Benki ya Dunia yamwaga mabilioni kujenga masoko, barabara Mara

Jamii Africa

BENKI ya Dunia (WB), imetoa ufadhili wa zaidi ya sh. Bilioni 13 katika Manispaa za mkoani Mara, na kwamba fedha hizo zimelenga kujenga barabara za lami na masoko ya kisasa, ambapo baadhi ya masoko hayo yatajengwa kwa gorofa.

Imeelezwa kwamba, fedha hizo zitatolewa na benki hiyo kwa awamu tofauti, ambapo awamu ya kwanza Manispaa hiyo imepewa dola za Kimarekani milioni 2.5, ambazo ni sawa na karibu sh. Bilioni 4 za Kitanzania, na utekelezaji wa miradi hiyo utaanza mara baada ya taratibu zote kukamilika.

Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo ya Musoma, Alex Malima Kisurura ameiambia FikraPevu mchana huu wa leo, wakati alipohojiwa kuhusiana na utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Manispaa hiyo iliyopo kwenye jimbo la Musoma mjini, chini ya mbunge wake Vincent Nyerere (CHADEMA).

Alizitaja barabara zitakazojengwa kwa kiwango cha lami katika jimbo hilo la Musoma mjini kwa ufadhili huo wa benki ya dunia, kuwa ni barabara ya kuanzia Nyasho itakayopitia Kamunyonge sokoni, Kennedy pamoja na barabara la Kawawa hadi Mwigobero, na alisema ujenzi wa barabara hizo utachochea maradufu ukuaji wa uchumi kwa wananchi wa Musoma.

“Benki ya dunia imekubali kutupatia sh. Bilioni 13 kwa ajili ya kujenga barabara za lami na masoko ya kisasa katika Manispaa yetu ya Musoma. Ufadhili huu ni muhimu sana kwa maendeleo ya wananchi!. Kawaida benki ya dunia wao wanatoa fedha kwa ajili ya miradi ya barabara. Lakini sisi Musoma tukawaomba fedha hizo tuzitumie pia kujenga masoko ya kisasa likiwemo soko moja tutakalojenga kwa gorofa”, alisema Meya huyo wa Musoma, Kisurura.

Hata hivyo, Meya huyo wa Musoma aliyataja masoko yatakayojengwa kuwa ni lile la Nyasho na soko la Nyakato kwa saa nane, na kwamba lile la Nyasho ndilo litakalojengwa gorofa, na kwamba tayari tenda ya ujenzi wa miradi hiyo ilishatangazwa na Oktoba 16 mwaka huu tenda hiyo inatarajiwa kufunguliwa, na makampuni yatakayopata kazi ya kujenga miradi hiyo lazima yatekeleze kwa kujenga na kukamilisha ndani ya muda unaotakiwa kwa mujibu wa mkataba, na si vinginevyo.

Habari hii imeandikwa na Sitta Tumma – FikraPevu, Musoma

1 Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *