SERIKALI ya awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli, imethubutu kwa dhati kupambana na biashara haramu ya dawa za kulevya.
Uthubutu huo unatokana na kuweka majina ya “vigogo” wa siasa, biashara, dini na muziki. Hawa mbali ya kutajwa, pia waliamuriwa kufika Kituo Kikuu cha Polisi Kanda ya Dar es Salaam kwa kuhojiwa.
Baadhi yao walipandishwa kizimbani na sasa bado wanaendelea na mashitaka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.
FikraPevu inatambua kwamba, wakati operesheni hiyo ikianzishwa, Jeshi la Polisi kupitia Kitengo cha Kudhibiti Dawa za Kulevya pamoja na Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya wamekuwa wakiendelea na operesheni zao za kila siku ambapo katika kipindi cha Januari hadi kufikia Februari 17, 2017 walikuwa wamekamata kete 328 za dawa aina ya heroin pamoja na kuteketeza ekari 93 za mashamba ya bhangi katika mikoa 15 walikofanya operesheni.
Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa (kulia) akiwachekesha jambo Rais Mstaafu wa awamu ya pili, Ally Hassan Mwinyi, Rais John Pombe Magufuli na Rais mstaafu wa awamu ya nne Dkt. Jakaya Kikwete.
Akitoa tathmini ya operesheni hiyo, Kamishina wa Operesheni ya Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya, Mihayo Msikhera, alisema mbali ya kuwakamata watuhumiwa wengi, lakini pia waliwakamata watumishi wawili wa serikali kwa kuingiza nchini kemikali inayotumika kutengenezea dawa za kulevya.
Kitendo cha serikali kuamua kuwakamata vigogo mbalimbali kufuatia orodha ya watu 95 wanaodaiwa kujihusisha na biashara hiyo haramu kimekuja baada ya ukimya wa muda mrefu, licha ya kuwepo kwa taarifa nyingi, zikiwemo za wafungwa wa Kitanzania wanaotumikia vifungo mbalimbali huko Hong Kong na China, ambao kwa nyakati tofauti wamekuwa wakiandika barua kuwataja wahusika wakuu, ambao miongoni mwao wamo wanasiasa, wafanyabiashara na viongozi wa dini.
Uwajibikaji umeimarika
FikraPevu inaona kwamba, hatua ya sasa ya serikali ni mwendelezo wa kutekeleza kwa vitendo bila woga ahadi zake kama inavyofanya katika kupambana na rushwa na ufisadi pamoja na uzembe, ambapo imeweza kuleta mabadiliko makubwa ya utendaji na nidhamu kwa watumishi wa umma.
Katika kipindi cha mwaka mmoja tangu aingie madarakani, Rais Magufuli ameweza kuwafichua na kuwawajibisha watendaji wa serikali ambao kwa namna moja ama nyingine wamehusika na uzembe, ufisadi na rushwa, ambapo wengine kesi zao zinaendelea katika mahakama za sheria.
Rais Magufuli alipozuru ghafla bandarini wiki iliyopita.
Idara mbalimbali za umma kama Mamlaka ya Mapato Tanzania – TRA, Mamlaka ya Bandari na nyinginezo zimeshuhudia vigogo wake wakiwajibishwa kwa sababu ya uzembe na ufisadi huku idara nyinginezo watumishi mbalimbali wakiendelea ‘kutumbuliwa’ katika kauli-mbiu yake ya ‘utumbuaji majipu’.
FikraPevu inaona kwamba, nidhamu sasa imeanza kuimarika, watu wanachapa kazi, vitendo vya rushwa vinaonekana kupungua na mafisadi wanaendelea kulia kwa sababu mirija yao imezibwa kama siyo kung’olewa kabisa.
Mabilioni ya Uswisi
Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo katika viwanja vya Mwembeyanga jana amewataja watanzania walioficha mabilioni ya Fedha katika Benki za nje ya nchi.
Hata hivyo, FikraPevu inaona kuwa, jitihada za sasa za serikali hazitaweza kukamilika ikiwa serikali haitageukia vigogo wengi walioficha mabilioni ya fedha ughaibuni, hususan nchini Uswisi, jukumu ambalo linamkabili Rais Magufuli.
Itakumbukwa kwamba, Ijumaa ya Mei 16, 1997 mara tu baada Laurent Desire Kabila kuipindua serikali ya Mobutu Sese Seko Kuku Ngbendu Wa Za Banga nchini Zaire, alitangaza kutaifisha mali zote za dikteta huyo aliyeitawala kwa mkono wa chuma nchi hiyo ya pili kwa ukubwa barani Afrika kwa miaka 32.
Siku moja baadaye, yaani Jumamosi Mei 17, 1997 serikali ya Uswisi nayo ikatangaza kuzuia mali za Mobutu kwa kipindi cha mwaka mmoja baada ya kupokea maelekezo kutoka kwa utawala mpya wa Kabila, ambaye wakati huo alikuwa ameweka makao yake makuu jijini Lubumbashi.
