“KUANZIA sasa nitakuwa najifungua kwa njia ya ‘operesheni’ tu, nimeteseka vya kutosha na nisingependa kurudia mateso yale,” anasema Martha (siyo jina lake halisi), mama wa mtoto mmoja.
Anajutia mateso aliyoyapata wakati wa kujifungua ambapo alikaa na uchungu zaidi ya saa 18 pasipo kujifungua jambo lililomlazimu daktari kuamua kumfanyia upasuaji wa uzazi na kujifungua mtoto wa kiume salama.
Kwa Martha, maumivu ya uchungu ni sababu tosha ya kuchagua upasuaji kama njia ya kujifungua siku za mbeleni.
Martha ni miongoni mwa wanawake wanaoamua kujifungua kwa njia ya upasuaji nje ya sababu za kitabibu.
Idadi hii imekuwa ikongezeka siku hadi siku na kuibua mjadala mkubwa juu ya ulazima na uhalali wa ongezeko hili na kuleta mkanganyiko miongoni mwa jamii.
Kujifungua kwa njia ya upasuaji ni aina ya uzazi ambapo humlazimu daktari kumtoa mtoto kwa njia ya kupasua tumbo na mfuko wa kizazi.
Uzazi wa njia ya upasuaji una historia ndefu duniani, historia hiyo inarudi nyuma miaka mingi Kabla ya Kristo.
Pia kuna ushahidi kuwa njia hii ilikuwa inatumika na jamii za Afrika hata kabla ya ukoloni.
R. Felkrin, daktari wa kimisionari anaandika na kushuhudia kufanyika aina hii ya uzazi huko Kahura, Uganda miaka ya 1897.
Kwa mujibu wa muongozo wa tiba unaoratibiwa na Wizara ya Afya Tanzania, sababu zinazomlazimisha daktari kutumia njia hii ya uzazi wa upasuaji ni sababu ambazo zinamweka aidha mama au mtoto au wote kwa pamoja katika hatari ya kupoteza maisha.
Baadhi ya sababu hizo ni pamoja na mtoto kuwa mkubwa kuliko njia ya uzazi, mtoto kukaa vibaya katika njia ya uzazi, mama kuwa na baadhi ya magonjwa ya moyo na kadhalika.
Pia kutokana na kukua kwa teknolojia na haki za mgonjwa katika tiba, wanawake wajawazito huweza kuchagua kujifungulia kwa njia ya upasuaji pasipo kuwa na sababu yoyote ya kitiba.
Kulingana na takwimu zilizofanyiwa utafiti katika hospitali ya rufaa KCMC ya Moshi, na kuchapishwa kwenye jarida la kitabibu la Open Journal of Obstectrics and Gynecology, zinaonyesha ongezeko la idadi ya uzazi wa upasuaji kutoka 984 mwaka 2005 mpaka 1,121 mwaka 2010.
Ila takwimu hizi zikiangaliwa kwa namna nyingine zinaleta picha tofauti. Wakati mwaka 2005 idadi ya 984 ya upasuaji ilikuwa ni sawa na asilimia 39.5 ya vizazi vyote, kwa mwaka 2010 idadi ya upasuaji 1,121 ilikuwa sawa na asilimia 28.5 tu ya vizazi vyote.
Kwahiyo, pamoja na kuongezeka idadi ya upasuaji, asilimia ya uzazi wa upasuaji ukilinganisha na uzazi wa njia ya kawaida ilikuwa ikipungua.
Kuna baadhi ya madhara anayoweza kupata mama pindi anapoamua kujifungua kwa njia ya upasuaji. Mosi, kuna uwezekano wa kupata madhara kutokana na dawa ya usingizi inayotumiwa wakati wa upasuaji. Pili ni makovu yanayoachwa kwenye kizazi na baada ya operesheni. Tatu, utokaji wa maziwa baada ya kujifungua huweza kuchelewa ukilinganisha na mama anayejifungua kwa njia ya kawaida.
Lakini pia tafiti za kisayanasi zinaonyesha uwiano kati ya ongezeko la uzazi kwa njia ya upasuaji na kupungua kwa vifo vya mama na mtoto wakati wa kujifungua.
Kutokana na hili serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Afya inahakikisha upatikanaji wa huduma hii ya upasuaji mpaka kwenye vituo vya afya na pia kuongeza idadi ya madaktari wenye ujuzi wa kufanya aina hiyo ya upasuaji.
Watumishi wa afya wanasemaje?
Dk. Patrick Kazinja wa Muhimbili anadokeza, “Njia ya upasuaji ndio njia salama ya uzazi kuliko njia ya kawaida.”
Anafafanua kuwa ni kwa sababu hii ndio maana madaktari wengi huamua kutumia njia hii ili kuhakikisha usalama wa kuzaliwa kwa mtoto pindi tu wanapohisi tatizo lolote.
Hali ikoje kwenye vituo vya afya binafsi na mijini?
Vituo vya afya binafsi vimekuwa vikilalamikiwa na wananchi kuwa vimekuwa vikiwalazimisha wamama kujifungua kwa operesheni hata kama hakuna ulazima huo.
Hii imekuwa ikitumika kama njia ya kujiongezea kipato zaidi maana kujifungua kwa operesheni ni ghali zaidi kwenye hospitali binafsi ukilinganisha na kujifungua kwa njia ya kawaida.
“Kujifungua kwa njia ya upasuaji ni Shs. 500,000 kwa uchache, ila kwa njia ya kawaida ni chini ya Shs. 100,000 kwenye kituo chetu hapa,” anasema muuguzi Peter wa hospitali binafsi katikati ya Jiji la Dar es Salaam.
“Daktari hulipwa zaidi akifanya uzazi wa upasuaji kuliko akisimamia uzazi wa njia ya kawaida na zaidi ya asilimia 70 ya wanawake wanaojifungua hapa hujifungua kwa njia ya upasuaji,” anaongeza.
Uchunguzi wa FikraPevu unaonyesha kasi ya ongezeko la uzazi kwa njia ya upasuaji ni suala la linaloonekana Afrika nzima kama njia ya kupunguza vifo vya akina mama na watoto wakati wa uzazi.
Lakini uzazi wa upasuaji usio wa lazima kitabibu upo sana kwenye hospitali binafsi kuliko hospitali za serikali kwa sababu za kiuchumi.