WALINZI wawili wa kampuni ya Cob Web Security Ltd wamelazwa katika Hospitali Teule ya Wilaya ya Sengerema Mkoani hapa, huku mmoja wao akiwa mahututi baada ya kupigwa na askari Polisi akidhaniwa kuwa jambazi.
Chanzo cha habari kutoka hospitalini hapo kimemtonya mwandshi wa habari hizi kwa sharti la kutotajwa jina gazetini kwamba walinzi hao walijeruhiwa usiku wa kuamkia Mei 31 mwaka huu, wakati wakiwa kazini katika mtaa wa Misheni mjini humo.
Walinzi hao wametajwa kuwa Zunya Kaswahili pamoja na Paul Damas, wote wakazi wa mjini Sengerema.
Habari hizo ambazo pia zimethibitishwa na mmoja wa walinzi hao zinadai wamelazwa katika wodi namba mbili(wanaume) kutokana na majereha pamoja na maumivu makali mwilini.
Inadaiwa kwamba walinzi hao walijeruhiwa kufuatia tukio la ujambazi katika mtaa wa Misheni ambapo mali kadhaa ziliporwa madukani.
” Kwa kweli hali ya Zunya siyo nzuri kwa sababu mbali na kujeruhiwa na majambazi, pia alipigwa na askari polisi waliofika eneo la tukio baada ya kupokea taarifa za ujambazi” kilidai chanzo cha habari.
Inadaiwa kwamba katika malindo tofauti walinzi hao walipigwa hadi Zunya alivuliwa sare kabla kuachwa huku akiwa amepoteza fahamu .
” Askari walipofika eneo la tukio walimkuta Zunya akiwa amelala chini na ndipo walipoanza kumpiga wakidhani kuwa ni miongoni mwa majambazi yaliyokimbia” alisema mmoja wa walinzi hao kwa njia ya simu, Paul Damas wakati akiendelea kupatiwa matibabu.
Alisema yeye amepoteza simu yake ya mkononi na kuongeza kuwa wakati wa purukushani baina yao na majambazi, mlinzi mwenzao mmoja alifanikiwa kutoroka wakati akwa na bunduki .
Alifafanua pia kwamba majmbazi hayo yalifanikiwa kupora simu kwenye duka linalomilikiwa na Simon Chai.
Majeruhi huyo alisema tukio hilo lilitokea majira ya saa 7 usiku na kwamba hadi anakimbizwa hospitali hakuna mtu yeyote ambayo alikuwa ametiwa mbaroni kuhusiana na ujambazi huo.
Alifafanua kuwa amejeruhiwa kwa mapanga kichwani na kwamba hali yake ilikuwa ikiendelea vizuri.
” Zunya amejeruhiwa vibaya shingoni, hasa kwenye mishipa ya damu” alisema mmoja wa wahudumu waliokuwa zamu, kwa sharti la kutotajwa jina kwa vile siyo msemaji wa hospitali hiyo.
Hadi tunakwenda mitamboni, Meneja wa Cob Web Security Ltd, Tumain Mahinduka pamoja na Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani hapa, Simon Sirro, hawakupatikana kwa njia ya simu ili waweze kutoa ufafanuzi juu ya tukio hilo.
Simu ya Sirro iliita bila kupokelewa ambapo simu ya Mahinduka haikuwa hewani.
Na. Juma Ng’oko (Mwanza)