Mali zilizozuiliwa kufuatia uamuzi wa serikali ya Uswisi ni pamoja na hekalu lake lenye vyumba 300 lililokuwa eneo la Savigny pembezoni mwa ziwa huko Lausanne, ambalo kwa wakati huo thamani yake ilikuwa yapata Dola 5 milioni.
Hili lilikuwa miongoni mwa vitegauchumi vyake vingi tu barani Ulaya ambako ilielezwa kwamba vyote kwa pamoja vilikuwa na thamani ya takriban Dola 37 milioni kwa wakati huo.
Ingawa kulikuwa na taarifa kwamba Mobutu, ambaye jina lake la ubatizo aliitwa Joseph-Desiré Mobutu, alikuwa ameficha karibu Dola 4 bilioni, lakini serikali ya Uswisi ilichunguza katika benki zote 400 nchini humo na haikuona fedha zozote zilizowekwa kwa jina lake au jina la wanafamilia wake.
Taarifa iliyotolewa na taasisi ya Transparency International kupitia Bribe-Payers Index ilieleza kwamba, Mobutu na Mohammed Suharto wa Indonesia na Ferdinand Marcos wa Ufilipino kwa pamoja walifisidi nchi zao jumla ya Dola 50 bilioni, kiasi ambacho kwa wakati huo kilikuwa sawa na bajeti nzima ya mwaka ya misaada kutoka nchi wahisani.
Suharto alikomba takriban Dola 35 bilioni katika kipindi cha utawala wake wa miongo mitatu kabla ya kufukuzwa wakati ambapo Mobutu yeye alichota nusu ya Dola 12 bilioni za misaada ambazo zilitolewa na Shirika la Fedha Duniani (IMF) kwa kipindi chote cha utawala wake na kuifanya nchi hiyo ibaki na madeni makubwa hadi sasa.
Mobutu, ambaye alithubutu kulipa Dola 10 milioni kwa mabondia Muhammad Ali na George Foreman (Dola 5 milioni kila mmoja) ili wakapigane jijini Kinshasa Oktoba 30, 1974, hakuona shida yoyote kutumia fedha hata kwenda kufanya ‘shopping’ Ulaya na ndiye rais pekee Afrika kutumia midege mikubwa na ghali zaidi duniani, Concorde.
Mwaka 1989, Mobutu alikodi ndege ya Concorde yenye namba za usajili F-BTSD kutoka Shirika la Ndege la Ufaransa (Air France) kwa ajili ya safari ya Juni 26– Julai 5 kwenda tu kutoa hotuba kwenye Mkutano wa Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani, Julai 16 akakodi ndege hiyo kwenda Paris, Ufaransa kuhudhuria sherehe za nchi hiyo baada ya kualikwa na Rais François Mitterrand, Septemba 19 akakodi dege hilo kutoka Paris hadi mjini Gbadolite, Zaire na safari nyingine ya moja kwa moja kutoka Gbadolite hadi jijini Marseille akiwa na kwaya ya vijana wa Zaire.
Kwa kutumia fedha za Wazaire, aliamua kujenga uwanja maalum mjini Gbadolite, kaskazini mwa nchi hiyo ambako ndiko alikotokea, ili kuliwezesha dege la Concorde litue na kuruka. Uwanja huo uliokuwa kwenye kilele cha meta 460 kutoka usawa wa bahari, njia yake ya kurukia ilikuwa na urefu wa meta 3,200 (kilometa 3.2) na upana wa meta 60.
Lakini kama tulidhani zama za akina Mobutu, Suharto na akina Marcos zimekwisha, tutakuwa tunajidanganya, kwa sababu mpaka sasa bado viongozi na maofisa wa kawaida wa serikali zetu, hasa kwa nchi za dunia ya tatu kama Tanzania, wanaendelea kukomba fedha za wananchi na kuzificha ughaibuni – mara nyingi wakitumia majina ya washirika wao kwa kuhofisa yasiwapate kama yaliyowakumba wengine.
Kwa miaka kadhaa sasa, tumeelezwa kwamba wapo vigogo wengi wa Tanzania – viongozi wa serikali, wafanyabiashara na hata viongozi wa dini – ambao mbali ya kuwa na mahekalu ughaibuni, pia wameficha mabilioni huko ng’ambo.
Wapo ambao majina yao yamekuwa yakitajwa kwa minong’ono, lakini kuna wale ambao licha ya kuanikwa hadharani, baadhi yao wamewahi hata kutoa kauli za kejeli kwamba “ni vijisenti tu”, kama alivyosema Mwanasheria Mkuu wa zamani wa Serikali, Andrew Chenge, mwaka 2008 baada ya kubainika kwamba alificha karibu Dola 1 milioni huko Uingereza.
Taarifa zinasema, orodha iliyopo ni ya Watanzania walioficha zaidi ya Dola 3.5 milioni kila mmoja, ambapo inaelezwa kwamba fedha nyingi za wanasiasa zimewekwa na makampuni ya nje yenye shughuli Tanzania.
