WAHENGA walisema tembea uone mambo,ndivyo nilivyofanya mimi kufunga safari kutoka mjini Songea hadi kufika katika kijiji cha Darpori wilayani Mbinga mkoani Ruvuma umbali wa takribani kilometa 200.
Kijiji cha Darpori kipo mpakani mwa Tanzania na nchi ya Msumbiji ,kutoka katika kijiji hicho kueleka nchini Msumbiji kwa mguu ni dakika 60,wakazi wa kijiji hiki ni wageni ambao wamefika katika kijiji hicho kwa ajili ya kufanyakazi ya uchimbaji na ununuzi wa madini mbalimbali yakiwemo dhahabu ambayo yanapatikana kwa wingi katika kijiji hicho.
- Kijiji cha Darpori wilayani Mbinga kilichopo mpakani mwa Tanzania na Msumbiji chenye wakazi 10,000 kimezungukwa na milima yenye utajiri wa madini ya dhahabu
Mwenyekiti wa kijiji cha Darpori Andason Haule anasema kijiji hicho chenye watu karibu 10,000 kilianza rasmi mwaka 2004 kikitokana na eneo ambalo ulikuwa msitu kugundulika kuwa na mkondo wa madini mengi aina ya dhahabu na kwamba kijiji kina karibu makabila yote 120 yaliopo nchini pamoja na wananchi kutoka nchi jirani za Malawi na Msumbiji.
Kijiji cha Darpori kilichopo katika kata ya Tingi wilayani Mbinga mkoani Ruvuma kinachoundwa na vitongoji vinne ambavyo ni Songeapori, Lunyere, Tanzania One na Njarambe, katika hali ya kusikitisha hakina kituo chochote cha kutolea huduma ya afya hali ambayo inasababisha matatizo mengi kwa wakazi wa kijiji hicho ikiwemo kusababisha vifo ambavyo vingeweza kuzuilika.
Moja ya mitaa maarufu yenye urefu wa mita 500 katika kijiji cha Darpori ambacho wakazi wengi ni wafanyabiashara na wachimbaji wa madini
Mwenyekiti wa kijiji hicho anasema akinamama wajawazito wanasafiri umbali wa kilometa 18 hadi kijiji jirani cha Mpepo ambako kuna zahanati ya kanisa katoliki kwa ajili ya kwenda kupima kliniki watoto pamoja na kupata huduma ya uzazi na kwamba katika kijiji hicho kuna mkunga wa jadi ambaye wakati mwingine anawasaidia akinamama kujifungua hata hivyo wengi wanapoteza maisha kila mwaka.
“Hapa kijijini makaburi ya akinamama wajawazito na watoto chini ya umri wa miaka mitano imekuwa ni jambo la kawaida, sisi viongozi tupo katika wakati mgumu tunashindwa hata kuitisha mikutano ya hadhara kwa kuwa kwenye mikutano hiyo kilio kikubwa cha wananchi ni kupata zahanati hivi sasa wanatumia shilingi 20,000 nauli ya kwenda na kurudi hadi kwenye zahanati ya Mpepo kufuata huduma ya afya hali ni mbaya’’, anasisitiza.
“Wanawake wamekuwa wakitoa kilio chao kwamba serikali ya kijiji haifanyi kazi wanakufa njiani kutokana na kijiji hicho kukosa zahanati sasa mimi mwenyekiti wa kijiji nitafanya nini, mbunge ameshaambiwa mara kadhaa, viongozi ngazi ya wilaya wameambiwa lakini ahadi zimekuwa nyingi kuliko utekelezaji’’, anasema.
Joyce Nchimbi mama mwenye watoto wanne anasema hali ya afya ni mbaya zaidi wakati wa mvua kwa kuwa barabara inakuwa haipitiki hivyo akinamama wengi wanashindwa kusafiri kutoka katika kijiji hicho hadi Mpepo kwenda kujifungua au kupima kliniki wao wenyewe pamoja na watoto wenye umri chini ya miaka mitano hali ambayo inaleta hofu katika hustawi wa jamii.
Hata hivyo afisa mtendaji wa kijiji cha Darpori Raphael Mapunda anasema katika kukabiliana na tatizo la huduma ya afya serikali ya kijiji imehamasisha wananchi katika vitongoji vyote vinne kufyatua tofali 700,000 za ujenzi wa kituo cha afya cha kata ya Tingi na hatimaye kulitafutia ufumbuzi wa kudumu tatizo la ukosefu wa huduma ya afya ambalo linatafuna maisha ya watu mara kwa mara.
Mmoja wa akinamama katika kijiji cha Darpori akishiriki katika kazi za kujitolea ubebaji wa tofali na mawe kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya ambacho kinatarajia kuanza kabla ya mwisho wa mwaka huu
Kwa upande wake diwani wa kata ya Tingi Aureus Masuja anasema kata hiyo yenye vijiji nane ambavyo ni Darpori, Tingi, Kiulunga, Mpepo, Malungu, Upolo, Kilindinda na Luhindo tangu nchi ipate uhuru haijawahi kupata zahanati ya serikali badala yake katika kata nzima yenye watu zaidi ya 16,000 inategemea zahanati mbili za kanisa katoliki ambazo zipo kwenye vijiji vya Mpepo na Tingi.
“Tangu tupate uhuru hatujawahi kuwa na hospitali au zahanati ya serikali, katika huduma ya afya katika kata nzima tunasaidiwa na zahanati mbili za kanisa katoliki,hatujawahi kuwa na mradi wa zahanati,hata hivyo miradi ya zahanati imeanza katika vijiji vya Upolo na Kilindinda zahanati zimefikia hatua ya ujenzi wa msingi, mradi wa zahanati katika kijiji cha Luhindo wamefikia hatua ya madirisha pia mradi wa kituo cha afya cha kata katika kijiji cha Darpori ufyatuaji wa tofali unaendelea’’,anasisitiza.
Masaju anabainisha kuwa huduma za afya zinazotolewa katika zahanati mbili za kanisa katoliki kwa wananchi wa kata nzima bado hazikidhi ukubwa wa eneo la kata nzima ya Tingi hali ambayo inawalazimisha wananchi kufunga safari ya kwenda mjini Mbinga kufuata matibabu ya uhakika na kwamba wananchi wanapata athari kubwa ambapo wajawazito wengi wamekuwa wanajifungulia barabarani au kupoteza maisha wakati wanakwenda kutafuta huduma za afya.
Anasisitiza kuwa idadi kubwa ya watoto wachanga wanateketea kwa kupoteza maisha kutoka na ugonjwa wa malaria ambao unaongoza kwa kuwashambulia wananchi wa kata hiyo ukilinganisha na magonjwa mengine.
Ametoa mwito kwa serikali ya Halimashauri ya wilaya ya Mbinga kuhakikisha kuwa wanawaunga mkono wananchi wa kata ya Tingi ili kuhakikisha kuwa miradi yao ya ujenzi wa zahanati pamoja na kituo cha afya inamalizika kwa muda uliopangwa ili hatimaye huduma za afya zianze kutolewa jirani na wananchi na kupunguza au kumaliza vifo visivyokuwa vya lazima ambavyo vinamaliza nguvu kazi ya taifa kila mwaka.
Thank you for opening my eyes about Tanzania!
Unafanya kazi nzuri sana wengi inabidi wajue hali ya nchi yetu na hasa Songea yetu…