MUSWADA mpya wa Sheria ya Afya unaotarajiwa kuwasilishwa Bungeni wiki ijayo umezua kizaazaa baada ya serikali kugomea mapendekezo yote ya wadau yaliyotolewa wiki iliyopita katika Kamati ya Kudumu ya Huduma za Jamii, FikraPevu inaripoti.
Katika muswada huo wa Sheria ya Madaktari, Madaktari wa Meno na Wataalamu wa Afya Shirikishi, Serikali imekataa madaktari wasaidizi (AMO) na madaktari wasaidizi wa meno (ADO) kutambuliwa kama Madaktari kwa kuwa hawana sifa.
Badala yake, wanataaluma hao wanatarajiwa kuwekwa katika kundi la ‘Wataalamu wa Afya Shirikishi’, na kwamba pamoja na serikali kutambua mchango wao, hawataitwa madaktari kwa kuwa sifa kubwa ni lazima wawe na shahada inayotambulika.
“Serikali inatambua na kuthamini mchango wa wataalamu hao katika huduma za afya lakini hawataitwa madaktari katika muswada huu kutokana na sifa za udaktari,” alisema Ummy Mwalimu, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, wakati wa kikao hicho cha wadau kilichofanyika mjini Dodoma.
Hata hivyo, inaelezwa kwamba, kuunganishwa kwa wanataaluma hao wa makundi mawili tofauti kutaleta athari kubwa kwa wananchi wengi, kwani hawaweza kufanya huduma za upasuaji zikiwemo operesheni za uzazi ambazo zimesaidia kupunguza kwa kiasi kkikubwa vifo vya mama na mtoto hasa kwa akinamama wanaoishi vijijini.
“Kutakuwa na madhara makubwa sana, kwa sababu wataalamu hao hawataweza kufanya upasuaji jambo ambalo linaweza kuongeza idadi ya vifo, hasa vya mama na mtoto,” kimeeleza chanzo kimoja.
Zipo tetesi kuwa watumishi wa kada hiyo wamejipanga kuacha kufanya operesheni za aina yoyote pamoja na zile za uzazi kama sheria hiyo itapita na kutumika.
Hoja wanayoitua wataalamu hao inaelezwa iko tofauti na iliyotolewa na serikali, kwamba wanachokitaka wao si kutambuliwa kama Madakatari (MD) bali wanataka watambuliwe kama madaktaria wasaidizi.
“Kuna upotoshaji kwamba eti wanataka kutambuliwa kama MD wakati siyo kweli, wao wanataka kutambuliwa kama madaktari wasaidizi na siyo wanataaluma shirikishi wa afya wakati wanafanya kazi kama MD na wanasaidia madaktari wanafunzi kazi za upasuaji,” kimeeleza chanzo kingine.
FikraPevu inafahamu kwamba, idadi ya madaktari wa tiba (MD) nchini Tanzania ni wachache kutokana na mzigo mzito wa kazi hasa katika hospitali za rufaa, ikilinganishwa na Madaktari Wasaidizi (AMO), ambapo wengi wao wako wilayani ambako mahitaji ya huduma za afya ni makubwa huku maeneo mengi yakiwa hayafikiki kirahisi.
Uchunguzi unaonyesha kwamba, madaktari wa tiba (MD) wako 1,709, idadi ambayo haipishani sana na Madaktari Wasaidizi wa Tiba (AMO) ambao wako 1,737 na wengi wao wako wilayani ambako uhitaji ni mkubwa na hawatoshi, huku Wahudumu wa Afya (Medical Attendant) wakiwa 20,622 nchi nzima.
Kwa upande wa afya ya kinywa na meno, Madaktari Wasaidizi wa Meno (ADO) wako 177 tu nchi zima wakati Madaktari Bingwa wa Meno (Dental Surgeon) wako 131.
Awali, wataalamu hao walipendekeza waondolewe katika kundi la wataalamu wa afya shirikishi na kutambuliwa kama madaktari kwa kuwa wana ujuzi na wanahudumia.
Waziri Ummy alisema wizara yake imekubali maoni ya wadau kuhusu usajili wa muda wa madaktari kuondolewa ili kuendana na mtengamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
“Tumeona haja ya kupanua tafsri ya Allied Health kwa taaluma kama Orthotics, Prosthetic, Occupational, Therapist, Speech Therapist na mengine na taaluma hizo ni sehemu ya wataalamu wa afya shirikishi,” alisema.
Alisema Wizara imependekeza pia jina la Baraza kubaki kama lilivyo na imekubali kuongeza idadi ya wajumbe kuwa tisa kwa kuongeza mwakilishi mmoja wa afya shirikishi na mtaalamu na mwakilishi kutoka mikoani.
“Kifungu 5 (4) kimeruhusu uwakilishi wa ziada wa taaluma nyingine pale inapobidi, hilo tumekubaliana nalo lakini suala la Mwenyekiti wa Baraza kupendekezwa na vyama vya kitaalamu tumelikataa na kushauri libaki kwa Waziri,” alisema Ummy.
Wizara pia imekataa pendekezo la Baraza lisitoe adhabu ya kuonya, kukalipia, kusitisha kwa muda na kufuta cheti bila kupata hukumu kwa kuwa suala hilo litadhoofisha Mamlaka ya Baraza na kuongeza urasimu wa maamuzi na pia kuwapo kwa hatua hiyo ni kuendana na sheria za Utumish wa Umma.
Alisema pia wameshauri kifungu kinachompa Waziri mamlaka kutoa maelekezo kwa baraza kibaki kama kilivyo pamoja na hoja ya wadau kudai kitapunguza uhuru wa baraza kwa kuwa baraza hilo linahudumia wataalamu na jamii.
Alisisitiza kuwa haiwezekani Msajili wa Baraza kuajiriwa na baraza hilo kwa kuwa anapaswa kuwa mtumishi wa umma na nafasi ya Naibu Msajili ambaye imependekezwa asiwe mwanasheria kufutwa huku pia akikubali wanataaluma wote wenye shahada kusajiliwa kwa kupendekeza iwapo watashinda mtihani utakaotungwa na Baraza kutoka Wizarani.