Katika majina ambayo yamekuwa yakinong’onwa, wamo vigogo waliopata kuwa mawaziri katika serikali zilizopita, lakini pia Julai 2015, Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Zuberi Kabwe, katika mkutano wake jijini Dar es Salaam, alitoa orodha ya Watanzania 99 wenye asili ya Kiasia ambao wameficha takriban Dola 114 bilioni katika benki mbalimbali nchini Uswisi.
Kisiwa Salama
Inafahamika kwamba Uswisi ni ‘kisiwa’ salama kwa watu kuficha fedha zao kutokana na mfumo na sheria za kifedha za nchi hiyo, ambapo wahusika hawaulizwi ‘maswali ya ajabu’ wanapotaka kufungua akaunti zao, hali ambayo inafanya hata fedha chafu zote zihifadhiwe huko.
Kati ya waliotajwa na Zitto, wapo wafanyabiashara ambao wametajwa katika kashfa nyingi za mikataba inayoendelea kulitafuna taifa hadi sasa, zikiwemo kashfa za ufisadi za EPA, Richmond, na mikataba ya rada, ununuzi wa ndege na magari ya jeshi na kadhalika.
Swali ni kwamba, vyombo husika vina taarifa? Kama taarifa zipo, zimefanyiwa kazi? Kama kazi imefanyika, matokeo yake yakoje? Ikiwa havina taarifa, viko hapo vinafanya nini? Kuna umuhimu wowote wa kuendelea na vyombo hivyo kama haviwezi kufuatilia hata minong’ono na kuchunguza kama minong’ono hiyo ina ukweli wowote?
Jibu ni kwamba taarifa zipo. Kama ilivyo kawaida ya nchi hii, hakuna anayejali. Lakini hapana, wanajali sana. Tatizo ni kwamba, hata huyo aliyetakiwa kushughulikia wahusika, naye ni mhusika. Hapo ndipo penye tatizo.
Julai 2012, Benki Kuu ya Tanzania kupitia kitengo chake cha Financial Intelligence Unit (FIU) ilisema kwamba imeanza kuchunguza madai ya Watanzania walioficha fedha Uswisi kama wanavyofanya wenzao wa mashirika ya kijasusi ya CIA (Marekani), MI6 (Uingereza), RAW (India) na Mossad (Israel), ambayo yamekuwa yakifuatilia nyendo za fedha haramu hasa za kighaidi dunia.
Inaelezwa kwamba, fedha nyingi kati ya hizo zilizofichwa huko zinadaiwa kutokana na biashara zilizofanywa na watendaji wa Serikali na wafanyabiashara kwenye Sekta za Nishati na Madini na kwamba sehemu kubwa ya fedha zililipwa na kampuni za utafutaji mafuta na gesi katika pwani ya Mkoa wa Mtwara zilizopewa mikataba kati ya mwaka 2004 na 2006.
Serikali ya awamu ya nne kupitia Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma mwaka 2012 ilianza kuwachunguza baadhi ya mawaziri wake pamoja na wabunge kutokokana na kujilimbikizia mali nyingi tofauti na kipato chao halali, lakini hakuna matokeo yoyote yaliyowekwa hadharani.
Fedha nyingi hutoroshwa
Ripoti ya Global Financial Integrity (GFI) ya mwaka 2008 ilionyesha kwamba kumekuwa na ongezeko la kiasi cha fedha kinachotoroshwa katika nchi mbalimbali duniani kutoka dola za Marekani 1.06 trilioni za mwaka 2006 hadi kukaribia dola 1.26 trilioni za mwaka 2008.
Katika kiasi hicho cha fedha, wastani wa dola 725 bilioni hadi 810 bilioni zilitoroshwa kwa mwaka tangu mwaka 2000 hadi 2008 kutoka katika nchi zinazoendelea.
Ripoti hiyo inaonyesha pia kwamba, Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini, zinaongoza kwa asilimia 24.3, nchi zinazoendelea za Ulaya asilimia 23.1, Afrika asilimia 21.9 na Asia asilimia 7.85.
Katika ripoti hiyo, nchi 10 zinazoongoza duniani kwa kuwa na kiwango kikubwa cha fedha kilichotoroshwa kati ya mwaka huo 2000 hadi 2008 na kiasi katika mabano ni China (dola 2.18trilioni), Russia (dola 427bilioni), Mexico (dola 416 bilioni), Saudi Arabia (dola 302bilioni), Malaysia (dola 291bilioni), Umoja wa Falme za Kiarabu (Emirates, dola 276 bilioni), Kuwait (dola 242bilioni), Venezuela (dola 157bilioni), Qatar (dola 138bilioni) na Nigeria (dola 130bilioni).
Benki ya Dunia (WB) ilianzisha mpango wa Stolen Asset Recovery Initiative StAR (Juhudi za Kurejesha Mali na Fedha Zilizoibwa) na kuongeza kwamba juhudi hizo zinafanya kila nchi na taasisi kama BoT kufahamu fedha za watu wake zilizofichwa nje.
Ni wakati muafaka sasa kwa serikali ya awamu hii kulivalia njuga suala la mabilioni hayo ya Uswisi, wahusika wahojiwe walivyoyapata, kama hakuna majibu ya kuridhisha, wataifishwe kwa sababu huo ni uhujumu uchumi.