WAKATI baadhi ya hospitali zikiathiriwa na mgomo wa madaktari, mkoani Mwanza kumetokea kituko baada ya zahanati kusitisha huduma na kufungwa kwa kuwa tu muuguzi wake ameanza likizo.
Zahanati ya Kata ya Ngula Wilayani Kwimba mkoani Mwanza, ndiyo ambayo imefungwa na huduma kusimamishwa kutokana na kuwa na muuguzi mmoja tu ambaye amelazimika kuanza likizo yake ya mwaka na zahanati kufungwa.
Zahanati hiyo ambayo muuguzi wake ametajwa kwa jina moja la Magdalena, inahudumia vijiji vinne vya Nyamatale, Ngula, Ng’hulya pamoja na kijiji cha Ngogo, na kwamba zaidi ya watu 25,000 wanategemea kupata huduma katika zahanati hiyo ambayo kwa sasa imefungwa.
Kwa mujibu wa uchunguzi huo, kwa sasa wananchi waliokuwa wakitegemea huduma katika zahanati hiyo wamekuwa wakilazimika kutembea umbali unaokadiriwa kuwa zaidi ya kilometa 30 hadi 50 kwenda kupata huduma katika maeneo mengine, huku baadhi yao wakishindwa kumudu safari hiyo ndefu, hivyo hujikuta wakiathirika.
Taarifa zisizo rasmi zinadai kwamba, wapo baadhi ya watu wamepoteza maisha yao kutokana na kukosa huduma kwa ukaribu, huku wengine wakilazimika kusafirishwa hadi hospitali ya wilaya iliyopo na umbali mrefu kutoka maeneo husika.
“Tulisikia kuna watu kama wawili hivi wamekufa baada ya kukuta kituo hakifanyi kazi kimefungwa. Tulisikia tu ila hatujui kama ni kweli maana ukweli watu wengi tunahangaika sana kutafuta huduma”, alisema mwana mama mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Mama Samwel.
Diwani wa Kata hiyo ya Ngula, Palu Mashagu (CUF), pamoja na Mkuu wa wilaya hiyo, Christopher Ryoba Kangoye (DC), wamethibitisha kufungwa kwa zahanati hiyo, ambapo Diwani Mashagu alisema: “Hili ni tatizo kubwa sana. Haiwezekani kituo kifungwe kutoa huduma kwa sababu ya Muuguzi wake kaenda likizo. Hivi tupo na Serikali ya aina gani hii?.”
Alisema, hiyo ni mara ya pili kufungwa kwa zahanati hiyo baada ya Muuguzi wake kwenda likizo nyumbani kwao, na kwamba hali kama hiyo ilijitokeza Machi mwaka jana 2011, ambapo wananchi hao waliathirika kwa kukosa huduma za matibabu baada ya huduma hiyo kufungwa hadi Aprili mwaka huo.
“Mwaka jana napo zahanati hii ilifungwa kwa tatizo hili hili la mtaalam kwenda likizo…ilikuja kufunguliwa mwezi wa nne. Nasema kwa niaba ya wananchi wangu wa kata ya Ngula hatutavumilia hali hii mbaya.
“Kwa nini Serikali isilete wauguzi wengine wengi?. Inakuwaje kituo kama hiki kinahudumia maelfu ya watu kiwe na mtaalamu mmoja tu?. Tunataka Serikali ilete haraka Muuguzi ili watu wangu wapate huduma”, alisema Diwani huyo wa Kata ya Ngula, Mashagu (CUF).
Hata hivyo, Mganga Mkuu wa wilaya hiyo (DMO), aliyefahamika kwa jina moja la Dk. Bisulu alipoulizwa leo kwa simu alitofautiana na kauli ya Mkuu wa wilaya hiyo pamoja na diwani wa Kata ya Ngula kwa kusema: “Mimi nipo safarini, lakini mbona alishapelekwa Muuguzi mwingine?. Ngoja niulizie maana si kwamba bado imefungwa, nimeambiwa yupo mtu kapelekwa huko Ngula”.
Habari hii imeandikwa na Sitta Tumma – Mwanza