Ripoti hiyo inabainisha kuwa hadi kufikia mwaka 2050 walaji wa mayai, nguruwe na kondoo wataongezeka maradufu.

                                    Maziwa ya ng'ombe yanawekwa kwenye chombo kimoja kwaajili ya kusindikwa

 

Licha ya fursa kubwa ya soko la bidhaa za wanyama barani Afrika, wazalishaji wa ndani hawakidhi mahitaji yote ya nyama na maziwa na matokeo yake bidhaa hizo huagizwa toka nje ya bara hilo. Uagizaji huo unakadiriwa kuongezeka kutoka tani 0.9 (2005) hadi tani milioni 5 (2050).  Ikiwa wawekezaji wa ndani hawatatumia vizuri fursa ya soko, inaelezwa kwamba kati ya 2030 na 2050, asilimia 15 ya mahitaji yote ya Afrika yatategemea  bidhaa kutoka nje.

Kwa kutambua hilo baadhi ya wafugaji wa ng’ombe katika Wilaya ya Kilosa na Mvomero wameanza kujihusisha kwenye ufugaji wa kibiashara ili kujipatia faida kwenye uzalishaji wa maziwa. Wameingia kwenye makubaliano na Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Mifugo (ILRI) ambayo inatekeleza mradi wa ‘MoreMilkiT’  ili kuinua maisha ya wafugaji wa wilaya hizo ambao kwa sehemu kubwa wanategemea ufugaji kama shughuli ya kiuchumi.

Mradi wa ‘MoreMilkiT’ unafadhiliwa na shirika la Misaada la Ireland na kutekelezwa na Chuo Kikuu cha Sokoine, Faida Mali, Heifer International Tanzania, Board ya Maziwa Tanzania na ILRI ili kuwaongea wafugaji ujuzi na teknolojia ya kuzalisha maziwa mengi. Pia kuwatafutia fursa za soko ndani na nje ya Tanzania.

Hata hivyo, mradi huo unalenga kuongeza uzalishaji wa bidhaa za maziwa ikiwemo siagi na protini.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *