Udalali, utapeli kukwamisha kasi ya ufugaji sungura nchini

Jamii Africa

MONICA Kiondo, mkazi wa Sinza jijini Dar es Salaam, yuko na mfanyakazi wake akihangaika kuwanyonyesha watoto wa sungura huku jua la utosini likiwaka.

“Mama yao hataki kuwanyonyesha, sasa naogopa wasije wakafa wote kama wa kwanza ambao walikufa,” anasema.

Anaongeza: “Ni wiki sasa nawapigia watu walionifundisha na kuniuzia sungura hawa ili wanipe msaada kama walivyoahidi, kila siku wanasema wanakuja lakini hawaji, wakati mwingine wakiiona simu yangu wanaikata ama hawapokei.”

Monica ni miongoni mwa wanajamii ambao wameamua kuingia kwenye mradi wa ufugaji wa sungura ili kujiongezea kipato, ingawa hakuwa na uzoefu wowote wa ufugaji wa wanyama hao wadogo wenye faida nyingi.

Anasema alishawishika kuingia kwenye ujasiriamali huo kwa vile ni wanyama wasiogharimu muda wake mwingi lakini pia anahitaji kuongeza kipato licha ya kuwa na ajira nyingine.

Pembeni ya banda la sungura lipo pia banda la kuku wa kienyeji wa kila aina wanaokadiriwa kufikia 30 hivi.

“Ninapenda kufuga, nimeachana na ufugaji wa kuku wa nyama ambao walikuwa wakinitia hasara sana nikaamua kufuga wa kienyeji na hawa sungura,” anasema.

Anasema kwamba, licha ya kutafuta kipato cha ziada, kuingia kwake kwenye ufugaji sungura kulitokana na matangazo ya kampuni moja ya uwakala (jina linahifadhiwa) ambayo ilidai kwamba inatoa mafunzo, mbegu  na mabanda kwa wakulima ikiwa ni pamoja na kuwatafutia masoko, achilia mbali kusaidia kuwahudumia sungura hao.

Tofauti na alivyotegemea kwamba baada ya mafunzo angeweza kuendelea mwenyewe na ufugaji huo, lakini kampuni hiyo licha ya kumuuzia mabanda na sungura wa kuanzia 14 – majike 12 na madume wawili – kwa gharama ya takriban Shs. 2 milioni, ilimsainisha mkataba wa miaka mitano kwa masharti kwamba lazima chakula cha sungura anunue kwao pamoja na dawa za kuwatibu wanyama hao.

Hata hivyo, kampuni hiyo hiyo kwa sasa imekwishapandisha bei ambapo seti hizo mbili zinauzwa kwa Shs. 4 milioni, hii ikiwa inatokana na mwamko wa wananchi katika ufugaji wa sungura.

“Walisema wangetoa wataalamu wao kuja kuwahudumia wanapokuwa na matatizo, lakini lazima nilipe mimi gharama za wataalamu na dawa, huku wakinizuia (kwa mujibu wa mkataba) kutafuta tiba za wanyama hawa sehemu yoyote.

“Lakini tayari nimeshapoteza sungura mkubwa mmoja na watoto nane ambao walikufa kutokana na mama yao kugoma kuwanyonyesha, kwa vile sina uzoefu na ufugaji huu, imekuwa ni hasara kubwa kwangu,” anasema.

Sharti jingine, kwa mujibu wa Monica, ni kwamba anawajibika kuwauza sungura watoto wote kwenye kampuni hiyo ya uwakala pindi wanapofikisha umri wa miezi minne na kwamba haruhusiwi kuwauza popote.

Sungura hao watoto, kwa mujibu wa Monica, wananunuliwa na kampuni hiyo kwa uzito wakiwa hai (live weight) ambapo kilogramu moja wananunua kwa Shs. 8,000.

Kwa mujibu wa mchanganuo wao ambao ndio kivutio cha wakulima wengi kuingia kwenye biashara hiyo, wanasema katika umri wa miezi hiyo minne, sungura anakuwa amefikisha uzito wa kilogramu 4, hivyo kwa bei ya Shs. 8,000 sungura mmoja atanunuliwa kwa Shs. 32,000.

Kwamba ikiwa kila sungura atazaa watoto 6, na ikiwa utawazalisha mara 6 pia kwa mwaka, maana yake kwa sungura 12 utakuwa na sungura watoto 432 ambao kwa Shs. 32,000 utapata Shs. 13,874,000 huku gharama zote zikiwemo za matunzo zikiwa Shs. 3,456,000 na hivyo kukusanya faida ya Shs. 10,368,000.

“Faida inaonekana kubwa na inashawishi. Mwanzoni niliona kwamba hiyo ni nafuu kwa sababu wanasema wao wana masoko na wanasafirisha kupeleka nje ya nchi, hasa Uarabuni na China, ambako mahitaji ya nyama ni makubwa, lakini kadiri ninavyoangalia naona nakula hasara,” anasema.

Hata hivyo, anasema uhalisi uko tofauti kwa vile katika umri wa miezi minne sungura hao wanakuwa hawajafikisha uzito wa kilo 4, wengi wao wakiwa na uzito wa kilo 1.5, tena waliotunzwa vizuri.

“Kinachoniumiza zaidi ni kwamba, tayari nimekwishaingia kwenye mkataba ambao umenifunga, maana yake siwezi kuwazalisha hawa watoto hata kama nataka waongezeke na kwa mujibu wa mkataba, nikitaka niongeze wengine, lazima nikanunue seti nyingine mbili, achilia mbali kuzuiwa kuwauza mahali pengine hata kama nitapata soko zuri zaidi,” anasema kwa masikitiko.

Kilio cha Monica kinaonekana kuwakumba wakulima wengi, siyo wa jijini Dar es Salaam tu, bali katika mikoa mingi ambako wameamua kuingia kwenye ufugaji wa sungura kupitia kwenye kampuni za uwakala.

Simon Marwa, mkazi wa Kivule jijini Dar es Salaam, ni miongoni mwa wakulima ambao wamenaswa kwenye mitego ya mwakala hao wa ufugaji wa sungura, ambapo anasema alishawishiwa kujiunga na kampuni moja (ambayo aligoma kuitaja kwa sababu ya usalama wa kibiashara) baada ya kuambiwa kwamba wangepatiwa sungura 10 kila mmoja pamoja na mabanda yake, chakula na utaalamu.

Anabainisha kwamba, kabla ya kupatiwa mafunzo, alilazimika kwenda na barua ya mjumbe, vitambulisho mbalimbali pamoja na ada ya kiingilio ya Shs. 500,000 na kuaminishwa kwamba atapata fursa zote muhimu ikiwemo kuunganishwa kwenye mifuko ya kijamii pamoja na kupatiwa bima ya afya.

Hata hivyo, licha ya kujiunga, aliambiwa kwamba ni lazima waunde kikundi cha watu 50 ili wakidhi vigezo, jukumu ambalo aliambiwa ni lake kuhakikisha anawashawishi watu mbalimbali wajiunge naye kwa vile wanachama wengine tayari walikuwa kwenye vikundi.

“Hapa ndipo niliposhtuka, kwa sababu mwanzoni tuliambiwa tunapewa mikopo ya sungura, sasa masharti ya kutafuta watu 49 yalikuwa mapya, na je, kama sikuwapata itakuwaje?

“Halafu najaribu kuangalia, kampuni inasema inatupatia mkopo – au inatudhamini mkopo kutoka benki ambao unalipwa kwa kuwauza sungura watakaozaliwa – lakini hebu piga hesabu, kama tayari mpaka sasa wameshafikisha wanachama milioni moja kama wanavyosema, kwa kukusanya kiingilio cha Shs. 500,000 kwa kila mwanachama maana yake wamekusanya jumla ya Shs. 500 milioni! Sisi ndio tumewapatia mtaji… huu ni utapeli,” anasema.

Hofu nyingine anayodai kwamba ilimpata ni maelekezo kuwa hata kama watapatiwa sungura hao, hawaruhusiwi kuwachukua kwenda kuwafuga majumbani mwao, bali wanatakiwa kuwekwa mahali pamoja na mhusika atakuwa anakwenda tu kuwaangalia baada ya kuonyeshwa banda lake.

“Inakuwaje huyo ni mtoto lakini unaambiwa huruhusiwi kumnyonyesha, anakaa kwa jirani na wewe unakwenda kumwangalia tu? Halafu ninawezaje kuwa na uhakika kama banda nitakaloonyeshwa ni langu mwenyewe na siyo kwamba linaweza kuonyeshwa kwa mwingine? Nimepata mashaka makubwa na ninahisi biashara hii imekwishaingiliwa na madalali na matapeli licha ya ukweli kwamba ufugaji huu ni mzuri na wenye tija,” anafafanua.

Kwa upande wake, Michael Samia, mkulima na mkazi wa Mbezi jijini Dar es Salaam, anasema yeye alishtuka mapema kuhusu masuala ya mikataba, lakini kwa vile anafahamu kuwafuga wanyama hao, alilipia seti nne na kupewa mahitaji yote huku akigoma kusaini mkataba.

“Mimi kazi yangu ya kwanza kunipatia fedha nilipokuwa mdogo ni ufugaji wa sungura, hivi sasa ninajiandaa kustaafu nataka kazi yangu ya uzeeni iwe sungura, kwa hiyo sikwenda pale kwa kubahatisha, nimedhamiria kufuga kibiashara.

“Walinifuata hapa nyumbani mwezi uliopita wakaja na mikataba yao, lakini nikawaambia sina haja ya mkataba na mtu yeyote kwa sababu ninaweza kujiendesha mwenyewe na kutafuta masoko… mkataba gani unaoingia na watu ambao hawajakupa bure kitu chochote? Huo ni wizi na utapeli,” alisema kwa kujiamini.

Mkulima huyo ambaye kwa sasa anao sungura takriban 80, anasema lengo lake kubwa ni kuwafuga kwa wingi shambani kwake Bagamoyo na kuanzisha biadhara ya ‘sungura choma’ kama ilivyo kwa ‘mbuzi choma’.

Hata hivyo, anawaasa wakulima wenzake kujihadhari na madalali na matapeli akionya kwamba, biashara hiyo hivi sasa imekwishaingiliwa na wajanja kama ilivyokuwa ufugaji wa kware.

Kauli ya Samia inaungwa mkono na Exaud Mkufya, ambaye licha ya kuwa mhanga wa ufugaji wa kware, anasema madalali na matapeli wameuvamia ufugaji huo wa sungura na muda si mrefu unaweza kuonekana hauna maana.

Anasema kwamba, kupanda ghafla kwa bei za mbegu za sungura pamoja na vitisho vinavyotolewa na baadhi ya madalali kwamba bila kupitia kwenye kampuni mkulima hawezi kufanikiwa ni ishara tosha kuwa wapo ‘wapiga dili’ wanaotaka kujinufaisha kupitia kwa wakulima.

“Kuna kijana namfahamu kabisa, aliwahi kuniulizia wapi anaweza kununua sungura, hawa wa kienyeji, nikamwelekeza mahali huko kijijini ambako alikwenda na kununua kwa Shs. 2,000 kila mmoja, hivi sasa namuona kwenye mitandao ya kijamii akiwauza sungura wale wale – ambao amewapachika majina ya sungura wa kigeni – kwa bei ya Shs. 35,000!” anasema Exaud.

Anaongeza kwamba, biashara ya ufugaji wa kware nayo ilianza hivyo hivyo, ambapo yeye alihamasika katika uuzaji wa mayai kwa maelezo kwamba bei ya tray moja ni Shs. 30,000, lakini baada ya kutumia Shs. 8 milioni, alishindwa kupata soko na kupata hasara ya ajabu.

Hata hivyo, amebainisha kwamba, ufugaji wa sungura ni kama wanyama wengine na kuwataka wakulima wafuge si kwa kupewa ndoto za mafanikio ya haraka, bali watambue faida na umuhimu wake.

Meshack Maganga ni mwalimu wa ujasiriamali anayeishi Iringa, ambaye anabainisha kwamba, ufugaji wa sungura ni muhimu katika kuongeza kipato bila kutumia muda mwingi.

Anasema kwamba, kwa uzoefu wake, sungura wala nyama yake haijawahi kusafirishwa kutoka Tanzania kwenda nje kama baadhi ya madalali wanavyowahadaa wananchi, bali wanyama hao wanaweza kufugwa kutokana na faida nyingi walizonazo.

“Ufugaji wa sungura ni kama wa kuku, na nyama ya sungura ni nyeupe kama ya kuku, samaki na nguruwe ambayo haina lehemu kutokana na kutokuwa na mafuta mengi, hivyo inafaa sana kwa matumizi ya binadamu,” anasema na kuongeza kwamba, ikiwa jamii itawafuga kwa kutambua umuhimu wa kwanza wa matumizi ya familia, hiyo itaondoa wimbi la matapeli ambao daima wanatafuta fursa za kujinufaisha.

Wataalamu wengi wa mifugo wanaeleza kwamba, licha ya nyama yake kuwa na viinilishe vingi, lakini mkojo wa sungura una faida kwa kuwa unatumika kwenye viwanda kutengeneza dawa za kuulia wadudu na unatumika pia kama mbolea hai ya majimaji (organic fertilizer) na unaweza kunyunyiziwa moja kwa moja kwenye miche kama kahawa, michunywa, miembe na korosho badala ya kutumia kemikali za kuulia wadudu.

Aidha, kinyesi cha sungura kinafaa kuzalishia minyoo kwa ajili ya kulishia kuku wa kienyeji pamoja na samaki, hivyo kama wanyama hao wanafugwa katika kilimo mchanganyiko wanakuwa na manufaa makubwa.

Serikali imekuwa ikihamasisha wananchi kujikita katika miradi endelevu ya ufugaji wa wanyama mbalimbali, wakiwemo sungura, ikiwa ni jitihada za kuongeza uhakika wa chakula na kipato na hivyo kutokomeza umaskini na kukabiliana na baa la njaa, kama inavyoelekezwa kwenye Dira ya Taifa ya Maendeleo kuelekea mwaka 2025, Mpango wa Kukuza Uchumi na Kupambana na Umaskini (Mkukuta II).

Aidha, ufugaji huo wa sungura na wanyama wengine upo katika utekelezaji wa malengo namba 1 na 2 ya Malengo Endelevu ya Dunia (SDG) yaliyopitishwa na Umoja wa Mataifa Septemba 22, 2015 ambayo yanasisitiza kutokomeza umaskini pamoja na kuongeza uhakika wa chakula.

Katika kipindi hiki ambacho serikali inahimiza kilimo na ufugaji endelevu wenye manufaa, taasisi za umma kama Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi imefungua milango kwa vijana wajasiriamali kujifunza ufugaji mbalimbali, ukiwemo wa sungura.

 

 

1 Comment
  • Sio huyoo tuu hata mm nilijiunga na tbcc lakini mpaka sasa hawajaniletea sungura na waenda mwezi wa tatu sasa kila nikiwapigia ni majibu ya mwisho wa mwez tu ndo utolewa… sasa nimebaki nisijue la kufanya hata… ni matapeli wakubwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *